Showing posts with label Taazia. Show all posts
Showing posts with label Taazia. Show all posts

Wednesday, 13 September 2017


TAAZIA: DR. BUYUNI JAHAZIDr. Jahazi amefariki mchana huu leo tarehe 13 September, 2017.
Kwake tumetoka na Kwake ni marejeo yetu.

Iko siku mwaka wa 1993 na ulikuwa mwezi wa Ramadhani nilikuwa nasafIri na ndege ya Air Tanzania Corporation (ATC) kuelekea Harare kwenye kozi ya Masoko ya Huduma yaani, ‘’Marketing of Services.’’ Wakati ule nilikuwa nikifanya kazi Bandarini Idara ya Masoko.

Ndege ilikuwa ya alfajir na kwa bahati nzuri Dr. Jahazi na yeye alikuwa anasafiri na ndege hiyo hiyo kuelekea Harare kwenye mkutano wa Madaktari. Wakati ule Dr. Jahazi alikuwa akisomesha pale Muhimbili Faculty of Medicine.

Basi nikamkuta Dr. Jahazi pale uwanjani amesimama anasubiri ATC wafungue ‘’desk,’’ lao abiria waanze mchakato wa ku -‘’check in,’’ abiria ili wapatiwe, ‘’boarding pass,’’ waelekee, ‘’departure lounge,’’ na kuingia katika ndege tayari kuwa kuruka.

Dr. Jahazi alikuwa amevaa kanzu nyeupe na amepiga kilemba cha tabligh.

Ukitamtazama picha ya haraka itakayokujia ni kuwa huyo ni sheikh wa tabligh siyo Mhadhiri wa Chuo Kikuu.

Siku zile ilikuwa hakuna, ‘’security check,’’ kama hizi za siku hizi za kupitisha watu na mizigo katika, ‘’metal detector,’’ ambazo kwa sasa ziko kila mahali kuanzia viwanja vya ndege hadi katika mahoteli makubwa.

Wakati nasalimiana na Dr. Jahazi tukiubiri ATC wafungue, mara akatokea Balozi Ami Mpungwe wakati ule akifanyakazi Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje kama Balozi na Mkurugenzi wa Afrika na Mashariki ya Kati.

Ami akaja pale tulipokuwa tumesimama na akatusalimu.

Dr. Jahazi akamuuliza kama na yeye ni msafiri. Ami akajibu akasema yeye amekuja kuwasindikiza wageni wa serikali na alikuwa kawaingiza VIP Lounge na alikuwa anaondoka ndipo alipotuona akaona aje atusalimu.

Dr. Jahazi akamfahamisha Ami kuwa sisi tulikuwa tunakwenda Harare.

Dr. Jahazi alikuwa mkononi ameshika, ‘’briefcase,’’ na katika ile, ‘’briefcase,’’ alikuwa amefunga kidumu cha lita tano chenye maji.

Ami akawa kashangazwa na kile kidumu cha maji, akamuuliza Dr. Jahazi, ‘’Dr. haya maji ya nini?’’

Dr. Jahazi akajibu akasema, ‘’Haya maji natembea nayo kwa ajili ya kuchukua udhu isije wakati wa sala umeingia na mimi sina maji ya kutawadha.’’

Jibu lili lilimtosheleza Ami hata na mie pia kwani nami nilikuwa najiuliza yale maji yalikuwa ya nini ila tu sikupata fahamu ya kuuliza.

Ndani ya ndege tulikaa pamoja na ilikuwa safari nzuri sana kwangu.

Dr. Jahazi aliniwaidhi kuhusu utukufu wa Allah na Mtume Wake na akaniambia kuwa endapo nitaishika kamba ya Allah nitafanikiwa hapa duniani na akhera.

Siku ile tukiwa angani tukielekea Zimbabwe ndiyo kwa mara yangu ya kwanza nilipolisikia jina la Prince Badru Kakunguru wa Uganda.

Dr. Jahazi alipobaini kuwa mimi sikuwa namjua Prince Badru Kakunguru alianza kunieleza historia ya Uislam Uganda na vipi Prince Badru Kakunguru alivyofanya juhudi katika kuuepeleka Uislam mbele Uganda.

Nilishangaa sana kwani sikujua kuwa Dr. Jahazi juu ya kuwa Bingwa wa Micro Bio-Chemistry Uganga wenyewe alikuwa pia ni mjuzi wa historia.

Niliona safari ni fupi sana katika ya Dar na Harare.

Mimi nilikuwa sijafika Harare lakini yeye Dr. Jahazi alinifahamisha kuwa alikuwa akienda huko mara nyingi kwa shughuli za mikutano na makangamano ya kitaaluma.

Basi nikamuomba Dr. Jahazi anifahamishe hoteli nzuri ya mimi kwenda kukaa.

Ilikuwa kozi ya takriban mwezi mzima na nilitaka nikae mahali pazuri.

Dr. Jahazi alinitazama usoni akaniambia, ‘’Sikiliza mdogo wangu Mohamed, mimi sikai hoteli, mimi nalala msikitini.’’

Ukweli ni kuwa nilishtuka na kushangaa sana.

Juu ya mshtuko wangu sikusema kitu nilinyamaza kimya.

Wakati tunatoka nje ya uwanja wa ndege wa Harare mie nikawa nimemganda Dr. Jahazi niko ubavuni kwake. Mara tu tulipokuwa tushapita, ‘’Customs,’’ kundi la vijana wa kila rangi nikaona wamemvamia Dr. Jahazi wakimpokea mizigo yake na kutokana na mazungumzo yao nikajua hawa ni madaktari wanataaluma wanzake.

