Friday, 11 May 2018

DK. MAHATHIR, ''ROLE MODEL'' WA ZITTO KABWE, MWENYE MAAJABU NA YUSUFU LULUNGU

Dk. Mahathir ‘Role Model’ wa Zitto Kabwe, Mwenye Maajabu

Na Yusufu Lulungu

Zitto Kabwe na Mahathir Mohamed

Kuala Lumpur


Mara kadhaa Mbunge wa Kigoma mjini(ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amekuwa akiandika mambo kumuhusu Mzee huyu Dk. Mahathir Mohamad.

Miongoni mwa maandiko yake kwa Mzee huyu ni lile la mwaka 2013 katika gazeti la Raia Mwema lililokuwa na anuani ya “Uhuru wa fikra utawango’a madikteta,” na lile la hivi karibuni la kumtakia heri ya kuzaliwa na kutimiza miaka 92.

Pia baadhi ya watu wakaribu na Zitto Kabwe wamewahi kunijuza kuwa mbunge huyo anamchukuliwa Dk Mahathir kama mmoja wa ‘kioo’ chake muhimu kuelekea harakati zake za kisiasa huko mbeleni na ujenzi wa nchi.

Sababu moja wapo ya Zitto kumchukulia Dk. Mahathir kama mfano wake wa kuigwa ni uwepo wa mshabaha kiasi katika historia zao za kisiasa. Nitaeleza hili huko mbeleni kwenye makala haya.

Kwenye anuani ya makala haya nimedokeza kuhusu maajabu anayoendelea kuyafanya Dk. Mahathiri ambae alikuwa Waziri Mkuu wa nne wa Malaysia  kuanzia mwaka 1981 hadi mwaka 2003 alipojiuzulu.

Moja ya maajabu hayo yanatokana na matokeo ya Uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Malaysia  Jumatano iliyopita ambapo Muungano wa vyama vya Upinzani(Pakatan Harapan au Alliance of Hope) ukiongozwa na Dk. Mahathir ulishinda uchaguzi huo.

Upinzani huo ulinyakuwa viti vya wabunge 113 na kuubwaga Muungano uliyokuwa madarakani, Barisan Nasional (BN), ukiongozwa na waziri mkuu aliyenyofolewa kitini ndugu Najib Razak. BN waliambulia  viti 79.

Matokeo hayo yanatoa maajabu haya, Mosi, ni kuwa Dk. Mahathir aliyeshika nafasi ya uwaziri mkuu kwa miaka 22 na kustaafu siasa kwa muda wa miaka 15 amerejea tena kwenye nafasi hiyo wakati huu akitokea chama cha Upinzani.

Na kwa sasa Dk. Mahathir mwenye umri wa miaka 92 ndio anakuwa kiongozi mwenye umri mkuwa duniani kuchaguliwa kuwa kiongozi wa kisiasa.

Dk. Mahathir ndiye anatajwa kuwa ‘Baba wa taifa’ wa Malaysia kwa kulifanya taifa hilo kuwa na nguvu kubwa za kiuchumi na kisiasa na hata kuingia kwenye ‘Asian Tigers’.

Pili, Dk. Mahathir amechangia kuung’oa madarakani Muungano huo wa BN ambamo ndani yake kuna chama chake cha UMNO alichokulia kwa zaidi ya miaka 50. Mahathir alikihama chama hicho hapo mwaka 2016 na kujiunga na Muungano wa vyama vya upinzani.

Miongoni mwa sababu za Dk. Mahathir kukihama chama hicho ni shutuma za ufisadi zinazomkabili Razak, ambapo anadaiwa kupokea kiasi cha dola milioni 700 kutoka taasisi moja ya maendeleo nchini humo.

Pia Dk. Mahathir anamtuhumu Razak kwa kuongoza nchi kinyume na katiba ikiwemo kuharibu uchumi wa nchi.

Tatu, Dk. Mahathir amemngo’a mtu ambae alimkuza kisiasa kwa lugha nyingine mwanafunzi wake. Ni Dk. Mahathir ndiye aliyemuwezesha Najib Razak kushika nafasi mbalimbali ndani ya chama na kisha nafasi ya naibu Waziri mkuu na hapo mwaka 2009 kuwa Waziri Mkuu wa sita.

Akiandika kwenye kitabu cha wasifu wake ‘A Doctor in the House,’ cha mwaka 2011 ukurasa wa 768 Dk. Mahathir anasema: “Katika moja ya hotuba zangu za kushtukiza kabla sijastaafu, nilisema bayana kuwa natarajia Tun Abdullah(naibu waziri mkuu wakati huo) angemchagua Najib kuwa naibu wake.”

Tun Abdullah ndio alikuwa anachukuwa nafasi ya Uwazir mkuu baada ya kustaafu Dk.Mahathir mwaka 2003.

Ajabu la nne ni kuwa Dk. Mahathir ameshinda uchaguzi huo kupitia Muungano huo wa vyama vya Upinzani ulioundwa  na hasimu wake mkubwa kisiasa Anwar Ibrahim.

Wawili hao walikiingia kwenye ugomvi hapo mwaka 1998 baada ya Dk. Mahathir kumtimua Anwar kwenye nafasi ya unaibu Waziri mkuu na baadae kutimuliwa kwenye chama kwa madai ya ulawiti.

Anwar ambae alitajwa kuwa muumini mzuri wa dini, alishutumiwa kuwa na tabia ya kulawiti wasaidizi wake na wengineo. Madai hayo yalitajwa(yanatajwa) kuwa ni ya kisiasa na kudaiwa kuratibiwa na Dk.Mahathir ili kumzuia Anwar asiwe Waziri Mkuu.

