Sunday, 15 April 2018

SALUM MPUNGA NA YUSUF CHEMBERA MARAFIKI WAASISI WA TANU LINDI

Salum Mpunga

Yusuf Chembera
Akiwa Mayor wa Lindi Town Council


SHUKRANI

Ninatoa shukrani kwa waasisi wa walioleta mabadiliko ya siasa katika sehemu za kusini ya Tanganyika, Said Alley Mwalimu, Mohamed Ali Abdallah ‘’Makarios,’’ wote wawili wanatoka Mikindani; na kwa Salum Mpunga na Yusufu Chembera kutoka Lindi. Wote hawa sasa ni marehemu. Watu hawa wamenisaidia sana kwa kunieleza maisha yao katika siasa wakati wa ukoloni katika majimbo ya kusini.

SALUM MPUNGA NA YUSUF CHEMBERA
MARAFIKI WAASISI WA TANU LINDI

Vita vya Maji Maji vilipoanza kusini ya Tanganyika mwaka 1905 kwa nia ya kuwafukuza Wajerumani kutoka Tanganyika, zile sehemu zenye Wakristo wengi zilikataa kujiunga na vita na badala yake wakajiunga na majeshi ya Wajerumani na kupigana bega kwa bega na dhidi ya wazalendo. Hii ilitokana na sababu ya kuwa uasi dhidi ya dhulma wa Wajerumani ulianza katika maeneo yenye Waislam wengi na vita vikachukua sura ya vita vya Kiislamu dhidi ya Wazungu ambao dini yao ni Ukristo. Kwa kuwa wamishonari walikuwa washirika wa wakoloni, walichukuliwa kama maadui na hivyo ikawa vituo vyao vinashambuliwa na wapiganaji wa Maji Maji. Kutokana mashambulizi haya, Wakristo walivichukua Vita Vya Maji Maji kama vita dhidi ya Ukristo. Harakati za Maji Maji zilishindwa na Wajerumani walifanya fisadi kubwa dhidi ya wananchi na viongozi wao. Jambo hili liliacha kovu kubwa katika fikra za wananchi na kwa upande wa Wakristo ambao walinusurika na ghadhabu ya Wajerumani, wengi wao wakajiweka mbali na aina yoyote ya kupinga ukoloni.

Kufuatia historia hii Waafrika waliokuwa kusini ya Tanganyika sasa wakiwa chini ya utawala wa Waingereza na kuwa chini ya himaya ya wamishonari walipumbazwa kiasi kiasi kwamba waliogopa siasa. Baada ya Waafrika kushindwa vita kwa silaha kali za Wazungu sasa Kanisa likaona ndani ya fadhaa ile fursa yao kutawala sehemu hiyo kwa kutoa vishawishi kama vile shule na hospitali. Kwa hiyo Wamishionari na Waingereza walionekana kama mabwana wema wenye kuwajali raia zao kinyume na serikali katili na ya kidhalimu ya Wajerumani. Vuguvugu la siasa kama ilivyokuwa Vita vya Maji Maji, lilianza katika maeneo ya Waislam kufuatia mfumo ule ule kama ilivyokuwa katika upinzani wa ukoloni wa Wajerumani. Wakristo katika Jimbo la Kusini waliiona TANU kama walivyoviona Vita Vya Maji Maji, kama harakati nyingine za Waislam zilizowa zinakuja tena kwa mara ya pili kuvuruga amani na utulivu. TANU ilipoanza ikawa inavuma kuwa safari hii Waislam walikuwa wamemua kuanzisha vita dhidi ya Waingereza kama walivyoanzisha vita na Wajerumani.

TANU ilipoanzishwa mjini Dar es Salaam na hisia za utaifa zilipokuwa zikipanda pole pole katika fikra za wananchi katika sehemu nyingi za Tanganyika, Jimbo la Kusini lilikuwa bado usingizini likiishi  katika zama za kale. Mnonji na Waziri, kwa sababu ya utu uzima wao, daraja yao katika jamii na hasa kutokana na kuhusika kwao katika siasa za pale mjini, walikuwa na nguvu kubwa katika TAA. Wakati TANU imeshachukua nafasi ya TAA, uongozi wa TAA Lindi haukutaka kufungua tawi la TANU. Mtu wa kwanza kuutanabaisha uongozi wa TAA mjini Lindi juu ya mageuzi yaliyokuwa yakitokea Tanganyika na kuanzishwa kwa chama kipya cha siasa mjini Dar es Salaam alikuwa Abdallah Juma Makopa, kijana kutoka Tanga akifanya kazi ya ukarani Posta ya Lindi. Makopa aliwaendea Mnonji na Waziri na kuwajulisha kuhusu kuanzishwa kwa TANU mjini Dar es Salaam na aliwashauri waanzishe TANU pale Lindi. Jambo hilo lilipingwa moja kwa moja na Mnonji, Waziri, Said Nassoro, Abdallah Mhuji na wanachama wengine wa TAA.

