Sunday, 11 February 2018

MAISHA YA MWINYI BARAKA: MAADHIMISHO KARNE MOJA TOKA KUZALIWA SEHEMU YA PILI NA HAMZAH RIJAL


Masheikhe wetu: Sayyid Omar Abdalla (Mwinyi Baraka)
Sehemu ya (2)
Na Ben Rijal
Katika makala haya ya leo yatamuangalia Sayyid Omar Abdalla katika kuendelea kusoma na kazi alizozifanya alipokuwa bado yupo Zanzibar, sio kitu cha kawaida katika Wasomi wengi wa Kiislamu kwenda nazo sambamba elimu ya dunia na elimu ya dini. Sayyid Omar Abdalla alielimika na elimu zote mbili hizo aidha alikuwa akijisomea vitabu mbalimbali na majarida katika kuendeleza uwezo wake kielimu.

            Katika makala ya wiki iliopita nilianza kwa kunukuu misitari miwili mitatu ya Kiengereza kwa yule aliojuwana na Sayyid Omar Abdalla na leo aidha nitaanza hivyo hivyo na mistari miwili mitatu alioyaandika yeye mwenye Sayyid Omar Abdalla.
            Dear Mr. Harvey, I have just received your circular in connection with Religious Teaching in School. Thank you very much. During the last vacation I resumed my discussion with the Chief Kadhi and at the end we arrived to a definite conclusion which I am sure you would like to hear. Since the beginning of the term I have been trying to come and see you at your office but in vain, as I am very busy throughout the week including Saturday. Could you kindly therefore fix me up on any one convenient Sunday so that I might come to see you in your home? Your sincerely, Omar Abdalla (Kumbukumbu  ZNA AD 3/8). Tafsiri ya juu juu kutokana na Faili lake lenye nambari ZNA 3/8  akimuandikia Mkurugenzi wa elimu Mr. Harvey akimwambia, “Nashukuu  kuwa nimepata chapisho ulionitumia kuhusu usomeshwaji wa masomo ya dini katika maskuli. Katika mapumziko yangu bada ya mhula wa masomo  nilishafanya mazungumzo juu ya masaala hayo na Kadhi Mkuu ambaye tulifikia makubaliano,  imani yangu kuwa wewe Mkurugenzi wa Elimu utapenda kusikia juu ya mazungumzo hayo. Nilijitahidi kupiga hodi kwenye ofisi yako pasi mafanikio, ikiwa na mie nimebanwa na mashughuli kwa wiki nzima pamoja na Ijumamosi yake, nitaomba uitenge siku ya Ijumapili tuweze kuonana.  Wako mtiifu. Omar Abdalla.”
            Nitapenda kugusia jambo mmoja muhimu sana ambalo katika utawala wa Muiengereza uliweza kusaidia sana katika uwekaji wa kumbukumbu. Ilikuwa Maofisa wote wa Serikali wakitakiwa taarifa zao kuhifadhiwa katika mafaili maalumu kisha kuwekwa kwenye ofisi ya nyaraka (Archives).
            Ilikuwa ofisa yoyote akipandishwa cheo, akiongezwa mshahara, akipata uhamisho barua atakayopewa lazima ikawekwe kwenye faili lake huko ofisi ya nyaraka na mpelekaji wa taarifa hizo ni tarishi ambaye kila mtu akimjua kama ni tarishi au kwajina hilo la zama hizo akiitwa Ofisi boi, kwani akivaa shati na surula ya khaki na baskeli yake nyekundu.
            Ofisi boi akijivunia kazi hio kwani ilikuwa siku hizo ukiwa mfanya kazi wa Serikali basi maisha yako utayaweza kutokana na mshahara unaolipwa. Taarifa nyingi za waliopita tunaweza kuzipata kwa njia hio ambazo kwa leo ni kitu kigumu kuweza kuzipata taarifa za wafanya kazi mbalimbali.
            Aidha katika sehemu hio ya kumbukumbu utaweza kupata taarifa za kila aina, hata zile za magazeti yaliopita ambayo kila nakala iliokuwa ikitolewa hupelekwa hapo na kuwekwa.
Sayyid Omar Abdalla akiwa na Masheikhe na walimu mbalimbali hapo Ukutani
            Sayyid Omar Abdalla akiwa amerudi kusoma Makerere College huku anasomesha, alikuwa ansubiri nafasi ya kwenda kuongeza masomo kwa hamu huko nchi za nje, kama nilivyokwisha kueleza kabla  kuwa Sayyid Omar alikuwa kati ya wanafunzi wa mwanzo kusoma masomo ya Sekondari viiswani Zanzibar aidha alikuwa kati ya wanafunzi wa mwanzo wa kwenda kusoma masomo ya juu katika Chuo cha Makerere.
            Ilipofika mwaka wa 1951 Sayyid Omar Abdalla na Abdalla Jahadhmi walikuwa wanafunzi wawili waliopata fursa ya kwenda Uiengereza kwa masomo ya juu. Sayyid Omar Abdalla alikwenda chuo cha SOAS kufanya masomo ya Ulinganisho wa dini pamoja na Kiarabu.
            Kuna mapendekezo mengi ambayo watawala wa Kiengereza walikuwa wakijadiliana katika uongozi wa elimu pamoja na mahusiano ya mambo ya nje juu ya kumsomesha Sayyid Omar Abdalla ili aweze kuja kuwa Mwalimu Mkuu wa Chuo cha Kiislamu ambacho kilikuwa katika katika mataarisho ya kufunguliwa mwisho wa miaka ya 40.
            Sayyid Omar Abdalla alikuwa akitamani kwenda kusoma nchi za Kiarabu lakini fursa ilipomuangukia ya kusoma Uiengereza kufanya masomo ya Ulinganisho wa dini ngazi ya Shahada ya Diploma hakusita akakubali, huku akijuwa kuwa atakuwa na pengo katika kuzungumza Kiarabu, ingawa akizungumza Kiarabu lakini sivyo namna alivyokuwa akitamani mwenyewe kukimudu hicho Kiarabu. Wengi wa watu wa visiwani siku hizo katika maisha yao ya kujifunza Msikitini tangu utotoni hadi utuzimani mwao walikuwa wakizungumza Kiarabu lakini wenyewe wakikiita Kiarabu cha Msikitini.
Ahlil Darsa wa Msikiti wa Ijumaa mdogo
            Alipokuwa anafanya masomo yake hayo hapo Uiengereza alipewa magwiji wawili ambao kazi yao ilikuwa kuhakikisha analifikia lengo lilokusudiwa, akisimamiwa na mjuzi wa elimu ya Ulinganisho wa dini David Cowan (al Dundawi) na R. B. Serjeant inagawa msimamizi mwengine alimkataa kumsimamia na kujiunga na chuo hicho alikuwa  ni J.N.D Anderson.
            Akiwa anasoma huko Uingereza alikuwa akiwasiliana na wanafunzi wa maeneo mbalimbali kuweza kupata kwenda kujiendeleza bada ya kukamilsiha masomo yake na khasa alilenga kuweza kupata fursa ya kwenda kujiendeleza katika nchi za Kiarabu na za Kiislamu.
            Ilipofika mwaka wa 1953 akiwa bado yupo Uiengereza alifanya safari ya kwenda Marekani na kuhudhuria mafunzo ya nyakati za kiangazi, masomo ya muda mfupi, huku akiwa amefanya aridhilhali ya kupata kwenda kusoma masomo ya Kiarabu.
            Hakuchoka kuandika na kuwataka Waiengereza wamlipie masomo yake katika nchi za Kiarabu kitu ambacho katika siku zake za utuzimani bada ya kuondoka Zanzibar hakuwa ni mtu wa kushikilia jambo analolitaka ila akipenda kuona ajiachie na aone upepo utavyomchukua utakavyo.


