Friday, 18 November 2016

KUTOKA JF:KUNA UHUSIANO WOWOTE KATI YA UONGOZI WA JUU TANZANIA NA VATICAN RUMI?
Britanicca,
Unauliza kuhusu uhusiano wa Vatican na nafasi ya Urais katika Tanzania.

Nakuwekea jibu hapo chini ni ''document,'' ya utafiti ya maneno 19,000+
kwa hiyo litahitaji muda mtu kusoma:

Mohamed Said: MWL. JULIUS K. NYERERE, KANISA KATOLIKI NA UISLAM: DOLA NA TATIZO LA UDINI TANZANIA

Hapo chini nakuwekea, ''excerpts,'' kwa kusoma mswada mzima fungua hapo juu:
MWL. JULIUS K. NYERERE, KANISA KATOLIKI NA UISLAM: DOLA NA TATIZO LA UDINI TANZANIA

Utangulizi

Baada ya kifo cha Julus Kambarage Nyerere tarehe 14 Oktoba 1999 mengi yamesemwa na kuandikwa kuhusu msimamo wake na uadilifu kuhusu Uislam Tanzania. Nia ya kitabu hiki ni kueleza jinsi Mwalimu Nyerere katika kipindi chake cha uongozi alivyoshughulikia suala la Uislam na Waislam wa Tanzania. Hii ni historia ya uhusiano wa Mwalimu Nyerere na Waislam kwa kipindi cha takriban robo karne toka pale aliposhika madaraka ya nchi mwaka 1961 hadi alipoachia madaraka mwaka 1985. Ni mategemeo ya mwandishi kuwa kitabu hiki kidogo kitaweka wazi yale ambayo hayafahamiki kwa wengi.

Theluthi mbili ya Waislam wote wa Afrika ya Mashariki wanaishi Tanzania [2] ambayo ndiyo nchi yenye watu wengi kuliko zote katika Afrika ya Mashariki, yaani Kenya, Uganda na Tanzania. Hii ni pamoja na Zanzibar – nchi ya Kiislam yenye Waislam takriban asilimia tisini na tisa na kuna wakati ilikuwa ndiyo kitovu cha maarifa ya Kiislam katika Afrika ya Mashariki na Kati. Kutokana na sensa ya mwaka 1957, kwa kila Waislam watatu walikuwepo Wakristo wawili. Kwa wakati ule hii ilionyesha kuwa Tanganyika ilikuwa na Waislam wengi katika nchi zote Kusini ya Ikweta. Lakini katika sensa ya kwanza mwaka 1967 baada ya uhuru jumla ya Wakristo Tanzania Bara ilikuwa asilimia thelathini na mbili na Waislam asilimia thelathini na Wapagani asilimia thelathini na saba. Sensa hii inaonyesha kuwa Wapagani ndiyo walio wengi Tanzania. Sensa hii ya mwaka 1967 haikueleza kwa nini katika kipindi cha miaka kumi kwa ghafla Waislam wamepungua nchini au kwa nini ghafla Wapagani wameongozeka katika nchi ya waumini. Hii ndiyo ilikuwa sensa ya mwisho iliyokuwa ikionyesha mgawanyo wa dini. Inaaminika kuwa matokeo ya sensa hii yalifanyiwa mabadiliko kwa ajili ya sababu za kisiasa pale ilipobainika kuwa Waislam Tanzania walikuwa wengi kupita Wakristo. Upo ushahidi kuwa mwaka 1970, ilipobainika kuwa Waislam ni wengi Tanzania serikali iliiamrisha Idara ya Takwimu kuchoma moto matokeo yote ya sensa ya mwaka 1970.[3]

Bahati mbaya mgao wa madaraka katika siasa Tanzania umewatupa nje Waislam, ingawa inafahamika kuwa usalama na utulivu wa nchi yeyote unategemea mizani hii kuwa sawa. Vyanzo tofauti vya takwimu vinatoa takwimu tofauti zinazopingana kuhusu hesabu ya Waislam na Wakristo katika Tanzania. Hii inatokana na ukweli kuwa somo hili ni nyeti. Katika nchi za Kiafrika ambazo zina wafuasi wengi wa dini hizi mbili, kwa mfano Tanzania na Nigeria,[4]uchunguzi wa kuwa ni dini gani ina wafuasi wengi kupita mwenzake ni chanzo cha mgongano na mzozo. Tatizo hili lipo Tanzania. D.B. Barret [5] anasema kuwa Waislam Tanzania ni wachache wakilinganishwa na Wakristo. Takwimu zake zinaeleza kuwa Waislam ni 26%, Wakristo 45% na Wapagani ni 28%. Takwimu za Tanzania National Demographic Survey za mwaka wa 1973 zinaonyesha kuwa Waislam ni wengi kidogo kupita Wakristo wakiwa 40%, Wakristo 38.9% na Wapagani 21.1%. Lakini takwimu za Africa South of the Sahara,[6] zinaonyesha Waislam ni wengi Tanzania kwa 60%. Takwimu hizi zimebaki hivyo bila ya mabadiliko toka mwaka 1982. Kwa kuwa utafiti wa Waislam wenyewe katika suala hili ni mdogo sana au haupo kabisa, suala la wingi wa Waislam katika Tanzania halijafanyiwa utafiti na Waislam wenyewe.[7]