Chama cha Waafrika ambacho kilianzishwa siku nyingi mjini Lindi na kwa hakika ndicho kilikuwa chama cha pekee kushughulikia maslahi ya Waafrika sehemu za kusini kilikuwa African Welfrare Association ambacho mlezi wake alikuwa John Nevi, Mjaluo kutoka Kenya na katibu wake alikuwa Casian Njunde, Mngoni wa Songea. Makopa aliposhindwa kukishawishi kile kikundi cha wazee wa TAA aliwaendea Yusufu Chembera na Rashid Salum Mpunga. Chembera alikuwa na umri wa miaka 34 na Mpunga alikuwa kijana wa miaka 27. Chambera alikuwa amesoma hadi shule ya msingi na Mpunga alikuwa amemaliza madras. Chembera alikuwa akifanya kazi katika kantini ya Lindi Welfare Centre, wakati Mpunga alikuwa dereva wa lori aliyeajiriwa na mfanyabishara wa Kihindi. Makopa aliwashauri Chembera na Mpunga juu ya uwezekano wa kuwahamasisha wananchi wawaunge mkono ili tawi la TANU lifunguliwe pale mjini. Aliwaambia alitaka sana kufanya hivyo yeye mwenyewe lakini asingeweza kwa sababu yeye alikuwa mtumishi wa serikali na hakuwa akifahamika sana mjini. Uongozi kama wao ndiyo ungeweza kuaminiwa na wananchi na usingetiliwa mashaka. Makopa, Chembera na Mpunga walikubaliana kuwa kabla ya kuanza kufanya kampeni waziwazi kwa ajili ya TANU, lazima wawaandikishe wanachama wachache kama waasisi wa chama. Mpunga na Chembera walimwandikisha kijana mmoja akiitwa Abdallah Faraj na katika muda mfupi waliweza kuwapata takriban wanachama kumi na tano walioridhia kujiandikisha kama wanachama waasisi wa TANU.

Baada ya kuandikisha wanachama waasisi mkutano wa siri uliitishwa katika Welfare Centre ambako ndiko alikokuwa akifanya kazi Chembera. Chembera aliwaeleza kwa ufupi wale wanachama wa mwanzo kuhusu malengo na madhumuni ya chama hicho kipya cha siasa. Mkutano huo ulichagua kamati ya watu watatu yaani, Makopa, Chembera na Faraj ili kuwakabili Mnonji na Waziri kuwaleza kuwa TAA haipo tena nchini Tanganyika. Lengo lilikuwa kuwasadikishia kuwa ilikuwa kazi bure na kupoteza wakati kujaribu kuihuisha TAA mjini Lindi wakati ambapo Tanganyika nzima ilikuwa ikisonga mbele na TANU. Baada ya mjadala mrefu sana na mkali wa wale vijana watatu na ule uongozi wa TAA wa wazee, walikubaliana TANU lazima isajiliwe mjini Lindi.

Uchaguzi ulifanyika na Shaaban Msangi, kijana wa Kipare akifanya kazi kwa Smith Mc Kenzie, alichaguliwa rais na Ahmed Seif, katibu. Mpunga, Chembera, Mnonji na Idd Toto walichaguliwa wajumbe wa kamati. Ahmed Seif alikuwa kijana ambaye ndiyo kwanza amemaliza shule, yeye alikabidhiwa kuendesha ofisi kwa niaba ya uongozi.  TANU mjini Lindi ilimwajiri ili kukiandaa chama kiweza kufanya kazi zake kwa ufanisi. Hassan Mohamed Kinyozi aliajiriwa kama mhudumu wa ofisi. Hawa wawili walikuwa ndiyo wafanyakazi wa kwanza wa TANU waliokuwa wakilipwa mshahara katika Jimbo la Kusini na wakawa miongoni mwa wafanyakazi wachache sana walioajiriwa na TANU kwa wakati ule. Mnonji alitoa nyumba yake katika mtaa wa Makonde kuwa ofisi ya kwanza ya TANU Jimbo la Kusini. Baada tu ya kuanzishwa kwa TANU, Athumani Mussa Lukundu, kiongozi wa Lindi Dockworkers’ Union, aliunganisha chama chake na TANU. Jambo hili, kwa TANU lilikuwa la kuitia moyo sana kwa sababu Dockworkers’ Union ilikuwa na wananchama wengi na hatua ile iliongezea TANU nguvu.
                                                                                   
Baada ya muda mfupi tu toka kufunguliwa kwa TANU Mkutano Mkuu wa Kwanza wa TANU wa mwaka 1955 ulifuatia. Tawi la Lindi lilikuwa tayari lina uhusiano na makao makuu ya TANU mjini Dar es Salaam, na lilikuwa likitarajia kuhudhuria mkutano huo na kukutana na Julius Nyerere na uongozi mzima wa TANU pale makao makuu Dar es Salaam. Mpunga, mwanachama muasisi wa TANU, na Ali Ibrahim Mnjawale waliteuliwa kuhudhuria mkutano huo kama wajumbe kutoka Jimbo la Kusini. Halmashauri ya TANU ya Lindi iliwaelekeza wajumbe hawa wafikishe ombi rasmi kwa makao makuu ili Julius Nyerere aje kufanya ziara kusini kwanza, kukutana na wananchi na kufanya kampeni kwa ajili ya TANU na pili aje kupambana na propaganda dhidi ya TANU zilizokuwa zikitawanywa na Yustino Mponda.  Mponda akitumia uhusiano wake na serikali ya kikoloni na nafasi yake kama mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria kutoka Newala; na vilevile akitumia ushirikiano wake wa muda mrefu na kanisa ambao bila shaka yoyote lilikuwa serikali ndani ya serikali kule kusini, alikuwa ameanza kampeni yake ya kuipinga TANU. Hili lilikuwa likiathiri msukumo wa uanachama. Mponda alikuwa mmoja wa wajumbe waliotumwa na Gavana Twining kwenda Umoja wa Mataifa Februari, 1955 kwa niaba ya serikali ya kikoloni kwenda kuipinga. Uongozi wa TANU huko Lindi ulitaka Nyerere aende kupambana na Mponda akiwa katika uwanja wake mwenyewe, ndani kabisa ya ngome ya Ukristo wa Kikatoliki katika Tanganyika.

