Thursday, 31 August 2017

MIONGO MIWILI WAMEKATAA KUBADILISHA JINA LA MTAA WA TANDAMTI KUWA ''MSHUME KIYATE''


Mzee Mshume Kiyate na Baba wa Taifa, 1964

Jina la Mshume Kiyate kwa sasa si geni tena katika historia ya TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.

Mzee Mshume alikuwa katika Baraza la Wazee wa TANU kuanzia lilipoundwa 1955.

Mshume Kiyate alikuwa kiishi Mtaa wa Tandamti na akifanya biashara Soko la Kariakoo toka miaka ya 1950. Yeye ndiye aliyekuwa dalali wa samaki wote walioletwa pale sokoni. Kazi hii ilimtajirisha kwa kiwango cha nyakati zile na yeye alitumia fedha zake nyingi katika harakati za kuijenga TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.

Kubwa ambalo lilimpambanua Mzee Mshume katika historia ya uhuru ni kule yeye kujitolea kubeba jukumu la chakula cha nyumba ya Baba wa Taifa kuanzia miaka ya mwanzo ya TANU hadi uhuru unapatikana mwaka wa 1961 na kuendelea kufanya hivyo hata pale Baba wa Taifa alipomwambia, ‘’Mzee Mshume sasa basi hivi vikapu vyako vya chakula, mimi sasa nalishwa na serikali.’’

Jibu la Mzee Mshume lilikuwa, ‘’Hapana Mheshimiwa sitoacha kuleta chakuka nyumbani kwako kwani nataka wewe na watoto wako ule chakula hiki na hicho cha serikali wape wageni wako.’’

Huyu ndiye mzalendo mpigania uhuru wa Tanganyika na rafiki kipenzi cha Baba wa Taifa, Mzee Mshume Kiyate.

Miaka takriban 20 iliyopita aliyekuwa Meya wa Jiji ;a Dar es Salaam marehemu Kitwana Selamani Kondo katika kutambua mchango wa Mzee Mshume Kiyate alibadili jina la Mtaa wa Tandamti kuwa, ‘’Mtaa wa Mshume Kiyate.’’
Hadi hivi ninavyoandika na nimepita mtaa huu leo nimekuta kibao kipya kimewekwa lakini jina ni lile lile la zamani.


Hii nini maana yake?
Dharau, khiyana au nini? Picha hiyo hapo juu ilipigwa mwaka wa 1964 baada ya maasi ya wanajeshi na Baba wa Taifa kurejeshwa madarakani na Jeshi la Waingereza. TANU ilifanya mkutano mkubwa sana Jangwani na Mzee Mshume Kiyate siku ile alimvisha Baba wa Taifa kitambi kama ishara ya kuonyesha kuwa Wazee wa Dar es Salaam wale waliompokea na kuwa na yeye bega kwa bega kupigania uhuru wa Tanganyika bado wako nyuma yake na wanamuunga mkono. 

Huyu ndiye Mzee Mshume Kiyate.


Waliosimama wa pili kulia ni Mzee Mshume Kiyate
Mshume Kiyate wa kwanza kulia aliyemshika mkono Baba wa Taifa na
pembeni kwa Baba wa Taifa ni Mzee Max Mbwana akifuatiwa na Mzee
Mwinjuma Mwinyikambi
Kuna picha mashuhuri ya Mzee Mshume na Baba wa Taifa iliyopigwa Novemba 1962 wakati wa Uchaguzi Mkuu. 

Picha hiyo inamuonesha Mzee Mshume akiwa amevaa koti, kanzu na kofia amemshika Baba wa Taifa mkono akimsindikiza kupiga kura. 

Karika utawala wa Baba wa Taifa, magazeti ya ''Uhuru'' na ''Daily News,'' yamekuwa yakiitumia picha hii kila baada ya miaka mitano katika uchaguzi wa rais kama njia ya kuwahamasisha watu kupiga kura na kumchagua Baba wa Taifa. 
Post a Comment