Thursday, 10 May 2018

UMUHIMU WA MAHKAMA YA KADHI KWA WAISLAM WA TANZANIA BARA - SHEIKH MOHAMED IDDI MOHAMEDUSHAURI WA WAZI KWA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, PROFESA PALAMAGAMBA KABUDI:

“SULUHISHO LA MGONGANO KATIKA SHERIA YA NDOA YA MWAKA 1971 NI UREJESHWAJI WA MAHKAMA YA KADHI TANZANIA BARA”

Sheikh Mohamed Iddi Mohamed
(Abuu Iddi)

Ndugu zangu Wanahabari,

Assalaam Alaykum,
(Amani ya Mwenye ezi Mungu iwe kwenu)

Maudhui ya tamko langu hili ni hitajio la Waislam wa Tanzania Bara kuwa na Mahkama ya Kadhi.

Ndugu Wanahabari,
Hivi karibuni kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumemsikia Mheshimiwa Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, akitoa nasaha alisema (nanukuu):

“…Mashauri ya ndoa, mashauri ya mirathi, mashauri yanayogusa mila na desturi, mashauri yanayogusa dini, ni vyema tukayaendea kwa uangalifu mkubwa. Na niseme kwa unyenyekevu mkubwa somo hili la ndoa nimelifundisha kwa miaka kumi na tisa, sio eneo jepesi” (mwisho wa kunukuu).

Maneno hayo ya Mheshimiwa Waziri Kabudi yanamaanisha mambo makuu mawili:
                Kwanza, anatuthibitishia kwamba yapo matatizo au kero nyingi katika masuala ya sheria ya ndoa na masuala ya dini.
                Pili, anatunasihi tuwe na umakini mkubwa katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo hayo au kero hizo.

Ndugu Wanahabari,

Kupitia taarifa hiyo ya Mheshimiwa Waziri Kabudi, nimeonelea nimshauri kwamba njia mojawapo ya kuiendea katika kuyatatua matatizo hayo ni urejeshwaji wa Mahkama ya Kadhi.

Ni vizuri nikamkumbusha Mheshimiwa Waziri kwamba maombi ya Waislam wa Tanzania Bara kutaka warejeshewe Mahkama ya Kadhi sio jambo jipya na tayari limeshapitia michakato kadhaa lakini kwa sababu haikuwepo dhamira ya dhati kwa Serikali kuwarejeshea Waislam Mahkama ya Kadhi, mafanikio hayakufikiwa.

Mheshimiwa Waziri anakumbuka mengi juu ya kadhia ya Mahkama ya Kadhi lakini kamwe hawezi kusahau kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliwahi kuunda Tume ya Kibunge chini ya uenyekiti wa Mheshmiwa Athumani Janguo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kisarawe Mkoa wa Pwani.

Tume hiyo ilihoji na kujiridhisha juu ya hitajio la Waislam kurejeshewa Mahkama ya Kadhi lakini ripoti hiyo haikusomwa Bungeni kama tulivyozoea kuona ripoti za Kamati na Tume mbalimbali za Kibunge.

Ndugu Wanahabari,

Mheshimiwa Waziri atakumbuka pia;
Juhudi zilizosimamiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Mizengo Peter Pinda, ambazo zilikwamishwa pia kwa hofu ya ‘turufu ya urais’.

Juhudi za mchakato wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ili sheria hiyo izitambue hukumu zitakazotolewa na Makadhi hawa wasiokuwa na meno (wasiotambuliwa na sheria za nchi) pia zilikwamishwa tena kwa hatua ya kusikitisha.

Ukweli ni kwamba hakuna ‘njia ya mkato’ katika kutatua migogoro inayotokana na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 zaidi ya kufanya mojawapo kati mambo matatu yafuatayo:

(1)         Kurejeshwa Mahkama ya Kadhi yenye ‘meno yake’ kamili;

(2)    Kuifanyia marekebisho Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ili kiwepo kipengele kitakachotambua hukumu zinazotolewa na Makadhi hawa waliopo sasa;

(3)       Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 itambue Ndoa ya Kiislamu kwa ujumla wake na ukamilifu wake (kwa maana itambue kufungishwa kwake, maisha yake, talaka yake, rejea yake, eda yake na kadhalika).

Ndugu Wanahabari,

Nina hakika kwamba Mheshimiwa Waziri Kabudi ambaye amekiri kusomesha somo la Ndoa kwa takriban miaka kumi na tisa, anafahamu wazi migongano iliyopo kati ya matakwa ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na usahihi wa Sheria ya Ndoa ya Kiislam.