Mkutano mkuu wa mwaka wa TANU ulifanyika katika ukumbi wa Hindu Mandal mjini Dar es Salaam. Siku kabla ya mkutano TANU ilimwalika Gavana Edward Twining kwenye tafrija katika Ukumbi wa Arnatouglo lakini alikataa kistaarabu na akamtuma Chief Secretary, Bruce Hutt, kumwakilisha. Baada ya mkutano, wakati wajumbe wengine wanaondoka kurudi kwenye majimbo yao, Mpunga na Mnjawale walibakia nyuma kukutana na uongozi wa makao makuu wa Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe, Said Chamwenyewe, Oscar Kambona na wengineo. Mpunga na Mnjawale waliwafahamisha viongozi wa makao makuu kuhusu hali mbaya ya siasa Jimbo la Kusini. Mbali na kampeni za kuipinga TANU za Mponda, katika ziara yake Lindi Gavana Twining aliwatahadharisha Waafriika wa Tanganyika wasijihusishe na ‘’wafanya fujo wanaotaka kuzusha vurugu.’’ Twining alikuwa akitoa onyo hili akiikusudia TANU ambayo ilikuwa imeanzishwa mwaka uliopita. Hotuba hii ya Gavana iliwatisha wananchi kujiunga na TANU. Mpunga na Mnjawale walisisitiza kuwa kuja kwa Nyerere mjini Lindi kulitakiwa haraka sana kukabiliana na vyote viwili, kwanza ile hotuba ya gavana na pili zile kampeni za kupinga TANU zilizokuwa zikiendeshwa na Liwali Yustino Mponda.

Wakati huo Abeid Amani Karume aliyehudhuria ule mkutano alimwalika Nyerere afanye ziara Zanzibar. Kitu cha kustaajabbisha ni kuwa, Nyerere alionekana kuiafiki zaidi ziara ya Zanzibar kuliko ile safari ya kwenda kusini kuiimarisha TANU. Mpunga alimsisitizia Nyerere umuhimu wa yeye kwenda Lindi ambako kunaweza kuwa ndiyo chanzo cha TANU kupata ufanisi Newala, Songea, Tunduru na Masasi ambako kulikuwa na upinzani mkubwa dhidi ya TANU. Kanisa lilikuwa likiwazuia Wakristo kujiunga na TANU. Sheikh Suleiman Takadir, Said Chamwenye, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe wote waliunga mkono ule ujumbe wa Lindi juu ya suala hili. Baada ya kufikia makubaliano, Mpunga na Mnjawale walipewa barua ya kuthibitisha safari ya Nyerere.  Ziara ya Nyerere ilikuwa ianze muda mfupi kutokea hapo kwa kuwa ilikuwa ndiyo siku za mwisho za kiangazi. Barabara sehemu ya kusini ya Tanganyika zilikuwa hazipitiki wakati wa masika, zikiitenga kabisa kusini toka sehemu zilizobaki za nchi. Ali Mwinyi Tambwe na Rajab Diwani walifuatana na Nyerere kwenda Jimbo la Kusini kuondoa wasiwasi na woga uliozushwa na Gavana Twining na kibaraka Yustino Mponda.

Nyerere na msafara wake ulipokelewa na uongozi wa TANU wa Lindi huko Mbanji, kijiji kidogo nje ya mji. Msafara wa Nyerere ulipowasili Mbanji ilikuwa kiasi cha saa moja jioni hivi na giza lilikuwa linaanza kutanda. Mbali na Mpunga na wale wajumbe wawili waliokutana na Nyerere mjini Dar es Salaam mwezi uliopita, hakuna hata mtu kati ya umma ule uliokuja kupokea ujumbe kutoka makao makuu ya TANU aliyekuwa anajua Nyerere anafanana vipi. Mpunga, dereva wa lori, alijibagua kutoka kwa lile kundi la watu akawa amesimama pembeni ili Nyerere apate kumuona. Baada ya Nyerere kumtia Mpunga machoni, Mpunga alimwendea kumsalimu Nyerere, Tambwe na Diwani; kisha aliligeukia lile kundi la watu kumtambulisha Nyerere kwa wananchi akilitaja jina lake kwa sauti kubwa. Baada ya hapo aliutambulisha ule ujumbe wa Nyerere. Nyerere na ujumbe wake ulisindikizwa kwa shangwe na kundi la watu hadi ofisi ya TANU kwenye nyumba ya Mnonji. Kupakana na ofisi ya TANU ilikuwepo nyumba ya seremala mmoja, Issa bin Ali Naliwanda. Hii ndiyo nyumba iliyochaguliwa alale Nyerere na ujumbe wake, si kwa sababu ilikuwa nzuri kupita zote. Ilichaguliwa na kupewa heshima hii kwa sababu ilikuwa karibu sana na ofisi ya TANU na hivyo basi ilirahisishia TANU kazi ya ulinzi wa Nyerere. Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili na Nyerere aliwaomba wenyeji wake apelekwe kanisani kwa ajili ya ibada.