Mkristo akawa ananufaika na mfumo wa kikoloni. Waislam wakawa wanataabika kwa kuwa dini yao ilikuwa inapingana na dini ya mtawala. Mwafrika Mkristo akawa mnyeyekevu kwa serikali wakati wa ukoloni na baada ya kupatikana kwa uhuru akaja kushika madaraka ya serikali. Waislam wakatengwa na kuteswa katika ukoloni kwa kubaguliwa na kunyimwa elimu hivyo kuwaondolea fursa ya maendeleo. Kuwepo kwa Waislam kama raia na ili kuinusuru dini yao ilibidi Waislam wasimame kuutokomeza ukoloni. Baada ya uhuru Kanisa likabaki na msimamo wake wa enzi ya ukoloni wa kutii na kujipendekeza kwa serikali mpya iliyokuwa madarakani. Ushirika huu kati ya Kanisa na serikali, uliojengwa na tabia ya Kanisa ya kukubaliana na mfumo wowote wa serikali ulililelewa vyema na umeisaidia sana Kanisa. Kanisa likaweza kujijengea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zake bila ya kipingamizi wala wasiwasi. Kutokana na uhusiano huu maalum Kanisa likajifanyia msingi imara wenye nguvu kutokana wa Wakristo waliowasomesha katika shule zao. Kanisa likatumia nafasi na uhusiano huu kwanza na serikali ya kikoloni kisha na serikali ya wananchi kujijengea himaya ambayo wafuasi wake wakaja kushika nafasi zote muhimu katika uongozi wa juu wa serikali, bunge na mahakama katika Tanzania. Katika miaka yake mia moja tu Kanisa likaweza kupata safu yake ya viongozi ambao wanadhibiti kila sekta katika jamii ya Watanzania.

Kanisa Katoliki ambalo ndilo lenye nguvu zaidi, lilikuwa tayari limeshajikita Tanganyika. White Fathers walikuwa wapo Tabora, Karema, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Bukoba; Holy Ghost Fathers walikuwa Morogoro na Kilimanjaro; Benedictine Fathers walikwepo Peramiho na Ndanda; Capuchin Fathers walikuwepo Dar es Salaam; Consolata Fathers walikuwepo Iringa na Meru; Passionist Fathers walikuwa Dodoma; Pallotine Fathers walikuwa Mbulu; Maryknoll Fathers walikuwapo Musoma; na Rosmillian Fathers walikuwa Iringa. [8]

Haiwezekani kuielewa ahadi ya Nyerere katika haki na usawa kwa raia wote kama alivyoahidi wakati wa kudai uhuru, hadi usome hotuba yake aliyoitoa tarehe 10 Desemba, 1962 katika Bunge wakati Tanganyika inakua jamuhuri. Hotuba ya Nyerere ilijikita kwenye matatizo ya upogo kati ya Waislam na Wakristo. Nyerere alifanya hivi labda akijua kuwa ingawa yeye alikuwa Rais Mkatoliki lakini waliomuweka madarakani kuitawala Tanganyika walikuwa Waislam. Nyerere alikuwa na haya ya kusema:

''Hakuna njia nyepesi ya kuondoa tafauti baina ya raia wetu Waafrika na wasio Waafrika; hakuna njia nyepesi ya kuondoa tofauti za elimu kati ya Wakristo na Waislam, au baina ya wachache wenye elimu na wengi wa watu wetu wasio kuwa na elimu; hakuna njia nyepesi ambayo Wamasai na Wagogo wanaweza wakalingana na Wahaya na Wachagga na Wanyakyusa.''[24]

Hii ilikuwa kauli ya serikali ya kudhihirisha nia yake njema. Kauli hii ilikuwa ya kuwapa matumaini na kuwahakikishia Waislam na wale wote walioathirika na dhulma ya wakoloni, kuwa serikali ilikuwa inatambua shida zao na itachukua hatua zifaazo kurekebisha hali hiyo. Wakati Nyerere anatoa kauli hii ya kutia moyo, serikali iliyokuwa imejaa viongozi wa Kikristo na taasisi za Kikristo zilikuwa imejaa hofu wakiogopa harakati za Waislam za kujiletea maendeleo zilizokuwa zinatapakaa nchi nzima kwa kasi. Walifahamu fika nguvu na umoja wa Waislam ukitumiwa vyema hapana shaka Waislam watakuja juu. Kwa viongozi wa Kikristo waliokuwa wameshika madaraka ya serikali hii ilimaananisha kugawana madaraka sawa na Waislam, kwao wao harakati hizi mpya ziliashiria kuanguka kwa himaya yao katika madaraka kama viongozi.