Ghafla Dr. Jahazi akawa kageuka si yule aliyekuwa na mimi ndani ya ndege. Hapa alikuwa Dr. Jahazi ‘’Lecturer,’’ yuko darasani anasomesha.

Mara atamjibu huyu hiki mara atamjibu huyu kile kwa Kiingereza kilichonyooka kisawasawa. Hakika wale jamaa ilionyesha walikuwa wanamuusudu Dr. Jahazi na walikuwa wamengoja kwa hamu.

Yalikuyokuwa yanazunguzwa pale mie sikuambulia hata moja.

Baada ya kutulia tukaingia katika gari kuelekea mjini na akanambia kuwa atanipeleka Ambassador Hotel iko katikati ya mji na akamwambia dereva apite barabara fulani ili anionyeshe msikiti nitakaokuja kuswali tarweh.

Nakumbuka kichekesho kimoja.

Dr. Jahazi aliposema neno, ‘’mosque,’’ yule dereva akawa hajui lina maana gani.

Dr. Jahazi alipomfahamisha dereva kuwa ni ‘’msikiti,’’ yule bwana akajibu akasema, ‘’Oh! You mean Muslim church.’’

Dr. Jahazi alikuwa rafiki kipenzi wa kaka yangu Prof. Mgone toka wote wakiwa wanafunzi pale Muhimbili na nilikuwa nafurahishwa na kitu kimoja kila tunapokutana.

Ingawa sasa mimi ni mtu mzima lakini yeye hakuacha kuniangalia mimi kama, ‘’bwana mdogo,’’ wake na katika mazunguzo yetu siku zote hiki kikijitokeza na mimi nilikuwa siachi kutanguliza, ‘’kaka,’’ kila ninapozungumza na yeye.

Miezi michache iliyopita tulikuwa sote tukaachana Msikiti wa Shadhly baada ya kuzungumza njia nzima.

Mwaka wa 2002 Tanzania ilipopitisha Sheria ya Ugaidi, Dr. Jahazi alivamiwa nyumbani kwake na kutiwa nguvuni kwa kushukiwa kuwa ni gaidi. Wapelelezi walipekuea nyumba yake chini juu juu chini kutafuta ushahidi wa ugaidi lakini walichokutananacho katika nyumba na maktaba yake ni mavolumu na mavolumu ya majarida na mabuku na mabuku ya taaluma yake ya udaktari.

Kosa lake Dr. Jahazi ilikuwa ni yake mapenzi yake katika dini yake na kuenzi kivazi chake cha kanzu na kilemba hata anapokuwa darasani Chuo Kikuu Muhimbili akihadhiri.

Allah ampe kaka yangu Dr. Jahazi kauli thabit na amweke mahali pema peponi.

Amin.

Jeneza likitoka Msikiti wa Shadhly

Maziko ya Dr. Jahazi Makaburi ya Kisutu
Wednesday, 7 June 2017

Mufri Sheikh Abubakar Zubeir akiongoza Sala ya Jeneza
Amenipigia simu mhariri wa gazeti moja maarufu akiniomba niandike taazia ya Cisco kwa gazeti lake litokalo kila juma. Nikamjibu kuwa hakika namfahamu Balozi Cisco Mtiro kwa miaka nenda miaka rudi lakini sijui niseme nini kuhusu yeye. Nikamshauri amjaribu Balozi Mohamed Maharage Juma maarufu kwa sisi tuliokuwa karibu na yeye kwa jina la ‘’Sancho.’’ Hakika kama kuna mtu anaweza kumweleza Cisco basi ni yeye Balozi Maharage. Wakati tunanyanyukia mjini Dar es Salaam kila mtu alikuwa na jina lake la kupanga, yaani, ‘’nickname,’’ na majina haya wakati mwingine yalimganda na kumwenea mtu kiasi ya kuua jina lake halisi alilopewa na wazazi wake. Hili ndilo lililomfika Abdulkarim Omar Mtiro. Ilikuwa ukimuuliza Cisco kwa jina la Abdulkarim utahangaika sana lakini ukitaja jina la Cisco hata jiwe litakuelekeza nyumbani kwake.

Cisco alizaliwa Mtaa wa Kipata baadae baba yake akahamia Temeke na huko ndiko alikokulia. Mimi binafsi kila Balozi Cisco anapokuja katika fikra zangu basi atafuatia na Balozi Mohamed Maharage Juma. Si kwa sababu ya wao kufanana kwa maumbo watu wa miraba minne au kwa kuwa wote waliingia katika kazi moja Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje la hasha, kinachonigusa mimi ni jinsi wawili hawa walivyoshabiana katika hulka zao ambazo hata kama utakutananao kwa mara moja tu basi wataacha alama katika kichwa chako kama si kuwa rafiki wa maisha. Mohamed Maharage alinipigia simu kuniuliza kama nilikuwa nina taarifa za msiba wa Cisco na akaniambia kuwa yeye tayari yuko nyumbani kwa Cisco pamoja na jamaa wengine na akaniomba nifanye hima niende mara moja. Alifanya hivi akijua ukaribu sote wawili tuliokuwanao na Cisco.