Kanisa Katoliki mjini Lindi ni jengo la fahari lililoko ufukweni katika Bahari ya Hindi. Lindi ulikuwa mji wa Waislam. Mbali na mlio wa kengele za kanisa hakuna mtu pale mjini aliyekuwa akishughulishwa na kile kilichokuwa kikifanyika kwenye viwanja vya kanisa. Watu wachache waliokuwa wakienda kusali kanisani walikuwa Wakristo waliokuja Lindi kutoka sehemu nyingine za Tanganyika kufanya kazi katika ofisi za serikali. Ghafla mahala hapa palipokuwa pweke, palipopuuzwa kwa miaka na Waislam wa mjini, pakawa muhimu kwa sababu rais wa TANU ambae alikuwa Mkatoliki alikuwa na haja ya kuhudhuria ibada pale kanisani. Hakuna mtu katika uongozi wa TANU wa Lindi aliyejua ndani ya kanisa lile kulikuwa vipi wala hapakuwa na yoyote kati yao aliyewahi kuingia ndani ya kanisa, si Lindi wala mahali popote pale. Uongozi wa TANU wa Waislam mjini Lindi haukumwamini Mkristo yoyote kumsindikiza Nyerere kanisani ili kumpa ulinzi. Baada ya kujadili suala hilo kwa urefu hatimaye iliamuliwa kuwa  Mpunga na wanachama wachache Waislam wenye kuaminika lazima wamsindikize Nyerere kanisani na wengine wabakie nje kulinda mlango.

Jumapili hiyo Nyerere aliingia ndani ya kanisa Katoliki mjini Lindi akifuatwa nyuma na walinzi wake Waislam wakiongozwa na Salum Mpunga, dereva wa lori shupavu. Misa hii ‘’maalum’’  ilidumu katika fikra za wale Wakristo waliokuwepo pale kanisani kwa miaka mingi kwa kuwa tukio hilo liliwagusa sana Wakristo walioshuhudia mkasa ule ndani ya kanisa la Lindi. Hii huenda ilikuwa mara ya kwanza na ya mwisho kwa Nyerere kumsalia Mungu wake huku akiwa amesimamiwa na Waislam.

DC mkoloni alikataa kutoa kibali kwa TANU kufanya mkutano wa hadhara. Akiwa amekasirika sana, Shabaan Msangi aliitisha mkutano wa dharura wa tawi uliohudhuriwa na Nyerere na Tambwe. Baada ya mkutano huo Tambwe alikwenda kumwona DC. Ruhusa ilitolewa, na adhuhuri hiyo siku ya Jumapili, katika kiwanja ambacho Wazungu walikuwa wakicheza gofu, ambako mwaka mmoja uliopita Gavana Edward Francis Twining alitoa hotuba iliyowavunja moyo Waafrika, Nyerere alihutubia mkutano wa hadhara. Kamwe haijapata kutokea kabla ya siku ile katika historia nzima ya Jimbo la Kusini, watu wengi kiasi hicho kujumuika mahali pamoja. Wazungu na Wahindi pamoja na askari, watu wakiwa wamekaa na wengine wamesimama katika ya jua kali walikuja kumsikiliza Nyerere akihutubia. Ili kuhakikisha amani na usalama pale mkutanoni serikali iliweka askari waliouzunguka uwanja mzima wa mkutano. Nyerere aliwafikishia watu ule ujumbe wa TANU wa kuwa, kutawaliwa ni fedheha, na Waafrika wa Tanganyika lazima wadai uhuru wao. Uingereza ilikuwa ikiitawala Tanganyika chini ya udhamini kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, na wakati ukiwa muafaka inabidi Uingereza ikabidhi nchi kwa wananchi wenyewe. TANU ilikuwa imewasili Jimbo la Kusini.


Tangu mwaka 1954 tetesi za chama cha siasa kilichoanzishwa Dar es Salaam kupigania uhuru zilikuwa zimepenya na kufika Mikindani, mji mdogo kusini mwa Lindi. Huko Mikindani kama ilivyokuwa mjini Lindi, harakati za utaifa zilianzia kwa wakazi wa mjini, Wamakonde wengi wao wakiwa Waislam. Kinyume na imani ya watu wengi kuwa Wamakonde ni wapagani, Wamakonde pekee waliokuwa si Waislam walikuwa wale waliokuja kutoka Msumbiji, koloni la Wareno. Hawa ni Wamakonde waliovuka mto Ruvuma kuingia Tanganyika kutafuta kazi katika mashamba ya mkonge kama manamba. Uislamu ulikuwa umeimarika Kilwa na sehemu nyingine za pwani kwa zaidi ya miaka elfu moja. Wamakonde wasio Waislam wanaweza kutambulika kwa chale walizochanja katika nyuso zao na ndonya kwa wanawake wao. Wamakonde wa Tanganyika kutoka Lindi, Mikindani na Mtwara katika mwambao wa ukanda wa pwani wa kusini ni kabila la Waislam wengi. Wamakonde Wakristo wanatoka katika maeneo yanayozunguka Masasi ambayo hadi sasa ni eneo la Wamishonari. Wamishonari wa UMCA waliingia Masasi, nchi inayokaliwa na Wamakua na Wamakonde katika mwaka 1876.