Sura ya Tatu

Kusalitiwa kwa Maadili

Tarehe 5 Novemba, 1985 kabla hajastaafu urais, Nyerere aliwahutubia wazee wa Dar es Salaam. Hotuba hii ilijaa simanzi, Nyerere akikumbuka jinsi Waislam walivyompokea Dar es Salaam kwa mapenzi makubwa ingawa yeye alikuwa Mkristo. Wazee hawa wengi wao walikuwa wanachama wa zamani wa TANU waliomuunga mkono Nyerere wakati wa kudai uhuru. Nyerere aliusifia mchango wa Waislam katika kipindi kile kigumu cha kudai uhuru. Nyerere alisema kuwa upogo katika elimu uliorithiwa na serikali yake kutoka kwa Waingereza baina ya Waislam na Wakristo yeye ameuondosha katika kipindi cha utawala wake:

''Waislam wametupa nafasi kupitia sera yetu ya elimu, kurekebisha upogo. Sasa nipo katika hali ya kufarahisha kwa kuwa wakati mwingine sielewi kama Mbunge mpya, Waziri, au Katibu Mkuu katika wizara zetu za serikali, ni Muislam au Mkristo au hana dini labda pale jina lake la kwanza linapotoa utambulisho. Na hata hivyo hiyo siyo njia ya kuaminika kutoa utambulisho wa dini kwa kuwa tuna Wakristo wenye majina ya Kiislam, na Waislam wenye majina ya Kikristo. Kuvumiliana huku nyie ndiyo sababu; nilichofanya mimi ni kuzungumzia maadili haya kwa niaba yenu.''[79]

Hotuba hii ilikuwa ya ulaghai. Ukweli ni kuwa miongo mitatu baada ya uhuru Waislam hawajanufaika chochote wako katika hali ile ile aliyowaacha wakoloni au mbaya zaidi. Sivalon amefichua kuwa Kanisa limeweza kujenga himaya yake ambayo inahodhi asilimia sabini na tano za viti katika Bunge la Tanzania. Kati ya viti hivyo asilimia sabini vipo mikononi mwa Wakatoliki na vilivyobaki vimegawika kati ya Waislam na Wakristo wa madhehebu nyingine.[80]Baada ya kupatikana uhuru, Kanisa lilipohisi wasiwasi, limeweza kwa urahisi kabisa kuwazuia na kuwadhibiti Waislam. Serikali imeweza kutumia nguvu iliyokuwanayo katika kudhibiti siasa kuzuia harakati za Waislam kudai fursa sawa na Wakristo katika kugawana madaraka katika serikali. Kanisa limehakikisha kuwa kupinduliwa kwa ukoloni si kizingiti kwa Ukristo, ingawa ingetegemewa kuwa Kanisa lingedhirika kwa kuanguka kwa ukoloni. Katika miaka yake zaidi ya mia moja, Kanisa lilikuwa limestarehe kama muokozi wa nafsi na watu wenyewe. Kanisa lilikuwa salama na halikupambana na msukosuko wowote kutoka kwa serikali kwa kuwa lilikuwa Kanisa ndilo lilishika hatamu ya serikali.

Hivi sasa Waislam wanamshutumu Mwalimu Nyerere na uongozi wa Kanisa kwa kusaliti dhamana aliyokabidhiwa na Waislam ambao ndiyo waliopigania uhuru wa Tanganyika. Waislam wa Tanzania hivi sasa ni kama wanazaliwa upya. Kila kukicha wanatafakari hali yao na jinsi historia yao ilivyokuwa ya kishujaa na ya kupendeza kwa namna walivyopambana na wakoloni, kuanzia vita vya Maji Maji mwaka 1905 hadi kuanzishwa kwa African Associatioin mwaka 1929 na TANU mwaka 1954; hadi uhuru ukapatikana mwaka 1961. Waislam wanaamini kuwa baadhi ya majibu ya matatizo yanayowakabili hivi sasa yapo kwenye hii historia yao ya kudai uhuru.

[1] A.A. Ahmed, ‘Lamu’s Sacred Meadows’, Fountain, April-June, 1995 Vol. 2 No. 10, p.30.
[2] August H. Nimtz Jr, Islam and Politics in East Africa, University of Minneapolis, 1980, p.11.
[3] See Family Mirror, Second Issue, November 1994, uk. 6.
[4] Ali A. Mazrui, ‘African Islam and Competitive Religion: Between Revivalism and Expansion’, in Third World Quarterly Vol. 10. No. 2 April 1988, uk. 499-518.
[5] D.B. Barret, Frontier Situations for Evangilisation in Africa, Nairobi, 1976. 
[6] Africa South of the Sahara, Europa Publication, London, No. 20, 1991, uk. 1027.
[7] Utafiti wa kuaminika kidogo ni ule uliofanywa na Dar es Salaam University Muslim Trustee (DUMT), Angalia ‘The Position of Muslims and Islam in Tanzania’, katika Al Haq International, (Karachi) September/October 1992.
[8] Angalia Kiongozi No. 6 June 1950. Kwa maelezo zaidi kuhusu kueneza kwa wamisionari Afrika ya Mashariki, angalia M. Langley & T. Kiggins: A Serving People, Oxford University Press, Nairobi, 1974, uk. 19.
[9] Mengi kuhusu kuingia kwa wamishionari wa mwanzo mwandishi ameandika kwa msaada wa Dr. Hamza Njozi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.
[10] C.D. Kittler, The White Fathers, London 1959, uk. 22-23 vilevile  R. Clarke (ed) Cardinal Lavigerie and Slavery in Africa uk. 302.
[11] Angalia  ‘Proceedings of CMS 1880-8’, uk. .22-23.
[12] Angalia I.N. Kimambo,  na A.J.A. Temu, History of Tanzania, EAPH, Nairobi, 1969 uk. 126.
[13] Katika kuuhisha vita dhidi ya Uislam serikali ya Tanzania mwaka wa 1993 ilitiliana sahihi mkataba na makanisa, mkataba uliokuja kujulikana kama Memorandum of Understanding makubaliano ambayo yalikuwa serikali kuidhinisha elimu, huduma za jamii na afya ziendeshwe na Christian Council of Tanzania (CCT) and Tanzania Episcopal Conference (TEC) kwa kushirikiana na serikali. Mkataba huu ulitayarishwa kwa siri  na Dr. Costa Mahalu, wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na ukatiwa sahihi na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Mkataba huu ulitiwa sahihi bila ya kuwashirikisha  au kuwafahamisha Waislam. Ili makubaliano haya  yaweze  kutekelezeka, serikali ilibidi ifanye marekebisho kifungu 30 cha  Education Act No. 25, 1978.