Add capRais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Sheikh Alhadi Mussa na
Paul Makonda wakitoka makaburini Kisutu baada ya mazikotion

Kama jana vile namkumbuka Cisco akija mjini katika, ‘’Boogie,’’ akiwa amepanda baiskeli yake nyeusi akitokea nyumbani kwao Temeke. Boogie ilikuwa ni dansi za mchana maarufu kwa sisi, ‘’teenagers.’’ Hii ilikuwa miaka ya katikati ya 1960 na wastani wa umri wetu ulikuwa miaka 15. Nawakumbuka vijana waliokuwa wakija mjini Arnautoglo Hall palipokuwa panachezwa boogie kutokea Temeke pamoja na Cisco. Kulikuwa na Moses jina halisi Mussa, Micky Jones, huyu jina lake ni Mikidadi, Allan Brown yeye ni Ali Ngotta akitoka katika familia maarufu sana Temeke. Hawa walikuwa vijana watanashati sana. Turudi katika baiskeli ya Cisco. Ukweli ni kuwa baiskeli ilikuwa haiendani na wakati ule na hali ile ya ule ujana tuliokuwanao. Unaweza kupanda baiskeli kuja shule lakini si kujanayo katika boogie. Huwezi kuja na baiskeli kwa kuwa utakuwa, ‘’umeuramba,’’ yaani umevaa vizuri sana sasa katika hali hiyo kuikwea baiskeli na kupiga pedali kutoka Temeke hadi mjini kwa kweli kutavuruga nguo achilia mbali hilo jasho litakalokutoka. Lakini Cisco toka utoto alikuwa mtu wa mikasa na vituko akiyafanya haya kwa makusudi ya dhati yake.

Cisco alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kuzungumza suala lolote kwa umakini wa hali ya juu iwe ni siasa, muziki, mpira nk. Lakini kubwa ambacho Allah alimjaalia Cisco ni kipaji chake cha kuchekesha huku uso wake ukiwa unakupa wewe taswira ya kuwa lile analokueleza ni kweli kabisa kwani uso wake haukutoa taswira kuwa anafanya maskhara. Nadhani kipaji hiki alikitumia vyema katika kazi yake ya diplomasia. Miaka michache iliyopita wakati Cisco amestaafu kazi nilimtembelea Balozi Maharage nyumbani kwake Makongo. Balozi Maharage alikuwa likizo akitokea Abu Dhabi alikokuwa balozi wa Tanzania akiwa pia akiwakilisha na Iran. Balozi Maharage akanambia kuwa Cisco alipostaafu kampigia simu akiwa ofisini kwake Abu Dhabi kumpandisha midadi, akimwambia kuwa yeye anapiga simu ile akiwa Butiama Hoteli na tayari ameshatoa oda ya biriani anaisubiri iletwe mezani pake aishughulikie.

Hii Butiama Hoteli ina nafasi ya pekee katika nyoyo zetu sisi vijana wa zamani. Hii ilikuwa moja ya hoteli maarufu Magomeni Mapipa na ikiwa imemtokea mtu kuwa yuko mitaa ya Magomeni ilikuwa hakosi kuingia hapo kupata biriani yake iliyokuwa inapikwa kwa umahiri mkubwa. Hii kama utakuwa Magomeni wakati wa chakula cha mchana. Lakini ikitokea kuwa uko mjini basi hoteli itakuwa Royal Restaurant, Zahir au Khalid migahawa hii yote ilikuwa ikipika chakula kizuri sana na umaarufu wao mkubwa sana ilikuwa ni upishi wa biriani. Miaka ikapita na sisi tukakua tukatoka katika utoto na ujana tukawa watu wazima si kwa umri tu bali hata kwa nafasi kiasi ambacho ikawa tumepita kuingia baadhi ya migahawa ambayo katika ujana wetu tulikuwa hatupungui. Kama nilivyotangulia kusema, Cisco alikuwa mtu wa mikasa na kupenda kukufanya ucheke na ufurahi. Usingetegemea balozi mzima leo aingie Butiama Hoteli kwenda kula biriani kisha akabishana Simba na Yanga na wahudumu wake. Balozi Cisco hakuwa limbukeni.

Kulia: Balozi Cisco Mtiro, Mwalimu Julius Nyerere na Nelson Mandela


Wapi ambako mguu wake haukutua katika dunia hii akifuatana na maraisi wote waliotawala Tanzania, achilia mbali kusuguana mabega na wakubwa wa dunia kama Bill Clinton na Nelson Mandela, kuwataja wachache. Hapa wala sitaki kugusa alipokuwa na Mwalimu Nyerere akizungukanae kote duniani wakati wa South to South Commision ya Mwalimu Nyerere. Mafanikio haya yote na ukubwa na ukuu wake wote huu haukumvuruga kichwa chake. Barza zake na marafiki zake ni wale wale akina Mohamed Said, Ali Ngota na Ali Mzuzuri waliokuwa pamoja toka utotoni. Mimi nilikuwa ni yule yule ‘’Sidney,’’ rafiki yake wa udogoni na alipokuwa akijisikia atanikumbuka katika, ‘’whatsapp,’’ kwa kuniwekea ‘’clip,’’ ya Earl Klugh mpiga gitaa wa jazz maarufu ambae sote mimi na yeye tukimpenda kwa miaka au, ''clip,'' ya mpiga jazz yeyote yule. Nami kwa kukataa kushindwa na kutaka kuoneshana mizungu nitamrushia, ''clip,'' ya Wes Montgomery, mpiga gitaa nguli lakini wa enzi kabla ya Earl Klugh.