Nitoe mifano michache ya migongano hiyo, kwa mfano:

             Sheria ya Kiislam katika ufungishaji wa Ndoa inahitajia kuwepo Walii (mfungishaji ndoa) ambaye huwa ni Baba, Babu, Kaka na kadhalika (mtu yeyote atakayefungisha ndoa ukimuondoa Walii atakuwa amewakilishwa na Walii). Wakati Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inamtambua Sheikh tena mwenye leseni kuwa ndiye mfungishaji ndoa na wala haimtambui Baba kama mhusika mkuu wa ndoa.

             Sheria ya Ndoa ya Kiislam hailazimishi kuwa ndoa ili iwe ni halali ifanywe maeneo yaliyo wazi bali kuitangaza ndoa ni sunnah (jambo jema lenye malipo kwa Mungu). Lakini Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inalazimisha hilo suala la uwazi katika kufunga ndoa.

             Sheria ya Ndoa ya Kiislam inampa Walii (Baba na kadhalika) nguvu ya kukataa Binti yake kuolewa na mwanamume wa dini nyengine kwa kuwa ndoa hiyo haiswihi (haikubaliki) na waliooana kwa ndoa hiyo wanahesabiwa kuwa ni wazinifu kama wazinifu wengine katika jamii. Lakini kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inaiona na kuitambua ndoa hiyo kuwa sahihi haswa baada ya kutolewa tangazo la kusudio la ndoa na kukosekana pingamizi lolote kuzuia kusudio hilo.

Ndugu Wanahabari,

Huo ni mgongano kati ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na matakwa ya Sheria ya Ndoa ya Kiislam kwa upande wa kufunga ndoa (kuoana).

Ama kwa upande wa Talaka na kuvunjika kwa ndoa:

             Talaka anayoitoa Muislam inatosha kuvunja ndoa kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya Kiislam. wakati talaka kwa upande wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 haipati uzito wa kisheria mpaka kipatikane cheti cha Mahakama kinachothibitisha kuvunjika kwa ndoa hiyo. Kwa muktadha huo, Muislam hana uwezo wa kutoa talaka na talaka yake ikatambulika kisheria kwani talaka anayoitoa Muislam inahesabika kuwa ni kusudio la kuivunja ndoa.

             Aidha, hiyo Talaka ya Muislam ambayo Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 haiitambui mpaka ithibitishwe na Mahakama, katika Uislam imegawanyika katika makundi kadhaa ambayo hiyo Mahakama ya nchi na Mahakimu wake hawawezi kuzitambua wala kujua kinachozaliwa baada ya talaka hizo.

Naomba nitoe mifano michache katika eneo hilo la Talaka ya Kiislam:

(a)          Kuna talaka iliyo wazi ambayo inaitwa “TWALAQ SWARIIH”.

(b)          Kuna talaka ya fumbo ambayo inaitwa “TWALAQ KINAAYAH”.

(c)           Kuna talaka iliyotundikwa ambayo inaitwa “TWALAQ MU’ALLAQ”.

(d)          Kuna talaka inayopita haikutundikwa inaitwa “TWALAQ MUNAJJAZ”.

(e)          Kuna talaka ya kurejeleka ambayo inaitwa “TWALAQ RAJI’IYYAH” (katika talaka ya kurejeleka, kama mke ameachwa talaka ya rejea pindi mume akifariki kabla eda haijakwisha mke huyo atamrithi mtalaka wake).

(f)           Kuna talaka isiyo ya kurejeleka ambayo inaitwa “TWALAQ BAIN”. Na hiyo BAIN kuna SUGHRAA (ndogo) na KUBRAA (kubwa).

(g)          Kuna talaka kabla ya kukutana kimwili.

(h)          Kuna talaka ya kujivua ambayo inaitwa “KHUL-I”.

(i)            Kuna ndoa inayovunjika yenyewe bila ya kutamkwa talaka pale mmoja kati ya wanandoa anapobadilisha dini.

Kwa uchambuzi huo, Mheshimiwa Waziri Kabudi ataungana nami kwamba Ndoa na Talaka katika Uislam ni jambo kubwa sana na pana linalohitajia Mahakimu maalum wenye utaalamu usiotiliwa shaka.

Ndugu Wanahabari,

Naomba nitumie fursa hii kumuomba Mheshimiwa Waziri Kabudi kwa kuzingatia kwamba katika wakati huu ambayo yeye ni Waziri wa Sheria na Katiba, Mwalimu wa Sheria na Mtaalam katika Somo la Ndoa alilolifundisha kwa takriban miaka kumi na tisa; naamini ndio wakati muwafaka wa kuitafutia ufumbuzi migongano na migogoro inayotokana na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971.

Wakati mwengine wowote kamwe hauwezi kuwa ni muwafaka kwani Mahkama ya Kadhi kwa muda wote imekuwa ni kadhia iliyotumiwa kama ‘chambo’ cha kuvuna kura za Waislam katika chaguzi zilizopita na kamwe hitajio lake halichukuliwi kuwa ni kutatua kero na migogoro inayowasibu sehemu ya jamii ya Watanzania.