Mikindani haikuwa kama Lindi. Lindi ilikuwa kituo cha biashara na utawala wa kikoloni katika Jimbo la Kusini. Lindi ilikuwa na uwanja wa gofu, sinema na kilabu mahususi kwa Wazungu ambayo hakuna Mwafrika au Mhindi aliyekanyaga hapo bila sababu ya maana. Lindi ilikuwa na barabara za lami na mitaa yake iliwashwa taa usiku kuondoa giza. Kadhalika mji ulikuwa na idadi ya kutosha ya Waafrika waliokuwa katika utumishi wa serikali. Wakati huo Lindi ilikuwa manispaa iliyokuwa ikikua na yenye shughuli nyingi. Ikilinganishwa na Lindi Mikindani ilikuwa kijiji kikubwa cha uvuvi kisichokuwa na mambo ya mjini na wakazi wake bado walitumia taa za kandili. Si watu wengi waliokuwa wakihamia Mikindani kutoka sehemu nyingine kuja kutafuta kazi. Uhamiaji wa watu kutoka sehemu nyingine kuja mjini Mikindani ulikuwa katika kiwango cha chini sana. Watu pekee waliokuja Mikindani walikuwa Wamakonde kutoka Newala na Masasi ndani ya Tanganyika na wale kutoka upande wa pili wa mpaka toka Msumbiji. Hawa walikuja kufanya kazi katika mashamba ya mkonge yaliyokuwa yakimilikiwa na ukoo wa Karimjee. Hawa Wamakonde wahamiaji walikuwa wakidharauliwa na wenyeji na kwa ajili hii Wamakonde wakiwa hawana dini walijitenga na wenyeji. Hakukuwa na maingiliano baina ya Wamakonde kutoka koloni la Wareno la Msumbiji na Wamakonde Waislam wa Tanganyika. Wakiwa mbali na nyumbani ambako maisha chiini ya Wareno yalikuwa magumu sana hawa Wamakonde waliangukia chini ya ulezi wa Kanisa.

Ili kuepuka mgongano na Waislam wamishonari walikuwa wamejenga kanisa kubwa sana juu ya kilele cha mlima maili chache toka Mikindani sehemu moja ikijulikana kama Mchuchu.  Karibu na kanisa walikuwa wamejenga shule ambayo Alfred Omari alikuwa akifundisha. Baba yake Alfred alikuwa Mmakua Muislam lakini mwanae alibatizwa kwa ajili ya kupata elimu. Inasemekana Mwafrika wa kwanza kusoma shule ya misheni kule kusini alikuwa Charles Suleiman. Huyu alikuwa kijana wa Kiislamu aliyebatizwa na wamishonari. Alikuja kuwa Mwafrika wa kwanza kufuzu ualimu katika miaka ya mwishoni ya 1800.

Mbali na changamoto hii kwa Uislamu kutoka kwa wamishonari, Mikindani ilibakia kuwa chemchemu ya elimu ya Kiislamu. Mikindani ilijivunia mchanganyiko wa wanachuoni wenye sifa kubwa ndani na nje ya Tanganyika. Elimu ya dini ya Kiislamu ilifundishwa  Mikindani na Sheikh Suleiman bin Said na mdogo wake Ali, Wagunya kutoka Mombasa; Kenya; Sheikh Saleh Maondoa kutoka visiwa vya Comoro; Sheikh Hassan bin Hassan Mchendange, Mmakonde kutoka Mikindani; Sheikh Ahmed Mohamed Ghazal, Mwarabu kutoka Mombasa; Sheikh Abdallah wa Mwalimu; Mohamed bin Abdallah na Sheikh Fumai bin Silim, Mmakonde wa Mikindani. Kutokana na hawa usufi uliota mizizi na tariqa za Kadiria na Shadhly zilidumu katika sehemu zote za Waislam huko kusini. Kadiri miaka ilivyopita wenyeji wa sehemu zile za kusini, Wamakonde, nao wakaipata elimu hii ya Kiislam kutoka kwa wageni na mabadiliko haya yalikuja kukutana na kuibuka kwa harakati za kudai uhuru mara baada ya Vita Kuu ya Pili.