Kulia: Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande, Mkuu wa Usalama wa Taifa Mstaafu Rashid
Othman na Benard Membe Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje Mstaafu


Butiama bila shaka palimkumbusha mengi na njia ndefu aliyopita hadi kufikia pale alipofika akiwa na ofisi ndani ya Ikulu ya Jamburi ya Muungano wa Tanzania. Wafanyakazi wa Butiama wengi wao ni wale wale na wengi wana Yanga wenzake na bila shaka alipata wasaa wa kukumbushana enzi zilizopita na kucheka pamoja kisha kuwaachia, ‘’tip,’’ nono. Karibu na Butiama Hoteli ilikuwapo hoteli ya marehemu Shomvi Yanga mwenzake na hoteli yake ‘’Michuzi Mikali.’’ Shomvi akapichikwa jina Shomvi Michuzi Mikali. Shomvi yeye alijikita katika kuku wa kukaanga aliotoa kwa ugali au wali. Shomvi alikuwa anatengeneza pilipili ya ajabu chachandu nzuri kabisa iliyokwenda sawia na kuku wake wa kukaanga.

Hivi vyote vilikuwa viwanja vyetu katika miaka ile ya 1970 tukiwa vijana. Sehemu hizi si tu mtu alikuwa anapata chakula kizuri bali alikuwa anapata pia maongezi mazuri ya ushabiki wa Simba na Yanga na wakati mwingine wachezaji wa timu hizi hujumuika pale kwa chakula cha mchana. Na wapenzi walikuwa hawabagui ikiwa watalipa chakula basi watawalipia wote wachezaji wa  Yanga na Simba bila matatizo na kwa utani kidogo kama vile, ‘’Maulid kula nguvu yetu Simba uje utufunge tena,’’ na watu wote watacheka na kufurahi pamoja. Huyu Maulid alikuwa marehemu Maulid Dilunga, mshambuliaji mkali wa Yanga.

Pale alipokuwa ndani ya Butiama Hotel,Cisco aliweza kuona Shibam Hotel vizuri kabisa kwani ukivuka Barabara ya Morogoro ndipo ilipo Shibam hadi leo, ilipokuwa barza ya marehemu Mkanga shabiki mkubwa wa Simba toka enzi za Sunderland. Miaka mingi ya kuwa Balozi Cisco nje ya nchi haikumtenganisha Cisco na ndugu zake. Alikuwakumbuka na kuwasaidia rafiki zake alioukuwanao African Temeke na Good Hope za Temeke. Timu hizi za mchangani huko Temeke kwao Balozi Cisco ndizo zikitoa wachezaji hodari vijana kuja Yanga na Simba katika miaka ile kama akina Lenard Chitete na Shaibu Ngotta kuja Simba na Yanga.

Balozi Cisco kiti chake kilikuwapo Leaders Club lakini halikadhalika hakusahau kijiwe chake cha mtaani kilichomkuza. Meza yake ilikuwapo katika mahoteli makubwa ya sifa duniani lakini haikumpa shida kuja kula Butiama na kuwasalimia nduguze.

Turudi hoteli ya Butiama na biriani.

Cisco alijua hii ya Butiama atakuwa amemkomesha rafiki yake Balozi Maharage. Ndipo aliponyanyua simu yake ya bei kali akampigia kumfahamisha kuwa yeye yuko hapo Butiama anakula biriani. Balozi Cisco akamaliza mazungumzo yake kwa kumtahadharisha balozi mwenzake kuwa achukue tahadhari ya kuacha ofisi mapema apate mafao yake maana shilingi inaweza kuporomoka na yeye akatoka kapungukiwa pakubwa.  Balozi Maharage alipomaliza kunihadithia salamu na indhari aliyopewa na Cisco akaanza kucheka na mimi sikuweza kustahamili tukawa sote tunacheka na kupiga gonga. Hakika Cisco hawezekani tulikubaliana sote.

Siku moja niko darasani Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam mwalimu Mzungu kutoka Uholanzi akitusomesha kozi, ‘’Politics of Industrial States,’’ bila shaka alikuwa kahisi jambo kwetu sisi wanafunzi wake akasema kutuambia kuwa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje inashangazwa na kiwango cha chini cha miaka ya karibuni ya vijana kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam waliokuwa wanajiunga na wizara hiyo. Mwalimu akaendelea kusema kuwa kulikuwa na wakati hakika chuo kilikuwa kikitoa wahitimu hodari katika nyanja zote kuanzia lugha, Kiingereza na Kifaransa hadi ujuzi wa siasa za dunia. Akamaliza kwa kusema kuwa wizara inashangaa kimepitika nini kuwa vijana kama hawa ghafla wamepotea.

Cisco alikuwa ameingia Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje akiwa mmoja wa kundi hili la vijana, ‘’smart,’’ wa ‘’Foreign,’’ ambao walikuwa wa kupigiwa mfano na baadhi nikiwafahamu kama Eliud Aickim ‘’Brown,’’ Mwandembwa, Ami Mpungwe, Kassim Mwawado, marehemu Gasper Yusuf Hakili kwa kuwataja wachache. Vijana hawa walikuwa na, ''sophistication,'' ya aina yake kuanzia, ''etiquettes,'' hadi mavazi. Naukumbuka sana utanashati wa Cisco akiniacha mie kwa mbali sana.

