Friday, 5 February 2016

SALIM MSOMA AKIELEZA ZNP, ZPPP, ASP NA TANU KATIKA SIASA ZA ZANZIBAR MIAKA YA 1950/60

SALIM H. MSOMA
Salim Msoma

Utangulizi

Hapo chini ni barua niliyopokea kutoka kwa Salim Msoma akitia maoni kuhusu makala, ''Uchaguzi wa Zanzibar wa Mwaka wa 1961,'' ambamo niliweka nukuu ya Aman Thani akieleza uchaguzi uli ulivyokuwa. 

Wasiomfamahu Salim Msoma ni kuwa Msoma ni katika wasomi makini wa wakati wa mapinduzi ya Afrika. Alikuwa mwanachama wa University Students's African Revolutionary Front (USARF) chama ambacho kilianzishwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam mwaka wa 1967 na wanachama wake walikuja kuacha alama katika historia za ukombozi wa nchi zao kama John Garang na Yoweri Musevani.

Sheikh Mohamed Said,

Ahsante kwa kutuletea maandishi haya ambayo yanatukumbusha historia ya karibuni ya Zanzibar.Bila shaka waraka huu umeunakili kutoka kijitabu alokiandika mzee wetu Bw Amani Thani Fairuz miaka kadha iliyopita na ambacho binafsi nilibahatika kukisoma.Mimi naomba nitoe maoni ya mawili matatu kuhusu maelezo ya Mzee Amani Thani.

Kwanza nakubaliana nawe kuwa yapo ya kujifunza katika kadhia ya uchaguzi wa Januari na June 1961 Zanzibar khasa tukitilia maanani hali ya kisiasa ilivyo hii leo visiwani.Lakini ninalotaka kuchangia mimi ni kwamba maelezo ya Mzee Fairuz kama yalivyo maandishi mengine kuhusu mada hii niliyoyasoma yanakuwa na upungufu mmoja. Nao ni tabia ya kuelezea matukio (facts) bila ya kujadili kwa upana na kutafsiri yaliyo nyuma ya matukio hayo yaani muktadha wake. (broad discussion of related issues surrounding the narrated events).Kwa mfano unapozungumzia suala la kuwepo VITI katika majimbo ya uchaguzi vilivyokuwa vinagombewa na kueleza matokeo ya chama kile kilipata viti kadhaa na kingine kikapata viti zaidi na kushinda bila ya pia kuonyesha TAKWIMU za kura zilizopigwa hakutowi picha sahihi kwa wasomaji kuhusu mfumo mzima wa chaguzi zile. Hivi leo waandishi mbalimbali wanaeleza na kuonyesha jinsi ukataji wa majimbo (constituencies) ulivyokuwa wa mashaka na hila. Imebainika majimbo yaliyokuwa na wafuasi wengi wa ASP yalitengewa viti vichache wakati majimbo yalokuwa na watu kidogo wa ZNP yalipewa viti vingi. Ujanja huu ambao Waingereza wanauwita 'gerrymandering' ndio hatimae uliwapokonya ushindi halali ASP na kutulea mabalaa na maafa visiwani. Wasomaji lazima waelimishwe kuwa miongoni mwa sababu za kufanyika Mapinduzi Zanzibar ni hili la kunyimwa kwa hila na ujanja haki yao ASP ya kuunda na kuongoza serikali.

Jengine ninalotaka kulieleza kwa mnasaba huu huu wa kujadili mambo badala ya kuyataja tu kijuu juu ni kitendo cha Sheikh Mohamedd Shamte kujitoa ASP mwaka 1960. Bw Fairuz ameeleza haelewi sababu za Mzee Shamte kujitoa ASP. Lakini kadri ya muda ulivyopita imebainika wazi kuwa ZPPP kilikuwa ni chama kilichotokana na tawi lililokuwa la Shirazi Association huko Pemba. Mara zote imekuwa ikitolewa picha potofu kuwa Waswahili wa Zanzibar waliojitambulisha kwa jina la Shirazi Association walikuwa ni kitu kimoja (homogeneous). Kumbe hali ni tofauti kabisa. Washirazi wa Pemba na hata baadhi ya wale wa Unguza wamekuwa wakati wakiwemo ndani ya chama cha ASP wakipinga kile walichokihisi ujenzi wa uhusiano wa karibu kati ya ASP na TANU. Shamte aliwakilisha hisia hizo na alikuwa hamuamini kabisa Julius Kambarage Nyerere kinyume na alivyokuwa Mzee Karume. Na Mzee Shamte alipohisi huu usuhuba wa Nyerere na Karume unazidi kushamiri ndipo akagombana na Mzee Karume na kuamua kujitoa ASP. Lakini kuna jambo jengine ambalo ZNP hawakupenda kuliongea. Nalo ni kwamba huyu Mzee Shamte hapo mwanzoni alikuwa hawaamini pia Waarabu! Inaelezwa kuwa katika mwaka ule (1959) ambao Mzee Karume kwa shinikizo la PAFMECA alianza kuhutubia mikutano kupitia jukwaa moja na Sheikh Ali Muhsin, Shamte alikuwa ni ‘’diehard,’’ mmoja wapo aliekasirishwa ndani ya ASP. Cha kustaajabisha ni kumuona mtu yule yule alokuwa akipinga kumuona Karume akiwa pamoja na Ali Muhsin alikuja baadae kuunda Umoja na huyohuyo Ali Muhsin kuanzia uchaguzi wa 1961 na hatimae akapewa Uwaziri Mkuu ndani ya Serikali ya Uhuru 1963! Haya ndio mambo ambayo waandishi kama Bw Fairuz wanapaswa kuyasema kwa uwazi zaidi.  Wasalam.   
Post a Comment