Sunday, 9 July 2017

SHEIKH SULEIMAN TAKADIR ALIMWITA NYERERE MTUME WA AFRIKA MZEE MWINYI ANGEPENDA KUMPA MAGUFULI URAIS WA MAISHA

Mwandishi akimkabidhi Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi kitabu cha Maisha ya Abdul Sykes,
Ukumbi wa Korea Dar es Salaam

Kauli ya Rais Mstaafu Mzee Hassan Mwinyi kuwa kama isingekuwa katiba ya Tanzania kuweka kikomo cha rais kutawala kwa si zaidi ya awamu mbili basi Rais Magufuli ingefaa atawale labda maisha kutokana na kazi yake nzuri kwa taifa hili. Kauli hii imezua mjadala mkubwa kutoka kwa wananchi. Wako wanaopinga na halikadhalika wako pia wanaounga mkono. Mapenzi hakika humtia mtu upofo na ikamnyang’anya akili na uwezo wa kufikiri.

Nataka wasomaji wangu nikurudisheni miaka mingi nyuma wakati Tanganyika inapigania uhuru wake na kiongozi wa mapambano haya alikuwa Julius Kambarage Nyerere. Ilikuwa mwaka wa 1957 na Nyerere alikuwa kijana mdogo wa miaka 35. Naomba mkisome kisa hiki hapi chini kama nilivyokiandika katika kitabu cha Abdul Sykes:

''Ilikuwa katika taarab iliyoandaliwa kusheherekea kufunguliwa kwa tawi la TANU Dar es Salaam ya Kaskazini katika mtaa wa Mvita, nyumba namba 10, tarehe 10 Agosti, 1957, ulimi wa Sheikh Takadir ukateleza, akamuita Nyerere ‘’Mtume,’’ Tawi la TANU Dar es Salaam ya Kaskazini lilikuja kuwa lenye nguvu sana kuliko yote na tawi likawa na mafanikio labda kupita matawi yote katika Tanganyika. Mwenyekiti wake alikuwa Mtoro Kibwana na mweka hazina Haidar Mwinyimvua, ambae baadae aliingia Kamati Kuu ya TANU ya Taifa. Kwenye hafla ile, katika kumtambulisha Nyerere na kummiminia sifa, Sheikh Takadir bila kufikiri aliwaambia wasikilizaji wake kuwa, ‘’Nyerere ni Mtume wa Afrika.’’ Kama kauli ile ingetolewa siku nyingine yoyote ile, huenda tamko hilo lisingezua kishindo, na huenda lingepita bila kuwa na taathira yeyote mbaya. Lakini ufunguzi wa tawi la TANU la Mvita katika siku hiyo tarehe 10 Agosti, 1957 ilikuwa siku maalum kwa wakazi wa Dar es Salaam.


Kushoto Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadiri, Clement Mtamila na Titi Mohamed
Nyuma ya Nyerere Mama Maria Nyerere, Rajab Diwani na John Rupia


Kwanza, Dar es Salaam ilijitokeza kushuhudia kuhama kwa mwimbaji stadi, Nuru binti Sudi, kutoka Al-Watan na kujiunga na wapinzani wao Egyptian. Hivi vilikuwa vikundi viwili vya taarab vikishindana mjini Dar es Salaam. Siku hiyo Nuru alikuwa anaimba pamoja na kikundi chake kipya kwa mara ya kwanza na mashabiki wake walikuwa wamekuja kumwona bingwa wao akiimba katika hafla ya TANU. Halikadhalika mashabiki wa Egyptian walikuwa wamekuja vile vile kushangilia na kuwazomea washindani wao kwa kumchukua bingwa wao. Kulikuwa na sababu nyingine kwa watu kushangilia. Katika kuhama huko kutoka Al-Watan na kuingia Egyptian, Nuru alikuwa ameweka msimamo wa kisiasa. Nuru alikuwa na damu mchanganyiko. Baba yake alikuwa Mwarabu na mama yake alikuwa Mwafrika.  Kabla ya kutoka Al-Watan na kuingia Egyptian alikuwa mwanachama wa Coronation ambacho kilikuwa chama cha akina-mama wenye asili ya Kiarabu. Kwa hiyo ilichukuliwa kwamba, maadam Egyptian ilihusiana na Waafrika, kwa kitendo kile cha kuhama Al-Watan, Nuru alikuwa ameasi na kurudi kwa ndugu zake, yaani Waafrika.  Amerudi kwenye asili yake, kwenye tumbo la mama yake aliyemzaa. Hivi ndivyo mambo yalivyokuwa siku zile, kila jambo lilipewa tafsiri ya kisiasa. Wakati huo UTP ilikuwa tayari imeshanzishwa na Egyptian ilikuwa imetunga nyimbo maalum kwa ajili ya hafla hiyo ambayo Nuru aliimba kuidhihaki UTP. Sehemu ya mashairi yake yalikuwa yanasema hivi: ‘’Ma-UTP wana majambo, TANU wanaichukia.’’Chief David Kidaha Makwaia