Iko siku mimi na Mohamed Maharage tuko London Underground tunasubiri treni. Pembeni yetu walikuwa wamekaa viajana wa Kifaransa na walikuwa wanazungumza Kifaransa. Katika kusubiri kule hawa vijana ambao walikuwa watalii, maana walikuwa wakipiga picha nyingi mimi na Mohamed tukawa tunaingia katika picha zao. Mmoja kati yao, kijana wa kiume akawa anazangumza na binti aliyekuwanae kisha wanacheka kwa sauti kubwa. Mara nikaona Mohamed kawageukia na anaanza kuzungumza nao Kifaransa kwa kama dakika mbili tatu. Kutokana na jinsi niliyomuona yule kijana wa kiume anazungumza na Mohamed nikahisi pale pamepitika jambo.

Kweli kwa hakika palikuwa pamepitika jambo. Yule kijana alituita mimi na Mohamed ‘’maua meusi,’’  akimwambia mmoja wa wale akina dada kuwa picha zao zitapendeza sana kwa kurembwa na ‘’maua meusi,’’ ya London. Alisema maneno haya kwa Kifaransa. Hapo ndipo Mohamed akawageukia na kuwaambia kwa lugha hiyo hiyo yao kuwa, ‘’Basi ingawa mmeyapenda, ‘’maua meusi,’’ ingependeza kama mngeyaomba ruhusa kabla hamjayapiga picha. Vijana wenzetu Wafaransa wakatutaka radhi. Hawa ndiyo akina Cisco, vijana, ‘’smart’’ wa Foreign Affairs,’’ wa enzi zile. Mambo haya yametokea sasa zaidi ya miaka 30 imepita.

Balozi Mohamed Maharage Juma

Nimempa pole Balozi Mohamed Maharage kwa kuwa najua yeye msiba wa Cisco ni mkubwa sana juu yake umemuelemea kwa kuwa ameishi na Cisco kwa miaka mingi toka udogo wao hadi kufika kufanyakazi pamoja Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje kisha kustaafu na kuwa pamoja. Halikadhalika nimempa pole Ali Mzuzuru rafiki kipenzi wa Cisco toka utoto wao na ambao wazee wao walikuwa kati ya wazee wa Temeke waliojenga Msikiti wa Tumbi, Temeke wakisaidiwa na Aga Khan wakati wa enzi za East African Muslim Welfare Society (EAMWS).

Kushoto: Salum Matimbwa, Shaibu Ngotta
Nyuma Kulia: Ali Ngotta, Magombe Makongoro na Hamisi Chenja
Nyuma wa pili kulia Ilyas Abdulwahid Sykes

Nimempa pole Micky Jones ambae kanineletea picha akiwa na Cisco VIP Longe Copenhagen pamoja na Rais Kikwete alipokwenda huko. Nimempa mkono wa pole Ali Ngotta na mdogo wake Shaibu Ngotta. Nikiwapa pole na hawa wote hawa wote wakawa wananirejeshea mimi pole wakinambia na mimi pia nipoe.

Iko siku wakiwa safarini Cisco alimchekesha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere hadi machozi yakammwagika.

Lakini kisa hiki In Shaa Allah nakitafutia siku yake.
There was never a dull moment with Cisco.

Ali ''Stone'' Mzuzuri

Hakika Cisco amevuka milima na mabonde kutoka Kipata na Temeke hadi kufika duniani. Tunamuomba Allah amweke ndugu yetu Abdulkarim Omar Mtiro mahali pema peponi.


Amin


Cisco na Mwandishi katika Khitma ya Saigon 2010
Kulia: Cisco Mtiro, Bi. Mtoro bint Mohamed, Ibrahim Pamba na Mwandishi ni huyo chini
siku Cisco na Ibrahim Pamba mtoto wa mama yangu mdogo Bi. Mtoro walipopata shahada zao
mwaka wa 1979. Kwa miaka mitatu mfululizo Ibrahim alichukua zawadi ya Best Student (Chemistry)
hao wote watatu wametangulia mbele ya haki.
(Picha imepigwa na Said Ibrahim)

Monday, 5 June 2017


Abdulkarim Omar Mtiro (Cisco)

Maskini kaka yangu "Cisco" umetangulia mbele ya haki.

Huyu kwangu mimi ni baba maana marehemu mzee wangu Abdallah Salim Matimbwa alikuwa ni mmoja wanaosoma katika darsa ya marehemu Sheikh Omar Mtiro hapa Mtaa wa Kipata nyumba no. 1 ambae ni baba yake Abdulkarim Mtiro maarufu kwa jina la, ''Cisco.''

Hii nyumba no. 1 Mtaa wa Kipata na Msimbazi na Congo ndimo alimozaliwa Cisco. 

Nyumba yetu ni no. 2 kwa hiyo nyumba zetu zikitazamana miaka nenda miaka rudi na wazee wakifahamiana vyema kabisa.

Mwezi kama huu wa Ramadhani enzi hizo chano kiko barazani kwa Sheikh Omar Mtiro,  uji unapikwa kwetu na mama yangu na futari zote zinapelekwa kwa Bibi bint Seif (mama yake mzazi Cisco).

Dar es Salaam hii ya miaka ile ya 1950 wakati sisi tunazaliwa leo haipo tena.

Kwa daraja hiyo niliyoizungumza hapo juu, ya baba yangu Mzee Abdallah bin Salim Matimbwa kuwa mwanafunzi wa Sheikh Omari bin Mtiro, kwa nidhamu ya Kiislamu Sheikh Mtiro anakuwa babu yangu na Abdulkarim Mtiro, mwanae anakuwa baba yangu kwa maana yeye anamwita baba yangu kaka yake ki daraja.

