Saturday, 21 April 2018

NAMKUMBUKA: SHEIKH YUSUF SALUM

Sheikh Yusuf Salum

Maneno hayo hapo chini nimeyaandika majuma matatu yaliyopita katika moja ya group zetu tukijadili jinsi Waislam wanavyokosa nafasi katika utawala kiasi kutoa picha kama vile hakuna Waislam wenye sifa za kutosha kuweza kushika nafasi hizo:
‘’...hoja unazo lakini tujaaliwe hakuna (Waislam wenye elimu). Hapa tujiulize kwa nini hakuna. Ikiwa hakuna Waislam waliosoma jibu ni jepesi nalo ni kuwa Waislam tunabinywa kwenye elimu na hili tumeshaieleza serikali toka 1980s...ndani ya barua ya Warsha kwa Waislam, Wabunge na Serikali...mimi ndiye nilibeba upupu ule nikenda kuumwaga Karimjee Hall siku hizo Bunge linakutana hapo. Upupu tuliudurufu Masjid Quba. Hela ya kununua karatasi hatuna tulipokuwa njiani tunahangaika tukakutana na mtu baada ya kumueleza shida yetu akatuchukua hadi ofisini kwake akatupa karatasi...’’

Haukupita siku tukavamia Bunge Karimjee Hall baada ya Sala ya L’Asr kimya kimya tukitokea upande wa Independence Avenue na upupu wetu, tukaanza kuumwaga katika magari yaliyokuwa yameegeshwa nje.

Kisha taratibu tukaingia ndani ya viwanja vya Bunge na kuendelea na kazi yetu. 

Taratibu na kimya kimya kama tulivyoingia ndivyo tulivyoondoka katika viwanja vya Karimjee Hall.

Ilikuwa siku ya Ijumaa.
Mjini katika misikiti yote inayoswaliwa Ijumaa waraka ule wa Warsha uligawiwa misikitini.

‘’Upupu,’’ ulikuwa unakwenda kwa Waislam Wote wa Tanzania, Wabunge na Serikali.

Katika waraka ule Warsha walieleza kuwa ipo njama ya kuwabana viijana wa Kiiislam katika elimu na takwimu zikaonyeshwa katika ule ‘’upupu,’’ kuwa Waislam wako wengi katika shule za msingi lakini kuelekea sekondari idadi yao inapunguzwa kiasi ikifika Chuo Kikuu Waislam idadi yao inakuwa haivuki asilimia 10.

Haya yakiwa yanafanyika kwa miaka yote toka uhuru wa Tanganyika upatikane mwaka wa 1961.
Waraka huu wa Warsha ulimwagwa nchi nzima kwa wakati mmoja.

Waraka huu ulisababisha mshtuko mkubwa ndani ya Bunge na katika Serikali lakini hakuna aliyetaka ijulikane kuwa Waislam wametoa Waraka huo.

Nimepokea kwa masikitiko  taarifa ya msiba wa Sheikh Yusuf Salum.

Ndugu yetu marehemu Sheikh Yusuf Salum wakati ule miaka ya mwanzo 1980 akiwa kijana mdogo kama tulivyokuwa sote alisaidia sana pale Masjid Quba katika utayarishaji wa waraka huu.

Mwenzangu alimpa jina Sheikh Yusuf akimwita, ''Mass Support,'' lakini yeye mwenyewe hakujua kama kapewa lakabu hiyo.

Ikawa kila tunapomzungumza tukilitaja jina hilo na naamini Sheikh Yusuf kaondoka duniani halijui jina hili.

Allah amghufirie dhambi zake na amuingize mahali pema peponi.
Amin.

Maziko ya Sheikh Yusuf Salum Makaburi ya Mwinyimkuu


Post a Comment