[14] H.B Hansen, Mission, Church and State in Colonial Setting: Uganda 1890-1925, London 1984, uk. 26, vilevile angalia Ali M. Kirunda, “Uganda Muslims and their problems,” The Monitor June 4-June 8, 1993.
[15] Abel Ishuwi, Education and Social Change, (1980).

[16] Angalia P. Gerold Rupper, OSB, Pugu Hadi Peramiho: Miaka 100 ya Wamisionari Wabenediktini Katika Tanzania, Benedictine Publications, Ndanda-Peramiho, 1980, uk. 31-42.
[17] Angalia Yusuf Halimoja, Historia ya Masasi, East African Literature Bureau, Nairobi, uk. 163-175. Kwa kupata habari zaidi jinsi Wakristo walivyopigana upande wa Wajerumani katika Vita ya Maji Maji ili kulinda Ukristo dhidi ya kile kilichoonekana kuwa ni jihad, angalia Nimitz, op.cit. uk.12-13. 
[18] C.H. Becker, ‘Material for the Understanding Islam in German East Africa’, Tanzania Notes and Records, No. 68, 1968, p. 58.
[19] Al Jamiatul  Islamiyya ‘A’ iliundwa mwaka 1940 kutokana na mgogoro ulioanzishwa na Liwali wa Dar es Salaam wakati ule, Ahmed Saleh akishirikiana na Waingereza.
[20] Congress ilikuwa imegubikwa na matatizo ya ugomvi kati ya viongozi wake. Angalia Reporter (Nairobi), March – June, 1963. AMNUT ilikuwa katika siku zake za mwisho lakini ilikuwepo tamaa kuwa huenda kikapata nguvu mpya. Kassanga Tumbo aliyekuwa katibu wa TRAU ambae Nyerere alimteua balozi Uingereza, alikuwa amejiuzulu ubalozi akarudi Tanganyika na kuanzisha chama cha upinzani, Tanganyika Democratic Party. (TDP). Kulikuwa na mazungumzo ya kuunganisha TDP na AMNUT. Nyerere alifahamu kuwa endapo Waislam watamuunga mkono Tumbo utawala wake ungekuwa mashakani.Inasemekana kuwa nafasi ilie ya ubalozi Uingereza awali Nyerere alimpa Hamza Mwapachu. Mwapachu aliikataa kwa kuwa alihisi hiyo ilikuwa njama ya Nyerere kumeweka mbali na siasa nchini. Ilikuwa matumaini ya Mwapachu kuwa Nyerere angelimpa uwaziri ili achangie pamoja nae katika kuijenga nchi.
[21] Tanganyika Standard, 2 May, 1961. 
[22] Kilichofuata baada ya kupatikana uhuru ilikuwa ni kukamatwa, kuwekwa kizuizini na kuhamishwa kwa masheikh na Waislam wengine waliodhaniwa kuwa wanapinga utawala wa Nyerere. Mashuhuri miongoni mwao walikuwa: Abdillah Schneider Plantan, Sheikh Abdulkarim Abdulwahid, Maalim Popo Saleh, Suleiman Masudi Mnonji, Ali Migeyo, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Sharff Hussein Badawiy, Shariff Mwinyibaba, Shariff Adnan, Bilali Rehani Waikela, Sheikh Jumanne Bias, Maalim Matar, Abdalah Mwamba, Sheikh Hashim Haji Abdallah, Sheikh Nurdin Hussein, Salum Abdallah Popo, Sheikh Mzee Ali Comoriam, Sheikh Al Amin Maftah, Rajab Kiguu cha Mbuzi na wengine wengi.
[23] Tanganyika Standard, 15 April, 1961. Kwa hoja kama hiyo angalia vilevile John Hatch, Two African Statesmen, London, 1976, uk.128.
[24] Press Release B/1629/62 10th December, 1962.
[25] Tanganyika Standard, 12 th March, 1963.  
[26] K. Mayanja Kiwanuka, op. cit. uk. 57-58.
[27] Report ya East African Muslim Welfare Society, January/February 1961. 