Sayyid Umar bin Sumayt na Sayyid Omar Abdalla
             Akiwa bado yupo huko Uiengereza na kiu chake kutaka kujiendeleza masomo yake katika nchi za Kiarabu, hakuona tabu kukamata kalamu na kuandikia Wizara ya elimu, aliandika lugha nzito yenye ufasaha na unapoisoma barua hii utaona namna alivyokuwa akikimudu Kiengereza.
            “Sir, you may be pleased to hear that I have done well in my examination, and next year I hope to complete my course. I must thank the government for affording me the unique opportunity, being the first and the only student in the course. I am becoming a learned man. But you will agree that however high the standard   of knowledge I get here, I shall not be really competent to hold any post involving the use of Arabic or Islamic law unless I spend some time in a country where Arabic is the language, and where Islam form the background of the people. Here, there is no proper atmosphere. My stay in Arabia will be a shield against those who criticize my coming to London. It will give me a greater confidence, and I confess that I shall not completely qualified for a responsible position without actual living in Arabia” (kumbukumbu ANA AB 86/47, barua alioiandika tarehe 30.6.1953)
            Kwa kifupi aliandika barua kusema kuwa amemaliza masomo yake na amefanya vizuri ni vyema sasa wakampatia fursa ya kwenda kuongeza msomo yake katika nchi za Kiarabu, kufanya hivyo kutawafunga midomo wale watakao bwabwaja kuwa elimu yake kaipata Ulaya, ila tu kukosa kwenda kufanya mafunzo katika nchi za Kiarabu zenye utamaduni wa Kiislamu basi hatokuwa na uwezo wa kukamata nyadhifa kubwa za kitaaluma.
            Katika mwaka wa 1954 Sayyid Omar Abdalla aliandika barua ya kukumbusha azma yake ya kupata fursa ya kuendelea kusoma katika nchi za Kiarabu na Kiislamu na alitaka kuwa akiwa anarudi kutoka Uiengereza apewe ruksa ya kwenda Kuhiji Makka kisha apite Hadharmout huko Yemen akae kidogo ajifunze kwa Kiarabu masomo aliokwisha kuyasoma kisha ndio arudi nyumbani, alikubaliwa hilo na safari yake alilipiwa na Serikali.
            Kuna kumbukumbu ambayo sijaipata lakini niliisikia kuwa alipokwenda Makka na kupita Hadahrmout alichelewa kwa siku 2 kurudi Zanzibar kwahio alikatwa mshahara wa siku 2 lakini hapo hapo kutokana na kufanya vizuri masomo yake alipandishwa cheo na kupatiwa nyongeza ya mshahara.
Sayyid Omar Abdalla akiwa na Masheikhe na walimu mbalimbali hapo Ukutani

          Fatwana na mie katika makala inayofwata kumuangalia Sayyid Omar Abdalla akiwa amerudi masomoni kazi zake na kuhama Zanzibar kuhamia visiwa vya Comoro.  
Post a Comment