Wednesday, 10 January 2018

SIKU BABU YANGU SALUM ABDALLAH ALIPOMKABILI FREDERICK MCHAURU KATIKA MGOMO WA WAFANYAKAZI WA TANGANYIKA RAILWAYS TABORA 1947

SIKU BABU YANGU SALUM ABDALLAH ALIPOMKABILI FREDRICK MCHAURU KATIKA MGOMO WA WAFANYAKAZI WA TANGANYIKA RAILWAYS TABORA 1947

Frederick Mchauru

Ndani ya gazeti la Raia Mwema (Januari 3-9, 2018) kulikuwa na makala ya maisha ya Mzee Fredrick Mchauru. Kama kawaida yangu kupenda kusoma maisha ya Watanzania maarufu niliitupia jicho. Haikunipitikia kabisa kama Mzee Mchauru niliyemtaja katika kitabu change cha historia ya uhuru wa Tanganyika mwaka wa 1998 bado atakuwa hai. Jina hili likawa linajirudia akilini kwangu. Naam Mzee Mchauru yu hai akiwa sasa na umri wa miaka 97. Huyu Mchauru ndiye yule aliyekabiliana na na babu yangu Salum Abdallah katika uwanja wa mpira wa Town School Tabora chini ya miembe wakati wa kupambana na wakoloni, babu yangu akisimama na wananchi wa Tanganyika wakati Mchauru akiwa mtumishi wa serikali ya Waingereza? Naam ndiye yeye. Makala ile ilikuwa tamu haikuisha imekuja kuhitimishwa na toleo la juma hili la Raia Mwema (10 – 16 Januari 2018).

Katika toleo hili mwandishi Ezekiel Kamwaga kanitaja kwa jina kuwa nimemwandika Mzee Mchauru katika historia ya uhuru wa Tanganyika. Kamwaga akaeleza kuwa nimepata kusema kuwa Mzee Mchauru alipata shida kuelewana na wale waliokuwa wanapigania uhuru wa Tanganyika.


Raia Mwema (10 – 16 Januari 2018)


Dhulma ilikuwa imezidi sana na wafanyakazi wa bandarini Dar es Salaam wakiongozwa kwa siri na Abdul Sykes wakati ile kijana mdogo wa miaka 23 waliamua kufanya mgomo kudai haki zao. Mgomo wa Makuli kama ulivyokujafahamika ulienea Tanganyika nzima.

Lakini ili kuuelewa mgomo huu ni muhimu sana msomaji akasoma historia nzima ya mgomo huu chanzo chake na vipi wananchi waliweza kujiunga pamoja hadi kufikia kuwa na uwezo wa kuitingisha serikali kwa mgomo kuenea Tanganyika nzima.

Haiwezekani kwa hapa kueleza historia yenyewe nitakachifanya nitaweka link ili msomaji kwa wakati wake mwenyewe baadae aweze kusoma lakini kwa sasa napenda kukunyambulieni ilikuwaje hadi babu yangu akapambana uso kwa macho na Fredrick Mchauru katika mgomo wa wafanyakazi wa mwaka wa 1947:


Tabora, Western Province 11 Septemba, 1947
‘’…mgomo huo ulioenea kama moto wa makumbi ulikumba nchi nzima kwa kasi ya ajabu. Ilikuwa kama vile wafanyakazi wa nchi nzima wametaarifiana. Wafanyakazi wa Tanganyika Railways huko Tabora wakiongozwa na Salum Abdallah waliingia kwenye mgomo tarehe 11 Septemba. Chama cha African Association mjini Tabora kilimteua Mwalimu Pinda, aliyekuwa akifundisha shule ya St Mary, kuwa 'mshauri' wa wafanyakazi waliogoma.  Asubuhi ya siku ya mgomo wafanyakazi wa Tanganyika Railways walikusanyika kwenye kiwanja cha mpira chaTown School, wakakaa chini ya miembe kujikinga jua. Tabora ni maarufu kwa miti hiyo. Tangu siku hiyo kiwanja hiki kikawa ndicho uwanja maalum kwa mikutano yote ya siasa.

Serikali ilimtuma kijana mmoja kutoka Masasi aliyesoma katika shule za misheni, Frederick Mchauru kuwahutubia wafanyakazi na kuwaomba wasimamishe mgomo na warudi kazini.

Mchauru alikuwa Mmakonde kutoka Newala. Alielimishwa St. Josephís College, Chidya na St. Andrewís College, Minaki. Mwaka 1946, Mchauru alikuwa amerudi kutoka LondonUniversity akiwa amehitimu masomo yake na kuanza kazi mjini Tabora kama Assistant Social Development Officer. Wafanyakazi waliokuwa kwenye mgomo walimpigia kelele wakimtaka anyamaze huku wakimwita msaliti. Inashangaza namna shule za misheni zilivyowatengeneza watumishi wa serikalini walio wasomi wawe watiifu na waaminifu kwa dola. Wasomi hawa mara nyingi walijikuta wanasigana na wale waliokuwa wakipinga ukoloni na udhalimu.