[28] Kwa maelezo kamili ya mgogoro wa Waislam wa mwaka 1968, angalia M. Said, ‘Islam and Politics in Tanzania’, op. cit. Vilevile angalia ‘Kwikima Report’ katika The Standard, 12 th December, 1968, na katika The Nationalist, 24 th October, 1968.
[29] Mwaka wa 1963 hawa wafuatao ndiyo walikuwa viongozi wa EAMWS: Tewa Said Tewa, Aziz Khaki, Bibi Titi Mohamed, Saleh Masasi, Abdallah Jambia, Khamis Kyeyamba na Bilali Rehani Waikela.
[30] Kwa kiasi cha siku mbili Nyerere alikuwa hafahamiki yuko wapi. Wanajeshi walikuwa wakiwasiliana na Oscar Kambona kujaribu kutatua mgogoro uliokuwepo. Dossa Aziz ndiye aliyemtorosha Nyerere kutoka Ikulu akapita nae lango kuu Nyerere akiwa amejificha katika gari la taka chini ya takataka. Dossa akiwa na bunduki yake alienda na Nyerere hadi Kigamboni kwenye nyumba iliyokuwa ufukweni pwani ambayo ilikuwa ikitumiwa na Gavana kama mahali pa kupumzika. Baadae Rashid Kawawa aliyekuwa makamo wa rais alikwenda pale na wakawa pamoja na Kambona ambae alikuwa kiungo kati ya serikali na wanajeshi walioasi. Nyerere mwenyewe hajakieleza kisa hiki kwa yoyote. Baada ya kujitokeza waandishi wa habari walimuuliza alikuwa wapi wakati wote wa uasi wa wanajeshi. Nyerere kwa ukweli kabisa alijibu, ‘Nilikuwa Dar es Salaam’.
[31] Katika utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi na baada ya kupita miaka zaidi ya thelathini, amri ya kufukuzwa Sharif Hussein ilibatilishwa na akarudi Tanzania. Kwa kauli yake mwenyewe Shariff Hussein alimfahamisha mwandishi kuwa yeye wakati wa uhuru alikuwa akishiriki katika dua nyingi za kumuombea Nyerere mafanikio. Shariff Hussein akasema lakini malipo yake kutoka kwa Nyerere ilikuwa ni kumfukuza nchini. 
[32] Viongozi wa EAMWS walitishwa na makachero wa serikali watupe nyaraka na kumbukumbu zote za EAMWS au sivyo serikali itawachukulia hatua. Viongozi wengi walitishika na kuchoma moto majalada yao. Waikela alihifadhi nyaraka na majalada yake yote hadi yakamfikia mwandishi baada ya  zaidi ya miaka ishirini baada ya kufungiwa jumuiya hiyo. Regional Commissioner wa Jimbo la Magharibi wakati ule alikuwa Rashid Heri Baghdelleh yeye alikwenda kuonana na wafungwa wa siasa katika jela ya Uyui akiwa na salamu kutoka kwa Rais Nyerere kuwa wafungwa wa siasa waombe msamaha na yeye atawaacha huru. Waikela alikataa kuomba msamaha na hoja aliyotoa ilikuwa yeye hajatenda kosa lolote kwa hiyo haoni haja ya kuomba msamaha. Baada ya kutoka kizuizini mwaka 1965, Waikela alikuta ofisi ya EAMWS Tabora imefungwa na Waislam wanatishwa na serikali wasiifungue. Waikela aliwashawishi Waislam wakusanye sahihi zao na wamplekee kuomba ofisi ifunguliwe. Hili lilifanyika na ofisi ile ikafunguliwa upya chini ya Waikela na ikaendelea kutoa huduma kwa Waislam kwa miaka mitatu hadi serikali ilipoivunja EAMWS mwaka wa 1968. Hivi sasa Waikela ni mtu mzima na bado anajishughulisha na kuendeleza harakati za kueneza Uislam.
[33] Tabligh ilikuwa imepata mafanikio makubwa kiasi kuwa katika mkutano wa EAMWS wa mwaka 1966 Tewa Said Tewa aliomba kuwa taarifa maalum itolewe katika mkutano ujao kuonyesha takwimu za Wakristo waliorudi katika Uislam.
[34] Tewa Said Tewa, ‘A Probe…’
[35] Tewa op.cit.
[36] Habari katika sura hii zinatokana na mahojiano kati ya mwandishi na Tewa Said Tewa, Bilali Rehani Waikela na Ali bin Abbas mmoja wa wanafunzi wa Sheikh Hassan bin Amir. Habari nyingine zinatoka kwenye mswada wa Tewa ambao haujachapishwa, ‘A Probe in the History of Islam in Tanzania’. Tewa aliandika habari hizi kuhusu harakati za Waislam kujiletea maendeleo chini ya EAMWS miaka kumi na nne baada ya aliekuwa rais wa Tanzania Julius Nyerere kuivunja.
[37] Tewa Said, ibid.
[38] Angalia Kiwanuka, op. cit. uk. 75.
[39] Ibid.
[40] Benjamin Mkapa alishinda uchaguzi na kuwa rais wa tatu   wa Jamuhuri ya Tanzania mwaka 1995.
[41] Nyerere alizidi kutishika pale mara baada ya maulidi yale yaliyofanikiwa, mwezi Julai, 1968 Tewa akifuatana na masheikh wawili, Athumani Manzi na Sheikh Minshehe Mgumba akafanya safari ya kutembelea Dodoma, Kongwa, Mpwapwa, Kondoa, Tabora na Kigoma. Huko kote Waislam walikuwa wakijitokezakwa wingi kumpokea kiongozi wao. Tabora ulifanyika mkutano mkubwa uliohutubiwa na Sheikh Jumanne Biasi na Rehani Bilali Waikela. Kigoma Tewa alifanyiwa mapokezi makubwa akasindikizwa na magari hadi Ujiji msafara ukiongozwa na Sheikh Khalfani Kiumbe. Katika ziara hizi Tewa alikuwa akifungua shule zilizokuwa zimejengwa na EAMWS. Ilikuwa Kigoma ndipo Tewa Said Tewa alipoonyeshwa barua kutoka kwa Adam iliyoambatanishwa na miniti za mkutano kati ya Sheikh Abdallah Chaurembo na Sheikh Ramadhani Chaurembo akiuandikia uongozi wa EAMWS Kigoma akiwaomba Waislam wajitoe kutoka EAMWS kwa sababu ilisoma maulidi Ilala. Aliporudi Dar es Salaam Tewa aliufahamisha uongozi wa makao makuu kuhusu barua ile. 
[42]  Taarifa ya Kamati ya Utendaji EAMWS Mkoa wa Tanga 23rd Oktoba, 1968, Ripoti ya Sheikh A.J. Jambia. 
[43] Kiwanuka, op.cit., uk. 2.