Kwa umri aliokuwanao baba yangu anamzaa Abdulkarim pasi na shaka yoyote lakini ada ni ada Abdulkarim alibaki kuwa mdogo wake na kwangu baba.

Dada yangu wa kwanza Bi. Hidaya bint Abdallah Salim watoto wake kina marehemu Shaaban Juma Semlangwa Assistant Commissioner of Police (ACP) na dada yake Bi Mwanahawa Juma ndiyo walikuwa mchezo mmoja na Balozi Cisco katika utoto wao.

Hivyo nimeondokewa na baba yangu, kaka yangu, mzaliwa mwenzangu mtaani Kipata (sasa Mtaa wa Kleist Sykes) na kiongozi wangu katika nyanja mbalimbali.

Mwenyezi Mungu amuondolee adhabu ya kaburi na amsamehe makosa yake.
Aiweke roho yake mahala pema peponi.


Amin.

Tuesday, 30 May 2017


Kitwana Selemani Kondo katika ujana

BURIANI MZEE KITWANA KONDO

Ramadhani K Dau

Siku ya Jumatano tarehe 24 Mei 2017 ni siku ambayo itakumbukwa na Watanzania wengi na haswa Waislamu kwa kuondokewa na mzee wetu Alhaj Kitwana Selemani Kondo maarufu “KK” au mzee wa mjini. Siku 4 kabla ya kifo chake, mwanawe wa kiume Bwana Adnan-Msakuzi alinitumia ujumbe kwenye WhatsApp akiniarifu kuwa Mzee KK amelazwa Hindu Mandal na hali ya afya yake inazidi kuzorota. Siku ya pili yake nilimtumia ujumbe Adnan-Msakuzi kutaka kujua hali ya Mzee inaendeleaje. Majibu ya Adnan yaliniashiria kuwa mzee wetu amekaribia kufika mwisho wa safari yake hapa duniani. Aliniambia kuwa kwa sababu ya ukaribu wangu na Mzee KK hanabudi aniarifu ukweli ulivyo. Aliniarifu kuwa hali ya mzee ni mbaya sana na kwamba kinachosubiriwa na Rehma Zake Mwenyezi Mungu. Kwa kweli ujumbe ule ulinihuzunisha sana na sikuweza kuhimili uchungu ule peke yangu. Nikamwarifu Profesa Hamza Mustafa Njozi, Makamu Mkuu wa Chuo cha Waislamu Morogoro na Bwana Faraji Abdallah Tamim, mwalimu wa chuoni hapo.

Ilipofika siku ya Jumatano tarehe 24 Mei nikapata taarifa kupitia moja ya kundi sogozi (chat group) kuwa Mzee KK amefariki dunia. Pamoja ya kuwa hali hiyo ilikuwa tayari inatawala fikra zangu tokea siku niliyopata ujumbe kutoka kwa Adan lakini kifo hakizoeleki. Taarifa hiyo ilinikuta nikiwa najiandaa kwenda uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur kumsindikiza shemeji yangu. Wakati huo kwa saa za Malaysia ilikuwa kiasi cha saa 4 usiku. Nilipwelewa sana kwa sababu ya uhalisia kuwa sitowahi kumzika mzee wangu Mzee KK. Haikuchukua dakika 10 baada ya taarifa hizo, Adnan kanipigia simu ambayo hatukuweza kuzungumza hata neno moja kutokana na vilio vyetu. Kila mmoja alikuwa analilia kwake. Ghafla akakata simu na kunitumia ujumbe mfupi uliosema “KK is dead. Allah is Great”. Mara tu baada ya kupata taarifa hiyo nilichanganyikiwa na kuona uchungu sana baada ya kuona kuwa sitoweza kumzika Mzee KK ambaye aliwahi kunitamkia mbele ya mkewe Bi Hanifa kuwa ikitokea atafariki kabla mimi basi angependa asaliwe Masjid Mtoro, azikwe makaburi ya Tambaza na mimi niwe mmoja kati ya watu watakaoingia kaburini. 

Katika maishani mwangu, hii ni mara ya tano kuandika taazia yaani “obituary”. Buriani zilizotangulia ni za aliyekuwa mwalimu wangu Chuo Kikuu DSM na rafiki yangu wa karibu Profesa Ken Edwards mwenye asili ya Jamaika, aliyekuwa Afisa wa Uhusiano wa NSSF Alfred Ngotezi, rafiki yangu tokea utotoni Abubakar Mohamed Saleh Tambaza maarufu “Babu Chela” na Saidi Masimango aliyekuwa Mkurugenzi wa Teknohama NSSF.  Kila niandikapo taazia huwa nafanya hivyo nikiwa na moyo mzito na huzuni sana. Kila niandikapo huwa naomba kuwa hiyo iwe ndio ya mwisho kwani kuandika taazia ni jambo zito sana haswa ikiwa inamuhusu mtu wa karibu yako kama nilivyo mimi kwa Mzee KK na hao waliotangulia kabla yake.