Pili, ili kuadhimisha kufunguliwa kwa tawi la TANU Mvita, TANU iliwaalika wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria, wengi wao machifu, ili kushuhudia sherehe hiyo. Miongoni mwao walikuwa Chifu David Kidaha Makwaia, Humbi Ziota, Chief Msabila Lugusha, Mwami Theresa Ntare na wengine wengi. Vilevile walikuwepo watu wengine mashuhuri kama Hamis Mfaranyaki ambae ndiye alikuwa kiongozi wa Wangoni mjini Dar es Salaam, Paul Bomani, Said Chaurembo, kaka yake Sheikh Abdallah Chaurembo na watu maarufu wengine wengi. Pamoja na watu wote hawa mashuhuri kuhudhuria, huu ulikuwa usiku adhimu kwa TANU. Hapakuwa na shaka yoyote kuwa chochote kitakachosemwa katika hafla kama hiyo kitakuwa na athari kwa watu. Ilikuwa katika hafla hii ndipo siku ulimi wa Sheikh Takadir ukateleza akampa utume Nyerere.’’


Upepo ukabadilika baada ya mwaka mmoja tu katika joto la siasa lililoanzishwa na Uchaguzi wa Kura Tatu wa mwaka wa 1958 pale Nyerere alipoonekana kuwaleta watu katika TANU ambao walisimama katika uchaguzi ule kwa tiketi ya TANU ili kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria. Wengi katika hawa hawakuwa wamenyanyukia na TANU. Sheikh Takadiri uso na macho akamtuhumu Nyerere kwa tuhuma nzito na ya kutisha jambo ambalo TANU yenyewe ilionya mapema kabisa kuwa lisiletwe hata kwa mbali katika TANU nalo lilikuwa suala la Waislam. Vumbi zito lilifumuka kwa wanachama wa TANU kukiacha chama na kuunda kwanza African National Congress (ANC) ya Zuberi Mtemvu na kisha All National Union of Tanganyika (AMNUT) ya Mashado Plantan na wenzake. ‘’Utume.’’ wa Nyerere ulikuwa umetiwa dosari na mwenyewe aliyempa cheo hicho Sheikh Takadiri.
Zuberi Mtemvu Rais wa African National Congress (ANC)


Lakini vita hivi havikuishia hapo. Mwaka wa 1963 Nyerere akalivunja Baraza la Wazee wa TANU, baraza ambalo wajumbe wake wote zaidi ya 200 walikuwa Waislamu watupu na sababu iliyotolewa ni kuwa lilikuwa likichanganya, ‘’dini na siasa.’’ Huu pia haukuwa mwisho wa vumbi lile zito. Mwaka wa 1968, Nyerere akapiga marufuku East African Muslim Welfare Society (EAMWS) chama cha ustawishaji Uislam. Ilisadifu kuwa wakati haya yanatokea Sheikh Takadir hakuwepo kushuhudia mabadiliko haya ya ‘’Mtume,’’ wa Afrika. Baada ya kufukuzwa TANU na kupigwa pande na ndugu zake Sheikh Takadir hakuchukua muda akafa.

Sifa kubwa ya binadamu ni kukosa uwezo wa kujua ghaibu. Inawezekana Mzee Mwinyi kama alivyokuwa Sheikh Takadir kashindwa kutafakari ule ukweli kuwa binadamu ni kigeugeu na nyoyo za binadamu hugeuka. Aliye mwema leo ndiyo huyo mbaya wa kesho. Tuna mengi ya kujifunza katika historia ya nchi yetu. Sheikh Takadir alimpa Nyerere sifa ya utume, Mzee Mwinyi yeye angependa kumpa Magufuli urais wa maisha.
Post a Comment