Mchauru alishindwa kutambua hali halisi iliyokuwapo pale sike ile. Mchauru alipuuza zile kelele akaendelea kuzungumza akijaribu kuwasihi wafanyakazi warudi kazini kwao. Ghafla hali iligeuka.

Watu walipandwa na hasira na kusikia wakisema ashikishwe adabu. Watu waliokuwa wamehamaki wakaanza kumsogelea. Salum Abdallah, akiwa kiongozi wa watu wale, alihisi kuwa endapo hatachukua hatua ya kumnusuru Mchauru huenda watu wakamuadhibu.

Alienda pale aliposimama Mchauru. Aliinua mikono yake juu akawataka watu watulie. Salum Abdallah alikuwa mtu wa miraba minne na alikuwa na sauti kubwa.

Wanachama wengi wa TRAU wanamkumbuka kwa sauti yake, hasira zake na kwa umbo lake kubwa. Wafanyakazi walipomuona Salum Abdallah walitulia na Mchauru akaondoka pale kimya kimya kupeleka taarifa kwa hao waliomtuma kuwa watu wamegoma, hawasikii la muadhini wala la mnadi sala…’’

(Kutoka kitabu, ‘’Maisha na Nyakati za Abdulwahi Sykes (1924 – 1968)…’’)

Mwaka wa 1960 Salum Abdallah aliongoza tena mgomo wa wafanyakazi wa Railway uliodumu siku 82. Kwa miezi mitatu treni na mabasi ya Railway yalisimama hadi Waingereza waliposalimu amri na kuwaita viongozi wa wafanyakazi katika meza ya majadiliano.

Uhuru ulipopatikana babu yangu akapambana kwa fikra na msimamo wa Nyerere kuhusu vyama vya wafanyakazi Nyerere akitaka viwekwe chini ya TANU na viongozi wa vyama vya wafanyakazi pamoja na babu yangu wakipinga wazo hilo. Yalipotokea maasi ya wanajeshi tarehe 20 Januari 1964 baada ya maasi kuzimwa na jeshi la Waingereza, Nyerere aliwakamata viongozi wote wa vyama vya wafanyakazi na kuwaweka kizuizini. Babu yangu alizuiwa kwenye jela ya Uyui, Tabora na alipotoka kizuizini Tanganyika Railway African Union (TRAU) chama alichokiasisi mwaka wa 1955 kilikuwa kimepigwa marufuku pamoja na vyama vingine vya wafanyakazi na badala yake kimeundwa chama cha National Union of Tanganyika Workers (NUTA) kwa juhudi kubwa za Rashid Kawawa na Michael Kamaliza.

Babu yangu alihama Tabora na kwenda Urambo kupisha shari kwani zilienezwa taarifa za uongo kuwa yeye alikuwa katika kundi pamoja na Victor Mkello (kiongozi wa wafanyakazi wa mashamba ya mkonge) na Kassanga Tumbo walikuwa wamekula njama ya kupindua serikali na kumuua Rais Nyerere. Babu yangu akajikita katika ukulima wa tumbaku Urambo huku akiendelea na ukulima wake wa miaka yote Kakola na Uyui Tabora.

Fredrick Mchauru aliendelea na utumishi katika serikali ya kikoloni na uhuru ulipopatikana mwaka wa 1961 alishika nyadhifa mbalimbali katika serikali huru kama zilizvyoelezwa katika makala zilizochapwa na Raia Mwema. Kama mimi nisingeaandika kitabu cha Abdul Sykes huenda historia hii ya babu yangu na wazalendo wengine isingejulikana na historia ambazo zingesomwa ndiyo hizi za watu kama Fredrick Mchauru na wengineo.

Salum Abdallah alifariki mwaka wa 1974 akiwa na umri kama miaka 80 akiwa mkimya sana kwa kuwa hapakuwa tena pale mjini na barza zilizokuwa zikijadili siasa kama miaka ya 1950 wakati wa kudai uhuru. Siasa ilikuwa sasa jambo la kutisha watu wakihofu kukamatwa na kuwekwa gerezani. 

Babu yangu akiungulia ndani kwa ndani kwa chuki dhidi ya TANU chama alichokiendea mbio na kuhudhuria mikutano yake yote ya siri mwaka wa 1953 pamoja na wazee wenzake akina Maulidi na Abdallah Kivuruga, Rajab Saleh Tambwe, Abubakar Mwilima kuwataja wachache,  na kuwa mmoja wa waasisi wake mjini Tabora mwaka wa 1955.

Siku zote yeye baada ya kuona vyama vya wafanyakazi vimekwa chini ya TANU na serikali yake aliwaona viongozi wapya wa vyama hivi vibaraka wa serikali hawataweza kupigania haki za wafanyakazi kwa dhati.
Post a Comment