Kwa huzuni niliyokuwa nayo niliamua kutoandika taazia hii kwa sababu nisingeweza kufikia mwisho kwa kilio. Lakini mara tu baada ya habari za msiba kuenea nikaanza kupata salaam toka kwa watu mbali mbali akiwemo Prof Hamza Njozi, mdogo wangu Abdul Dau na Adnan-Msakuzi. Ujumbe kutoka kwa Adnan ndio ulizidisha majonzi yangu lakini pia ulinipa nguvu ya kuandika kwani kama alivyosema Adnan na nakuu “Dr please write a eulogy for KK. You knew him well, no one can talk of him better than you”. Baada ya kutafakari nikaona kama sikuandika ntakuwa sikumtendea haki Mzee Kondo. Kwa kuwa nimekosa fursa ya kumtimizia wosia wake kuwa niwe miongoni mwa watu watakaoingia kaburini kumzika, nimeona nisikose vyote.  Kwa kuzingatia kanuni ya fiqh kuwa kama jambo haliwezi kufanyika lote basi lisiachwe lote. Waswahili nao wana msemo wao “lisobudi hutendwa”. Hivyo basi nimeamua kuandika taazia hii kwa huzuni na unyonge mkubwa.

Mzee Kitwana Selemani Kondo alizaliwa Mtoni Kijichi, Dar es Salaam tarehe 1 Agosti 1930. Pale Mtoni Kijichi ukoo wake ni ulijulikana kwa jina la Mahembe. Wazazi wake wote wawili ni Wazaramo. Kiumeni kwake ni Mtoni Kijichi na kikeni kwake kijiji cha Gumba, Kisarawe. Alipata elimu ya msingi Mchikichini kisha akaenda Tabora Boys na baadae Chuo Kikuu cha Howard kilichopo Washington DC, Marekani. Pia Mzee Kondo alichukua masomo ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa darasa moja na marehemu Sheikh Mohamed Ali Al-Buhry.

Kwa upande wa kazi, Mzee Kondo alikuwa Polisi kwa muda mrefu hadi kufikia ngazi ya Inspekta na baadae akawa Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje, marehemu Oscar Kambona. Wakati wa uhai wake Mzee KK ameongoza Taasisi kadhaa za Umma zikiwemo Shirika la Magari la Taifa yaani State Motors Corporation (Mkurugenzi Mkuu), Mwenyekiti wa Bodi za TANESCO, Mamlaka ya Bandari na Bodi ya Korosho. Wakati wa uhai wake, Mzee Kondo alijaaliwa kupata watoto 8. Kati ya hao wanaume 3 na wanawake 5.

Nimemfahamu Mzee tokea nikiwa mdogo kwa sababu ya kuzaliwa na kulelewa Mwembetogwa, jijini Dar es Salaam. Wakati wa utoto wangu sikuwa na ukaribu sana na Mzee Kondo kwa sababu ya tofauti ya umri. Ukaribu wangu kwake ulianza mwaka 1995 wakati alipoteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA) ambapo mimi nilikuwa Mkurugenzi wa Masoko kwa miaka tisa. Nakumbuka siku moja mara tu baada ya kumaliza kikao cha Bodi niliamua kumsindikiza mpaka kwenye maegesho ya gari. Baada ya kufika kwenye gari yake, nikaona nichukue fursa hiyo nijitambulishe zaidi kwake kwani mpaka wakati huo alikuwa ananifahamu kama Mkurugenzi wa Masoko. Nikajitambulisha kuwa mimi nimezaliwa na nina asili ya Dar es Salaam.

Mara tu baada ya kumwambia hivyo haraka kabisa akaniuliza baba yangu nani. Ili kumtosheleza kiu chake sikutaka kumtambulisha baba yangu. Badala yake, na kwa makusudi kabisa nikamwambia mimi ni mtoto wa “John” Iddi. Mara tu nilivyojitambulisha akasema “wewe mwanangu, “John” Iddi alikuwa mkwe wangu”. Nilifanya makusudi kumtaja “John” Iddi ambaye ni baba yangu mkubwa. Jina lake halisi ni Thabit Iddi Dau. Jina la “John” aliitwa na mama yake baada ya kumzaa akiwa ana umri mkubwa sana. Baada ya kujifungua akasema mtoto huyu nimempata “Jioni” kwa maana ya kuwa amemzaa hali ya kuwa yeye ana umri mkubwa sana na alikwisha kata tamaa ya kupata mtoto.  Pamoja ya kuwa jina lake halisi lilikuwa Thabit lakini tokea utotoni alijulikana kwa jina la “Jioni” ingawa kwa urahisi wa matamshi badala ya kusema “Jioni” likavuma jina la “John”. Marehemu Bwana Thabiti alijulikana sana kwa jina hilo la utani hadi kufa kwake.

Nimesema niliamua kujitambulisha kupitia baba yangu mkubwa kwa makusudi kwa sababu Mzee Kondo aliwahi kumuoa Bibi Kijakazi wa Mgoto ambaye alikuwa anafanyakazi Halmashauri ya Jiji (City Council). Kwa bahati mbaya hawakuwahi kupata mtoto. Katika ndoa yake nyingine, Bibi Kijakazi alijaaliwa mtoto wa kike ambaye jina lake ni Kurwa. Sasa huyu Bibi Kurwa ndiyo aliyekuwa mke wa kwanza wa marehemu Mzee “John” Iddi. Katika uhai wao walijaaliwa kupata watoto wawili. Iddi “John” na Mwatatu Thabit. Iddi alifariki mwaka 2001. Mwatatu yu hai ameolewa na Mohamed Mfaume maarufu “Difu” ambaye alikuwa golikipa wa Yanga, Cosmo na Timu ya Taifa. Mpaka sasa Mwatatu anaishi Kariakoo mtaa wa Swahili kwenye nyumba ya urithi wa mama yake.