[44] Angalia Ripoti ya Kwikima katika The Standard, 12th Desemba, 1968. Vilevile The Nationalist, 24 Oktoba, 1968.  
[45] Angalia Ripoti ya Kwikima.
[46] Tewa, ‘A Probe…’
[47] Ujenzi wa Chuo Kikuu ulikuwa umeanza na jiwe la msingi lilikuwa limewekwa na Julius Nyerere rais wa Jamuhuri ya Tanzania.
[48] Tume ya Uchunguzi ya Waislam ilikuwa na wajumbe wafuatao: Mussa Kwikima (Dar es Salaam), Rajab Ukwaju (Mara), Dr. Hussein Lweno (Dar es Salaam), Mussa Nabahani (Lindi), Bilali Rehani Waikela (Tabora), Abdul Karim (Tanga) na Khamis Khalfani (Dodoma).
[49] Tewa ibid.
[50] Barua ya Mwenyekiti Halmashauri ya Uchunguzi Mogogoro ya Waislam kwa Waziri wa Habari na Utangazaji, 21 Novemba, 1968.
[51] The Nationalist, nukuu kutoka kwa Kiwanuka, uk.81.
[52] Maelezo kutoka mwanakamati wa Halmashauri Kuu ya TANU ambae ameomba jina lake listiriwe.
[53] Mwezi Novemba 1967 Tewa Said Tewa alikuwa amefanya ziara ya Mwanza na Bukoba iliyokuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa alifanya majadiliano na viongozi wa Waislam wa huko kama Sheikh Amin Abdallah wa Mwanza, Sheikh Ali Migeyo na Sheikh Suedi Kagasheki wa Bukoba.
[54] Kiwanuka, uk.2-3.
[55] Ibid., p.81
[56] The Standard, 9th November 1968 nukuu kutoka Kiwanuka p. 81. Vilevile angalia The Standard, 20 November 1968. 
[57] Sheikh Hassan bin Amir alianza kukosana na serekali mara tu baada ya uhuru pale Kanisa Katoliki ilipotoa vitu vya kukumbuka uhuru vilivyokuwa vimenakshiwa na picha za Kikristo. Sheikh Hassan bim Amir alikereka na hili na hasa pale George Kahama, Waziri wa Mambo ya Ndani, alipokwenda Italia kuweka uhusiano baina ya Tanganyika na Vatikano. Kuanzia hapo, Sheikh Hassan bin Amir, kupitia Daawat Islamiyya na kwa kupitia wanafunzi  wake waliokuwa wameenea nchi nzima alianza kuandika khutba za Ijumaa na kuzisambaza katika misikiti ya nchi nzima na khutba hizo zikawa zinasomwa katika sala ya Ijumaa. Ujumbe wake kwa Waislam ulikuwa Waislam watumie fursa iliyoletwa na uhuru kwa kujielimisha ili wagawane madaraka sawa na Wakristo katika kuiendesha nchi. Sheikh Hassan bin Amir akaanzisha mfuko wa elimu ambao Waislam walitakiwa kuchanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule. Kwa ajili ya kuingia kwake kati pale Nyerere alipotaka kuivunja EAMWS, Sheikh Hassan bin Amir akaonekana ni kikwazo kwa Ukristo kuukalia juu Uislam.
[58] Sheikh Kassim Juma aliitumikia serikali kwa karibu miaka ishirini hadi mwaka 1992 ghafla akaanza kuishitumu serikali na kumtaja Nyerere kama mtu aliyepanga njama za kuuhujumu Uislam. Sheikh Kassim alikamatwa mara mbili na kuwekwa ndani kwa kosa la ‘kuwachonganisha Waislam dhidi ya serikali’. Alipotolewa afya yake ikawa mbaya na akafa mwaka 1993. Historia fupi ya Sheikh Kassim ipo katika Al Haq Newline,(Pakistan) No.1 Muharram/Safar, 1415-A.H. ‘Sheikh Kassim bin Juma bin Khamis 1940-1994’ 
[59] Baada ya kundi la Adam Nasibu kutoka Tanga masheikh wakaanza kukamatwa na kuwekwa kizuizini na ni wakati huo Saleh Masasi alitangaza kujitoa kwa Iringa.
[60] Miaka mingi baadae Rashid Kawawa alisema kuwa anajuta kuunga mkono kukamatwa kwa Mufti wa Tanganyika na Zanzibar, Sheikh Hassan bin Amir akaelekeza lawama kwa wale waliomshauri kufanya hivyo.
[61] Ali Muhsin, op.cit. uk 87.
[62] Nyaraka za Tewa hazikuonyesha ni gazeti lipi lakini kwa kuwa wakati ule Tanzania magazeti ya Kiingereza yalikuwa mawili, The Nationalist gazeti la TANU na The Standard lililokuwa likimilikiwa na Lonrho, ni wazi gazeti lileThe Standard.
[63] Angalia Kwikima Report.
[64] Pamoja na mambo mengine Taarifa ya Tume ya Kwikima ilipendekeza mabadiliko katika katiba ya EAMWS, kuondolewa kwa nafasi ya Patron, kuasisiwa kwa jumuiya mpya ya Kiislam itakayokuwa haina ubaguzi wa rangi na taarifa ilisisitiza jumuiya mpya kutochanganya dini na siasa.
[65] Ibid.
[66] The Nationalist,15 December, 1968.
[67] Baraza,(Nairobi), 12 Desemba, 1968.
[68] Rashid Kayugwa Afisa wa Usalama Taifa, Dar es Salaam ndiye aliyepewa kazi ya kudumisha mawasiliano kati ya kundi la Adam Nasibu serekali. Kayugwa ndiye aliyekuwa akielekeza kundi la Adam Nasibu mbinu za propaganda na nini kifanyike na kwa wakati gani ili kuvunja umoja wa Waislam. Kayugwa alikuwa amepata mafunzo yake ya ukachero Israel, Checkoslovakia na Marekani. Katika kuhakikisha mafanikio ya mkutqano wa Iringa, Kayugwa ambae ni mzaliwa wa Iringa alipendekeza mkutano wa Waislam wa Taifa ufanyike Iringa kwa kuhofu vurugu na upinzani kutoka kwa Waislam wa Dar es Salaam. Baada ya kusoma kitabu cha Padri John Sivalon kilichoeleza kuwa Kanisa baada ya uhuru liliendesha hujuma dhidi ya Uislam na Waislam kwa kupitia serikali, ndipo ilipomdhihirikia ukweli na kuona kuwa alipokuwa akitumiwa kuhujumu EAMWS hakuwa akitumikia serikali kama alivyokuwa anadhani bali alikuwa akilitumikia Kanisa, kama kuomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu, aliamua kueleza mchango wake katika kuwahujumu Waislam na Uislam ili iwe fundisho na onyo kwa Waislam watakao kuwa katika utumishi wa vyombo kama hivyo siku za usoni. Kabla ya kufa kwake alieleza masikitiko yake kwa kukandamizwa kwa Waislam na akatoa mfano wake mwenyewe wa kutopandishwa cheo katika Usalama wa Taifa kwa sababu tu yeye alikuwa Muislam. 
[69] Tewa ibid.
[70] Angalia Kiwanuka, uk.85. Vilevile Proceedings of the Iringa Conference 12th – 15th December,1968 katika Maktaba ya Chama cha Mapinduzi, Dodoma. Vilevile The Standard, 18th December, 1968. 
[71] The Standard,18th December, 1968.
[72] The Standard, 20th December 1968.
[73] Ibid.
[74] Tewa, ibid. Vilevile angalia The Standard, 20th December 1968.
[75] Kiwanuka, uk. 86. Habari nyingine kuhusu Mussa Kwikima zimepatikana katika mazungumzo na yeye mwenyewe Kwikima pamoja na maelezo kutoka kwa Bilali Rehani Waikela. Katika mabadiliko makubwa na bishara Mussa Kwikima ndiye alisimama mahakamani kumtetea Sheikh Kassim Juma wakati aliposhtakiwa kwa ‘kuwachonganisha Waislam na serekali’. Sheikh Kassim Juma alikuwa akimpiga vita Kwikima wakati akiwa katibu wa Tume ya Waislam chini ya EAMWS, Kwikima alipokuwa akitafuta sulhu baina ya pande mbili. 
[76] Pamoja na watu hawa watatu wengine waliokuwa katika mpango ule walikuwa: Omari Muhaji, Juma Jambia, Juma Swedi
[77] Baada ya miaka mingi ya Waislam kuisusia BAKWATA ikafika mahali ikawa inashindwa hata kufanya mikutamo ya uchaguzi wa viongozi kwa mujibu wakatiba yake. Kwa hali kama hiyo ilikuwa kwa Msajili wa Vyama kuivunja. Serikali ilipooona imekabiliwa na hali hiyo ikachukua jukumu la kutayarisha mkutano ili kuihuisha BAKWATA. Tarehe 28 Aprili 1993 Waziri wa Mambo ya Ndani na Makamo Waziri Mkuu Augustine Mrema aliitisha mkutano kati ya Waislam na Wakristo katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam. Mkutano ulikuwa hauna agenda. Kanisa lilipeleka ujumbe wa hali ya juu kabisa. Waislam hawakutokea isipokuwa BAKWATA. Katika mkutano ule Mrema alieleza kuwa uchaguzi katika BAKWATA umechelewa sana kwa kukosa faedha.Kanisa paleplale lilijitolea fedha kuipa BAKWATA ili ifanye uchaguzi wake. Halikadhalika Mrema alisaidia kukusanya fedha kutoka kwa wafanyabiashara kwa ajili ya uchaguzi wa BAKWATA. Mkutano ulifanyika Dodoma tarehe 10th -12th Mei. Badala ya kufanya uchaguzi BAKWATA ilirekebisha katiba yake ili iweze kumpa ruhusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA haki ya kufukuza na kumweka katika uongozi au kumtoa mtu yeyote bila ya kipingamizi. 

