Saturday, 24 February 2018

IKO WAPI TANGA ILE? HASSAN R HASSAN


IKO WAPI TANGA ILE?
Tanga ya zamani zile, ya jagina Shaabani
Aliyesifika kule, na kote Uswahilini
Mbona kama izamile, haipo kwenye ramani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga yake Jinamizi, Sheikih Ali Zakuwani
Ilo ikikaza uzi, kwa mambo yenye thamani
Imegota zake mbizi, nani wa kuiauni?
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Mwalimu Pera, Pera bin Ridhiwani
Zama zake iling'ara, na kushika usukani
Doro leo yadorora, haitajwi midomoni
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Mdanzi, wa Hanasa muhisani
Iloenea mapenzi, na baraka tani tani
Ya sasa ni kama bunzi, makaziye jalalani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Mwinyihatibu, Mohamedi nambawani
Aloandika vitabu, vizuri vyenye maani
Mbali imejitanibu, haipo hatuioni
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Ghulamu, Mwabondo mtu makini
Aloifunza kaumu, ushairi pamwe dini
Umekwisha umuhimu, Tanga sasa Tanga duni
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Hemedi, Buhry wa Mnyanjani
Ilolea auladi, kwa kumcha Rahmani
Imeenda hairudi, imakeni hii shani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Salimu, Kibao niambieni
Iko wapi waadhamu, nikaishufu kwa mboni
Nikajifunze nudhumu, nikiwamo Tanga ndani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Saidi, Nuru aso mshindani
Ilopendwa ja waridi, au vile asumini
Hae! Imezama sudi, bahati si mara thani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga yake Sheikh Ali, Hemedi mwanachuoni
Iliyotajika mbali, Ulaya na Arabuni
Leo imelala chali, waruka watu na nyuni
Iko wapi Tanga ile?

Tanga yake Mohamedi, Ali Buhry mwendani
Aliyekuwa stadi, na fasaha wa uneni
Ilo sasa si ya jadi, ya jadi i wapi kwani?
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Kigamba, gwiji la Chongoleani
Iliyotoa miamba, waloongoza safuni
Kwa umbuji walitamba, kilugha hata kifani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Sheikh Kihere, Kihere wa Vibambani
Ilotamba si kwa sare, ingiapo shindanoni
Hadi wakaona gere, kina fulani fulani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga yake Abdalla, wa Baruwa Baruwani
Iliyokosa kulala, kwa kukirimu wageni
Watu wakanywa na kula, kindugu na kijirani
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya Mwalimu Mbega, yeye kwake ujombani
Wa kuiga wakaiga, kwa mazuri kusheheni
Tangu yahame mafiga, hakuna chungu jikoni
Iko wapi Tanga ile?

Tanga ya bin Matunga, Abdi alo rubani
Ilojaliwa malenga, mwambao huu wa Pwani
I wapi nende ienga, nikumbukie zamani
Iko wapi Tanga ile?

I wapi ile i wapi, Tanga ile nijuzeni
Imebadilika vipi, toka juu kuwa chini
Na warithiwe wa kupi, walipo nionesheni
Iko wapi Tanga ile?

Hassan R Hassan

Post a Comment