Wanachuoni wa Kiislamu mjini Mikindani hawakuwa wakipendeza machoni mwa Waingereza kama vile walivyokuwa hawapendezi kwa Wajerumani. Mbali na chuki dhidi ya utawala wa kikoloni kufuatia Vita Vya Maji Maji, Waislam walikuwa na chuki zao binafsi dhidi ya Waingereza kutokana na amri waliyotoa ya kumfukuza mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu, Sheikh Abdallah wa Mwalimu. Sheikh Abdallah aligombana na Waingereza juu ya jambo la akida na uadilifu. Sheikh Abdallah alikuwa liwali akihukumu kwa mujibu wa sharia za Kiislam pale Mikindani. Katika wadhifa huu, afisa wa kikoloni aliamuamuru kutekeleza wajibu ambao Sheikh Abdallah aliuchukulia kuwa ulimvunjia hadhi yake, heshima na itibari kwa Uislamu. Sheikh Abdallah, kutokana na ugomvi huu, alihamishiwa Kondoa Irangi, sehemu yenye Waislam watupu katika Tanganyika, jimbo la kati. Sheikh Abdallah aliishi Kondo Irangi katika miaka yake ya mwisho na kufariki huko. Waislam mjini Mikindani hawakuweza kuwasamehe Waingereza wala kusahau ule udhalimu dhidi ya Sheikh Abdallah. Mwanae, Sheikh Mohamed bin Abdallah wa Mwalimu aliitwa kutoka Lindi kuja kuongoza Tariqa ya Kadiria mjini Mikindani baada ya kifo cha baba yake. Mohamed bin Abdallah, alisoma elimu ya Kiislamu mjini Kondoa. Mjini Lindi alianzisha zawiyya, akahuisha Tariqa ya Kadiria na akawa na madras yake mwenyewe. Alipofariki Sheikh Suleiman bin Said na mdogo wake, Mikindani, nyumbani kwa Sheikh Abdallah wa Mwalimu kukawa hakuma khalifa wa kuongoza tariqa. Hatua ya Sheikh Mohamed kuja Mikindani ilisadifiana na kuibuka kwa TANU. Sheikh Mohamed akiwa khalifa wa Kadiria na murid wake ndiyo walikuwa watu wa kwanza kujiunga na TANU pale Mikindani.

Tukio dogo la kiburi cha askari mpumbavu wa mkoloni ndiko kulisababisha watu wa Mikindani wafungue tawi la TANU. Askari mmoja mpita njia aliingia katika ubishi na kijana mmoja wa pale mjini, akiitwa Hassan Masudi Vuni. Akitumia mamlaka yake ya kukamata mhalifu, askari huyo alimpiga Vuni kwa kumuonea. Miongoni mwa watazamaji wa tukio hilo alikuwa Rashid Ali. Rashid Ali alikwenda kusimulia tukio hili kwa Mohamed Ali Abdallah. Alipokuwa akisimulia mkasa ule, pamoja naye alikuwa Suleiman Hassan Msepele. Walipokuwa wakijadiliana Msepele alitamka kwamba tukio kama hilo kamwe lisingeweza kutokea Dar es Salaam kwa sababu Mwafrika mmoja kwa jina lake Julius Nyerere alikuwa ameanzisha chama cha siasa kupigania uhuru. Rashid Ali na Mohamed Ali Abdallah walitamani kujua mengi zaidi kuhusu Mwafrika huyu aliyekuwa akijulikana kwa jina la Nyerere na chama chake cha siasa, lakini Msepele hakuwa na mengi ya kueleza kuhusu Nyerere na chama chake. Kwa hiyo basi, hawa watu watatu waliamua kumtuma mtu Dar es Salaam kupata habari zaidi kuhusu chama hicho. Mohamed Ali aliandika barua na kumpa Msham Awadh na Ali Muhidin kumpelekea Nyerere. Ndani ya barua hiyo Mohamed Ali alimweleza Nyerere kwamba ukoloni ulikuwa bughudha kubwa katika Jimbo la Kusini, na wangependa kufungua tawi la TANU mjini Mikindani ili kupigania uhuru.

Mwaka 1955 Mohamed Ali alikuwa na umri wa miaka 45. Alikuwa hana elimu kama elimu inavyojulikana kwa kuwa hakusoma shule yoyote. Alipokuwa kijana mdogo baba yake alimpeleka Zanzibar kusoma elimu ya dini. Wakati huo Zanzibar ilikuwa ndiyo kitovu cha elimu ya Kiislamu. Huko Zanzibar kijana Mohamed Ali alisoma kwa Sheikh Mohamed L’ Khamus. Kisha aliendelea na masomo yake mjini Dar es Salaam kwa Sheikh Wazir bin Said, mwanafunzi wa Sheikh maarufu sana na aliyekuwa khalifa wa Tariqa ya Askariyya, Sheikh Idrissa bin Saad. Baada ya kumaliza masomo yake mjini Dar es Salaam alisafiri hadi Belgian Congo na halafu alirudi Ujiji nchini Tanganyika kufanya biashara ndogo ndogo. Katika mwaka 1947 alirudi Lindi na kutoka hapo alikwenda Mikindani na kuwa fundi cherahani.

Msham Awadh alikuwa akijulikana Lindi nzima na Mikindani kwa sababu ya biashara yake. Mshama Awadh alikuwa alikuwa muuza uzuri, yaani vitu vya urembo kama vile uturi, dalia, marashi, rangi na manukato mengine kwa wanawake wa hii miji miwili. Alikuwa akiuza bidhaa zake kikapuni akipita nyumba hadi nyumba. Hawa walikuwa ndiyo aina ya watu walioanzisha na kuongoza harakati za kumaliza utawala wa kikoloni. Hawakuwa wajuzi wa lugha ya Kiingereza wala hawakuwa na ujuzi wa maisha ya ulimwengu wa kimagharibi kama walivyokuwa baadhi ya Waafrika wengine waliyopata elimu ya kimagharibi. Msham Awadh na Ali Muhidin walikwenda hadi Dar es Salaam kukutana na Nyerere, Rupia, Chamwenye, Kambona na Dossa katika makao makuu ya TANU, New Street. Msham Awadh na Ali Muhidin walipewa kadi za TANU na wakaambiwa wafungue tawi Mikindani. Wakati Msham Awadh na Ali Muhidin wakiwa njiani kwenda Dar es Salaam kukutana na Nyerere, Mohamed Ali alisafiri kwenda Lindi kukutana na Mnonji na kumweleza kuwa Mikindani walikuwa wamekusudia kufungua tawi la TANU. Mnonji alimpa kadi Mohamed Ali na akawa mwanachama na akamwambia arudi Mikindani na kuanza kufanya kampeni kwa nguvu kwa ajili ya TANU na awafahamishe watu kuwa Nyerere yupo njiani kuja Jimbo la Kusini.