[78] Angalia Bergen, uk. 238.
[79] Daily News, 6th November 1985.
[80] Sivalon, op.cit. uk.49.
[81] Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Jamuhuri ya Tanzania mwaka 1985-1995.
[82] Warsha ndiyo jumuiya ya kwanza katika historia ya Tanzania baada ya uhuru kuanza kuwaanda Waislam na kupambana na dhulma zilizokuwa zikifanyiwa Waislam. Kwa kipindi chote cha uhai wake serikali ilikataa kukipa usajili. Hii ilikuwa heri kwao kwa kuwa kiliendesha kampeni zake chini kwa chini, kampeni ambazo zilileta mafanikio makubwa hasa katika kuwaelimisha Waislam kuhusu mbinu za adui. Warsha iliweza kufikia hatua ikachukua uongozi wa BAKWATA. Warsha haikudumu katika uongozi kwa muda mrefu. Serikali ikimtumia Adam Nasibu kwa mara ya pili iliweza kuwapiga marufuku vijana hawa wasishugulike na uongozi wowote katika jumuiya yoyote ya Kiislam. Hata hivyo athaari za Warsha zingalipo hadi sasa. Vongozi wengi wa jumuiya za Kiislam hivi sasa wamepata uamsho na mafunzo yao ya awali ya uongozi katika Warsha. Mwaka wa 1981 Warsha walifanya utafiti ambao ulikuwa haujawahi kufanyika kabla, Warsha walifanya utafiti katika elimu ya Waislam Tanzania. Utafiti ulionyesha Waislam walikuwa wana nafasi chache katika vyuo vya elimu ya juu. Taarifa ya utafiti huu ilisambazwa kwa Waislam wote wa Tanzania.
[83] Angalia Kiongozi, Julai 15-31, 1993.
[84] Hali ya Waislam katika Tanzania ni ya kusikitisha inapokuja suala la kueneza habari au propaganda. Vyombo vyote vya habari, vya serikali na vilivyo chini ya wamiliki binafsi vyote vipo katika mikono ya Wakristo. Vyombo hivi vinatumika vyema katika kupiga vita Waislam.
[85] Nje ya vyombo hivyo vya serikali, Profesa Malima alikuwa na jeshi kubwa ka Waislam waliokuwa nyuma yake, wengi wao wakiwa vijana. Wakiwa hawana vyombo vya habari wanavyovimiliki, Waislam walichapa makaratasi na kuyatawanya nchi nzima yakimuunga mkono Profesa Malima huku yakieleza udhalimu wa serikali, mengine yamkitaja Julius Nyerere na Kanisa Katoliki kama washiriki katika kuwadhulumu Waislam. Kwa ajili hii Profesa Malima alipendeza machoni mwa Waislam. Profesa Malima akawa anaalikwa katika kila hafla muhimu ya Waislam. Katika hafla zile Profesa Malima aliwahutubia Waislam kuhusu madhila wanayoyapata.

