Wednesday, 14 December 2016

TUME YA MUFTI WA BAKWATA NA MALI ZA WAISLAM ZILIZODHULUMIWA MWAKA WA 1968 ILIPOUNDWA BAKWATA NA TAMIM FARAJ


Dondoo Fupi Kuhusu Mali za Waislamu Zilizodhulumiwa mwaka 1968 Ilipoundwa Bakwata

1.       Kulikuwa na jumuiya ya Waislamu wakati wa ukoloni wa Muingereza ikiitwa East African Muslim Welfare Society (EAMWS). Jumuiya hii  ilifanya kazi za kuwaletea maendeleo Waislamu wa Tanganyika na kusimamia mali zao zilizokuwa ndani ya  jumuiya hiyo.

2.     Baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961wakajitokeza Waislamu wachache katika jumuiya hiyo ya EAMWS kwa kurubuniwa na Wakaanza kuleta chokochoko dhidi ya katiba na mfumo wake. Hata hivyo, Waislamu wengi  wanachama wa jumuiya hiyo walikataa madai yale ya wachache.

3.      Hatimae mwaka 1968 wale wachache wakaamua kuunda jumuiya yao iitwayo Bakwata kwa msaada wa kuungwa mkono na serikali. Lakini Waislamu walio wengi nchini hawakuitaka Bakwata. Waliipenda EAMWS.

4.  Mwaka huohuo katika kipindi cha kuundwa Bakwata,  serikali ikaivunja jumuiya ya EAMWS, Waislamu wanachama wa EAMWS waliipinga hatua hiyo ya serikali wakiungwa mkono na Waislamu walio wengi nchini.

5.      Serikali haikuishia hapo. Ikachukua mali za Waislamu zilizokuwa zikimilikiwa na  zikisimamiwa na EAMWS na kuzikabidhi Bakwata.  Waislamu wanachama wa EAMWS wakiungwa mkono na Waislamu wengi nchini walikipinga kitendo hicho cha serikali na kuendelea kuikataa na kuitenga Bakwata. Pamoja na mali za EAMWS, mali za jumuiya nyinginezo nazo zikachukuliwa na serikali na kukabidhiwa Bakwata. Jumuiya hizo ni pamoja na Al Jamiiyyatul Islamia fii Tanganyika, ambapo Bakwata hadi waliweka makao yao makuu katika majengo ya jumuiya hiyo huru iliyoanzishwa kabla ya EAMWS.

6.  Sasa tunatangaziwa kuwa kumeundwa Tume ya Mufti wa Bakwata kurudisha mali za Waislamu zilizopewa Bakwata na serikali mwaka wa 1968. Swali kubwa ni kuwa Je, Tume ya Mufti wa Bakwata hii itazirudisha mali za Waislamu wa EAMWS na za Aljamiiyyatul Islamia fii Tanganyika pamoja na zile za jumuiya nyinginezo kadhaa ikiwemo Arusha Muslim Union?

7.   Imetangazwa kuwa Tume hii ni ya Mufti na si Tume ya Bakwata. Lakini hapohapo  tunaambiwa kuwa Mufti kaunda Tume hii kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya katiba ya Bakwata.

8.    Hebu na tujaalie kuwa mtangazaji amejichanganya katika kutangaza hayo ya kumtofautisha Mufti na Bakwata.  Ni vema basi tukaambiwa, Mufti huyu asiye Bakwata alichaguliwa na jumuiya au taasisi ipi, katiba ya jumuiya au taasisi hiyo ni ipi, huyu Mufti hivi sasa anatumikia nafasi yake kwa kulipwa ujira wake na jumuiya au taasisi gani?

9.      Kwa kuwa tangazo limeonesha kuwa mali hizi chini ya Bakwata zimekumbwa na matatizo kadhaa yakiwemo ya kutojulikana zilipo, kufujwa, kukabidhiwa au kutumika chini ya mikataba isiyoeleweka, je, uchunguzi unaweza kuwa huru endapo itaonekana kuwa Mufti na hata baadhi ya wajumbe ni Bakwata?  Je, mali hizi endapo zitapatikana zinaweza kuwa salama endapo zitaendelea kuwa mikononi mwa Bakwata au kitengo chake? 

10.  Mwisho, kwa kuzingatia haki na uadilifu chini ya misingi ya sharia za Uislamu zitokanazo na Allah, kama baada ya Tume kumaliza kazi au hata pasipokuwepo kwa Tume, je, ni halali kwa Mufti au Bakwata kushiriki katika kuhodhi na kuzitumia mali zisizo zao, mali ambazo zilizoporwa kwa uonevu? Mali za dhulma zilizoporwa kwa kutumia mabavu, toka jumuiya zilizokuwa na wanachama wake na malengo waliojiwekea wenyewe, ambayo si ya Kibakwata na Mufti wake?Al Jamiatul Islamiyya Muslim SchoolChuo cha Maalim Mzinga kilichoanzishwa mwaka wa 1935


Moja ya shule walizojenga Waislam baada ya nakama ya mwaka wa 1968

Post a Comment