Julius Nyerere, Ali Mwinyi Tambwe na Rajabu Diwani waliwasili Mikindani kutoka Lindi siku ya Jumamosi. Kabla ya kuwasili ujumbe huo, kazi kubwa kuliko zote waliyokuwanayo uongozi wa TANU Mikindani ilikuwa kutafuta mahali pa kumlaza Nyerere. Walimwendea Ahmed Adam, Mnubi mmoja tajiri na mtu wa makamo, aliyemiliki nyumba moja ya fahari. Nyumba hii ilikuwa ya ghorofa moja na ilijengwa kwa mawe na chokaa. Ahmed Adam aliombwa awe mwenyeji wa Nyerere na ujumbe wake. Nyumba hii tayari lilikuwa na kisa chake. Ilijengwa na hayati kaka yake Ahmed Adam baada ya Vita Kuu ya Kwanza. Kaka yake alikuwa askari wa Kinubi aliyekuwa katika jeshi la Wajerumani. Huenda alichukuliwa Misri mwishoni mwa mwa karne ya kumi na tisa na Wajerumani kuja Tanganyika kama mamluki katika jeshi la Wajerumani wakati wa vita vya Maji Maji. Baada ya vita alilipwa kiinua mgongo na serikali ya Ujerumani na kwa kutumia fedha hizo alijenga nyumba hiyo. Katika Vita Kuu ya Kwanza yeye alipigana katika jeshi la Wajerumani dhidi ya Waingereza. Baada ya vita Wajerumani wakiwa wameshindwa vita, Waingereza waliitikadi nyumba hiyo kama mali ya adui wa himaya ya Kiingereza na kwa hiyo ilibidi itaifishwe. Hii ilikuwa ndiyo nyumba pekee iliyokuwa nzuri yenye kumilikiwa na Mwafrika na kwa ajili hii haikuweza kukosa kuhusudika.

Utawala wa Waingereza ulikuwa katika taratibu ya kuitaifisha nyumba hiyo wakati ilipofahamika kwamba serikali isingeweza kufanya hivyo kwa sababu ya kifungu cha sheria ambacho kilisema kuwa mali ya Waafrika waliokuwa wakitumika katika majeshi ya watawala wao haiwezi kutaifishwa.  Hii ilinusuru nyumba hiyo na hivyo ilibakia mikononi mwa mwenyewe mpaka alipofariki na nyumba hiyo ikaja kuwa katika miliki ya mdogo wake, Ahmed Adam. Ahmed Adam alikubali kumpokea Nyerere na ugeni wake nyumbani kwake. Nyumba hiyo ilikuja kuwa tawi la kwanza la TANU Mikindani. Siku hiyo hiyo ya Jumamosi, usiku Nyerere aliitisha mkutano na wanachama kama thelathini hivi walihudhuria. Nyerere aliwaeleza kwa ufupi juu ya ile safari yake ya Umoja wa Mataifa na hali ya siasa kwa ujumla mjini Dar es Salaam. Nyerere aliwahakikishia waskilizaji wake kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa sana kuwa Tanganyika itakuwa huru katika uhai wao.

Siku iliyofuatia mkutano wa hadhara ulifanyika mjini Mikindani mahali palipojulikana kama Jangwani, karibu na ufuko wa Bahari ya Hindi. Mkutano huu uliohudhuriwa na watu wengi na uliendelea bila mushkeli wowote ukitoa kitendo kidogo kilichofanywa na mwalimu mmoja wa shule, Abdulrahman Muhibu aliyekuwa amelewa. Muhibu alikuwa ametoka kunywa pombe na alipita karibu na uwanja wa mkutano ambapo Nyerere alikuwa akihutubia. Katika hali yake ya ulevi alimpigia kelele Nyerere akamwita muongo. Huenda Muhibu alikuwa akifahamu vyema ujumbe wa Nyerere, na akiwa vile alivyokuwa, mtumishi wa serikali na mlevi, aliona wazo la mwalimu wa shule Mwafrika kama yeye kuwaongoza watu hadi uhuru upatikane ni jambo lisilowezekana. Kwa haraka Muhibu alikamatwa na watu na ilikuwa karibu wamtie adabu ndipo Nyerere alipoingilia na hivyo kumnusuru.

Jioni hiyo baada ya mkutano Nyerere na ujumbe wake waliondoka kwenda Newala, kwenye ngome ya Yustino Mponda. Mponda alikuwa mmoja wa wale wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria waliosafirishwa na Gavana hadi Umoja wa Mataifa, New York, kumpinga Nyerere. Sasa TANU ilikuwa ikichukua mkokoto wake wa kampeni hadi ndani ya ardhi ya Mponda ambayo yeye alikuwa liwali na mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria. Nyerere alipomaliza ziara yake ya Jimbo la Kusini, fikra za Wakristo zilibadilika. Wakristo hawakuamini tena kuwa TANU ilikuwa harakati za Waislam sawasawa na Vita Vya Maji Maji. Nyerere, Tambwe na Diwani walipokuwa wanashika njia kurudi Dar es Salaam, matawi ya TANU yalikuwa yamefunguliwa Masasi, Ndanda na Newala ambazo zilikuwa sehemu za Ukristo na ngome ya Ukatoliki katika Tanganyika.