[86] Aboud Jumbe, The Partner-Ship, Amana Publishers, Dar es Salaam, 1995, uk. 125-138.
[87] Jan P van Bergen, Religion and Development in Tanzania, (Madras, 1981) passim.
[88] Kitabu hiki hivi sasa hakipatikani na kulikuwa na uvumi kuwa Usalama wa Taifa walikuwa wakikitafuta ili kikusanywe na kuteketezwa kwa kuwa kilikuwa kinahatarasha umoja na mshikamano wa wananchi na kwa ajili hiyo amani ya nchi. 
[89] John C. Sivalon, Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985, (Ndanda,1992)
[90] Ibid. uk. 37.
[91] K. Mayanja Kiwanuka, The Politics of Islam in Bukoba District (1973), B.A. Thesis, University of Dar es Salaam.
[92] Mohamed Said, ‘Islam and Politics in Tanzania’ (1989) makala hii ilichapishwa tena kwa jina hilo hilo katika Al Haq International (Karachi) Vol. 1 No. 3 August-December 1993.
[93] ‘Kwikima Report’ imo ndani ya The Standard, 12th December, 1968, vilevile The Nationalist, 15th December, 1968. Angalia vilevile Bergen, uk. 238.
[94] Angalia, USAID/Tanzania ‘Tanzania Flash Points Study’, April, 1999.
Post a Comment