Madai hayo baadae yalimpelekea Anwar kufungwa jela na mpaka sasa yupo gerezani. Licha ya kuwemo gerezani, Anwar ndio anatajwa kuwa kinara wa  Muungano huo wa upinzani (Pakatan Alliance).

Ajabu la tano, ni kuwa mke wa Anwar, Wan Azizah binti Wan Ismail aligombea kwenye muungano huo pamoja na Dk. Mahathir, akiwania nafasi ya unaibu Waziri Mkuu.

Tangu kutimuliwa kwa Anwar, Azizah, familia nzima na wapinzani wamekuwa wakimuangalia kwa jicho baya Dk. Mahathir. Wanamuona ndio mtu aliyeharibu maisha ya Anwar.

Leo hii mke wa Anwar na Dk. Mahathir wanafanya kazi pamoja, Dk. Mahathir akiwa Waziri Mkuu, Wan Azizah akiwa naibu wake.

Katika moja ya mahojiano yake na runinga ya Aljazeera, Dk. Mahathir ameonekana kumuonea huruma Anwar akihisi ni kweli anateseka kutokana na hatua yake ya kumfukuza Serikalini.

Lakini kwenye kitabu chake cha ‘A Doctor in The House’ ukurasa wa 698 Dk Mahathir anaonekana kutojutia hilo akisema: “Leo hii Anwar angekuwa waziri Mkuu wa Malaysia”. Lakini kwa kuwa hajawa, ni kwa sababu ya matendo yake mwenyewe. Sikuwa na chaguo lolote bali kumuondoa Serikalini na nilifanya nilichokiona ni sahihi kwa ajili ya nchi. Huenda nimefanya makosa mengi lakini la kumfukuza Anwar sio miongoni mwa makosa hayo.”

Hata hivyo Mahathir ameahidi kuwa atatawala kwa muda wa miaka 2 kisha kumpisha Anwar awe Waziri Mkuu.

Kwanini ni ‘Role Model’ wa Zitto?

Moja ya eneo ambalo linatajwa kumfanya Zitto Kabwe amuone Dk. Mahathir kama ni mtu wanaofanana kisiasa ni wote wawili kufukuzwa uanachama ndani ya vyama vyao kwa tuhuma za usaliti.

Kama ilivyokuwa kwa Zitto Kabwe ambae hapo mwaka 2013 alifukuzwa uanachama ndani ya Chama chake cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kwa tuhuma za usaliti, yakiwemo madai ya kutaka kumpindua Mwenyekiti Freeman Mbowe ndivyo ilivyokuwa kwa Dk. Mahathir.

Hapo mwaka 1969, Dk. Mahathir alifukuzwa uanachama kwa tuhuma za uchochezi na kutaka kumpindua aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo Tunku Abdul Rahman.

Chanzo cha yote ni hatua ya Dk. Mahathir kuandika barua kali iliyomtuhumu Tunku kuwa alikuwa ameshindwa kukiongoza chama(UMNO) mara baada ya chama hicho kushindwa kiasi kwenye uchaguzi mwa mwaka huo 1969.

Pia Dk. Mahathir alimtuhumu Tunku kuwa ameshindwa kuongoza Serikali, hapendwi na wananchi wake, na ameshindwa kulilinda kabila la Malay dhidi ya jamii ya Wachina ambao walijiona kuwa ndio Malaysia halisi na kuanza kuwatenga wenzao ikiwemo kuwafanyia vurugu.

Barua hiyo iliyosambazwa nchi nzima, ilimfanya Dk. Mahathir aonekane msaliti na mchochezi na kufanywa aitwe mbele ya Baraza kuu ili ajieleze na kufuta yaliomo kwenye barua hiyo. Hata hivyo Mahathir aligoma kuondoa maneno hayo, akishikilia msimamo wake kuwa alichokisema ni ukweli.

Dk. Mahathir anaetajwa kuwa ‘mbishi’ na ‘mbabe’ aliandika barua hiyo katika wakati ambao wakosoaji wa Serikali walikuwa wakikamatwa na kusekwa jela.

Hata hivyo kufukuzwa kwenye vyama vyao,  haukuwa mwisho wao kisiasa, Dk. Mahathir alirejea kwenye chama mwaka 1974 kwa msaada wa watu kadhaa akiwemo Harun Idris aliyekuwa makamu wa Rais wa UMNO.

Jambo la ajabu tena, hapo baadae Dk. Mahathir akagombea nafasi hiyo ya Harun, mtu aliyemsaidia kurudi chamani, na kummbwaga ‘muokozi’ wake huyo.

Nae Zitto licha ya kwamba hakuwa nje kabisa ya kisiasa, baada ya kutimuliwa, alihamia chama kingine  cha ACT Wazalendo na kugombea ubunge mwaka 2015 ambapo nae alimmbwaga mwalimu wake, marehemu Dk. Aman Walid Kaborou.

Moja ya tofauti zao ni kuwa Dk. Mahathir ameweza kufikia nafasi ya uwaziri mkuu, nafasi ya juu nchini Malaysia huku Zitto Kabwe akiwa bado kwenye Ubunge.

Kwa kuwa Zitto Kabwe anamtazama Dk. Mahathir kama kioo chake kisiasa huenda nae anatamani siku moja awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufikia rikodi ya ‘mwalimu’ wake huyo.

Mwandishi wa makala haya ni mwandishi wa habari, simu 0625592471.

Post a Comment