Nyerere aliporudi Lindi mwaka 1959, TANU ilikuwa ina nguvu sana na ilikuwa imekumba kila mtu. Wale watumishi wa serikali wengi wao wakiwa Wakristo, walio kuwa wakiibeza TANU mwaka 1955 kwa sababu ilikuwa ikiongozwa na Waislam ëwasiokuwa na elimu,í ukweli ulikuwa umewadhihirikia na sasa walikuwa wakionyesha heshima kwa chama. Hawakuwa na khiyari na ilibidi waonyeshe heshima kwa sababu bwana mwenyewe, yaani serikali ya kikoloni, ilikuwa na heshima kwa TANU. Serikali ilikuwa imetambua kuwa dhamiri ya watu ya kukataa kutawaliwa haiwezi tena kupuuzwa. Nyerere alikuwa amelihutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa mara mbili, mara ya pili ikiwa mwaka 1957. Ujumbe wa TANU ulikuwa wazi, watu wa Tanganyika walikuwa tayari kujitawala. Kila siku zilivyopita ndivyo TANU ilivyopata nguvu. Rashidi Salum Mpunga, dereva wa lori, aliweza kumshawishi na akafanikiwa kumuingiza TANU mmoja wa masheikh wenye kuheshimiwa sana mjini Lindi na mshairi maarufu, Sheikh Mohamed bin Yusuf Badi. Sheikh Badi alipoingia TANU kwa ajili ya heshima yake na kukubalika na watu, idadi kubwa ya Waislam walimfuata na kukata kadi za TANU. Nyerere alipokuja Lindi kujadili tatizo la kura tatu na uongozi wa Jimbo la Kusini, Sheikh Yusufu Badi alimpokea Nyerere na madras yake, wanafunzi wakimwimbia Nyerere kasda na kumpigia dufu. Kuanzia hapo sasa kila mtu alijiunga na TANU. Si Mponda wala Kanisa lilikuwa na uwezo wa kupambana na TANU kwa wakati ule. Polepole lakini na kwa kwa uhakika, TANU ilingia ndani ya maeneo ya Kikristo huko Songea, Masasi, Tunduru na Newala, nyumbani kwa Yustino Mponda.

Lakini matukio mawili ya kumbukumbu kubwa yalikuwa katika safari ya pili ya Nyerere alipozuru tena Jimbo la Kusini. Kumbukumbu ya kwanza ilikuwa tawaswil aliyosomewa Nyerere na Sheikh Yusuf Badi mwenyewe pamoja na Waislam aliowachagua yeye sheikh mwenyewe maalum kwa hafla hiyo, pamoja na waliochaguliwa na masheikh wengine.Kumbukumbu ya pili ni ile karamu  iliyoandaliwa kwa heshima ya Nyerere na Mussa Athumani Lukundu, kiongozi wa Dockworkers’ Union. Hii ilikuwa heshima kubwa aliyoonyeshwa Nyerere, ilikuwa kilele cha upendo na heshima kwa Muislamu yoyote anaweza kumfanyia asiyekuwa Muislamu.

Siku ya ukumbusho mkubwa sana mjini Lindi ilikuwa siku ya uhuru, tarehe 9 Desemba, 1961. Sheikh Badi, bingwa wa mashairi, aliombwa na TANU kuandika hotuba ya uhuru itakayotolewa na Yusuf Chembera mbele ya DC akiwa kama mwakilishi wa utawala wa Kiingereza uliokuwa uking’oka. Hotuba hiyo ya Sheikh Badi na iliandikwa kwa Kiarabu na Chembera. Akiwa mtoto mdogo Chembera alipelekwa kwa Sheikh Yusuf Badi na baba yake kwenda kusoma elimu ya dini na aliendelea kuwapo hapo chuoni kwa Sheikh Badi hadi alipohitimu. Sheikh Badi hakuona kama ipo hotuba yoyote iliyoandikwa na mwanadamu iliyostahiki hafla kama ile ya siku ya kujikomboa kutoka minyororo ya ukoloni. Sheikh Badi alimsomea mwanafunzi wake Chembera, dua ya kunut ambayo husomwa na Waislam katika kila sala ya alfajir. Usiku wa manane wa tarehe 9 Desemba, 1961 ulikuwa usiku adhim sana kwa wote wawili, mwalimu na mwanafunzi wake, pale watu walipokusanyika katika ule uwanja wa gofu na kumsikiliza Chembera akisoma kunut kupokea uhuru wa Tanganyika. Lakini mara tu baada ya uhuru Wakristo walianza kuuchimba ule waliouona kuwa uongozi wa Waislam katika TANU kwa kisingizio kuwa uongozi ule haukuwa na elimu. Suleiman Masudi Mnonji alikamatwa na kutiwa kizuizini kwa amri ya Nyerere chini ya Preventive Detention Act ya mwaka 1962 kwa kile kilichoitwa ‘’kuchanganya dini na siasa,’’ na Waislam wengine waanzilishi wa harakati za kudai uhuru walitupwa nje ya uongozi.


Post a Comment