Ndugu Wanahabari,

Nimalizie mazungumzo yangu kwa kusema mambo matano:

Jambo la kwanza, nimuombe Mheshimiwa Waziri Kabudi aniruhusu kumuona anapokuwa Jijini Dar es Salaam ili tubadilishane mawazo katika kuiendea kadhia hii. Katika hili nimuombe pia Mheshimiwa Waziri aombe kupatiwa Hansad za Bunge na taarifa mbalimbali juu ya kadhia hii ya Mahkama ya Kadhi ili tutakapokutana zitusaidie katika mazungumzo yetu.

Jambo la pili, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Kabudi na Watanzania kwa ujumla kwamba ukimya, upole na ustahamilivu wa Waislam wa Tanzania Bara katika kunyimwa haki yao hii ya Mahkama ya Kadhi ambayo wakipewa haina madhara yoyote kwa jamii nyengine ya Watanzania sio endelevu bali ni wa msimu tu.

Jambo la tatu, namuomba Mheshimiwa Waziri Kabudi akumbuke pia kwamba uwepo wa Makadhi hawa wa sasa ambao hawana ‘meno’ wala kinga ya kisheria pale watakaposhtakiwa katika Mahakama ya Tanzania kwa kosa la kuvunja ndoa ya mtu ambaye hakuridhishwa na maamuzi yao, kamwe hauwezi kuwa ndio ‘dozi’ ya nusu kaputi ya kuwasahaulisha Waislam wa Tanzania Bara madai ya hitajio lao hili yaliyodumu kwa takriban miaka thelathini sasa.

Jambo la nne, kupitia mkutano wangu nanyi ndugu wanahabari nichukue nafasi hii kumkumbusha na kumuomba Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Job Ndugai.
Nimkumbushe azikumbuke ‘mbinu chafu’ zilizotumiwa na baadhi ya Wabunge katika ‘kukwamisha’ rasimu ya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 isiingie na kujadiliwa ndani ya Bunge katika Bunge lililopita ambalo yeye Mheshimiwa Ndugai alikuwa ni Naibu Spika.

Rasimu hiyo ililenga mjadala wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ili itambue hukumu za ndoa za Waislamu kupitia Makadhi hawa waliopo ambao kwa mujibu wa sheria za nchi ‘hawana meno’. Nimkumbushe Mheshimiwa Spika Ndugai tena na tena kwamba waathirika wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 hawajasahau na wala hawatasahau mbinu ile iliyotumika kuwanyima haki zao.

Nimuombe Mheshimiwa Spika Ndugai kwamba kwa kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Taasisi na Mhimili unaojitegemea, atoe agizo kwa watendaji wa Bunge wazirejee na waziandae kumbukumbu zote za Bunge ikiwemo mchakato wa Kamati za Bunge kuhusu kadhia ya Mahkama ya Kadhi Tanzania Bara kupitia Bunge ili hoja hii itakapoibuka tena katika awamu hii ya tano isionekane ni hoja mpya bali ni muendelezo wa maombi ya Waislamu wa Tanzania yaliyodumu takriban miaka thelathini.

Jambo la tano, kupitia mkutano huu pia nimuombe Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli, amtake Waziri wake wa Sheria na Katiba, Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi, amuandalie taarifa ya madai ya Mahkama ya Kadhi Tanzania Bara tangu mwanzo mpaka hapa tulipofikia.

Taarifa hiyo pia ijumuishe hoja za wanaodai na hoja za wanaokataa uwepo wa Mahkama ya Kadhi Tanzania Bara na hitimisho lake ili Mheshimiwa Rais Magufuli kupitia vyombo vyake alifahamu suala hili ukweli wake bila ya wasiwasi na shaka yoyote.

Nimuombe Mheshimiwa Rais Magufuli alichukulie suala hili la Mahkama ya Kadhi kwa uzito wake kwa kuwa ni miongoni mwa kero zinazohitajia ufumbuzi na hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) anachokiongoza kwa nafasi ya uenyekiti Taifa kiliahidi kulitafutia ufumbuzi suala hili kupitia Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Kwa kuhitimisha, nimuombee dua Mheshimiwa Rais Magufuli ili Mola Muumba amuwezeshe kulisimamia hili ili kero hii itatuke katika wakati wake na historia imkumbuke kwa mengi ikiwemo na hili pia.

Ndugu Wanahabari,

Nawaomba ujumbe huu muufikishe kwa jamii ya Watanzania kwa usahihi wake.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Wabillaahi Ttawfiiq,

Sheikh Mohamed Iddi Mohamed (Abuu Iddi)
Mwenyekiti – Arrisaalah Islamic Foundation

Tarehe: 09.05.2018
Dar es Salaam.

Post a Comment