Kinasaba, Mzee Kondo alikuwa anamwita Mzee “John” Iddi mkwe kwa sababu yeye (Mzee KK) alimuoa Bibi Kijakazi ambaye alikuwa mkwe wa Mzee “John” Iddi. Kwa upande mwingine, marehemu Mzee “John” Iddi (Thabit Iddi Dau) na marehemu baba yangu mzazi (Kitwana Ramadhani Dau) ni mtu na kaka yake. Wazungu wanasema ni first cousins, sisi Waswahili tunasema wamezaliwa nyumba kubwa na ndogo (kwa maana ya baba mkubwa na baba mdogo) au kwa lugha nyingine tunawaita watoto wa Simba kwa Simba. Kwa hiyo kinasaba, uhusiano wangu na Mzee Kondo ni kwa kupitia baba yangu mkubwa marehemu Mzee “John” Iddi Dau.

Tokea siku ile ambayo nilijitambulisha kwa Mzee Kondo, tukajenga ukaribu sana na alikuwa ananipenda sana. Ilikuwa haipiti wiki bila kwenda nyumbani kwake Hill Road Oyster Bay na baadae mtaa wa Mtitu Upanga kwenda kumwamkia na “kupata habari za mjini”.  Ni kutokana na mazoea hayo ndipo Mzee KK akapata jina lingine la utani la “mzee wa mjini”. Na ni kweli, wakati wa uhai wake, kila utakapoenda nyumbani kwa Mzee KK hukosi kupata “habari za mjini” ingawa wakati mwingine zinakuwa ni habari au fikra zake yeye lakini ili kuzipa uzito atakwambia kuna habari mjini kuwa …(hapo anaeleza hiyo habari ilivyo). Moja katika hizo habari za mjini zilininufaisha sana na kuninusuru na janga kubwa sana ambalo lingenikuta. Leo hapa si mahala pake kuzungumzia habari hiyo. In Shaa Allah kuna siku ntaitafutia nafasi kuizungumza.  Naendelea kumshukuru sana kwa hilo na mengine mengi ambayo amenifanyia mimi na watu wengine wengi.

Mzee KK atakumbukwa na kuliliwa na wengi kwani alikuwa mwepesi sana kusaidia watu wenye shida. Marehemu alikuwa mcheshi na mwenye kupenda maskhara sana. Alichanganyika na watu wa kila rika. Alikuwa mtu wa msaada sana kwa watu wa aina zote, wake kwa waume. Nyumbani kwake kulikuwa hawapungui wageni wa kila aina kuanzia wanasiasa, wana michezo, viongozi wa dini nk. Mmoja kati ya watu wengi waliosaidiwa na Mzee Kondo ni marehemu Profesa Idrisa Ali Mtulia. Wakati wa uhai wake, Profesa Mtulia alinisimulia namna ambavyo marehemu Mzee Kondo alivyomsaidia kwenda kusoma Uingereza. IIikuwa mwaka 1978 wakati Profesa Mtulia alipochaguliwa kwenda kusoma Clinical Fellowship kwa miaka miwili kwenye hospitali ya Hammersmith ambayo ni sehemu ya Chuo cha Imperial London, Uingereza. Gharama zote za masomo zilikuwa zilipwe na Serikali. Kwa bahati mbaya siku chache kabla ya safari, jina la Profesa Mtulia halikuwemo kwenye orodha. Profesa akawa hana la kufanya. Akaamua kwenda kuomba msaada kwa Mzee Kitwana Kondo. Mzee Kondo akamhakikishia kuwa ataenda kusoma mwaka ule ule na wala asiwe na hofu. Mzee Kondo akazungumza na Karimjee na baada ya siku 4 tu Profesa Mtulia akapata udhamini kamili (full scholarship), ambao ulijumuisha tiketi ya ndege na fedha zote za matumizi akiwa Chuoni. Udhamini huo ulitolewa na mama yake mzazi Karimjee. Kutokana na masomo hayo, Profesa Mtulia akatunukiwa kuwa Member of Royal College of Physicians (MRCP) na baada ya kudhihirisha umahiri wake akatunukiwa kuwa Fellow of Royal College of Physicians (FRCP). Profesa Mtulia alikuwa ni mmoja kati ya watu wengi waliosaidiwa na Mzee KK.  Baada ya kurudi masomoni na baadaye kutunukiwa FRCP, Watanzania waliokuwa na hadhi hiyo walikuwa wachache sana; nadhani hawakufika 5. Mmoja kati ya hao alikuwa marehemu Dr. Aaron Chiduo; wengine nadhani ni Profesa William Makene na Profesa Shaba.

Kwa upande wa siasa Mzee Kondo ametoa mchango mkubwa sana kwa muda wote wa uhai wake nje na ndani ya Serikali, Bunge, TANU na CCM. Mzee KK alikuwa mzalendo ambaye aliitakia sana mema nchi yetu. Kwa wale wazee wa Dar es Salaam waliobaki watakumbuka sana mchango alioutoa tokea wakati wa Ukoloni na haswa baada ya Uhuru. Yapo mengi ya kihistoria aliyoyafanya kwa kuinusuru nchi yetu na kufika hapa ilipofika leo.  Mambo mengine hapa si mahala pake.

Moja kati ya sifa zake nyingi ni ujasiri. Mzee KK hakuwa mwoga na alikuwa na ujasiri wa kusimamia jambo ambalo anaamini ni sahihi na lina manufaa kwa nchi yetu. Mifano iko mingi. Kwa leo itoshe tu kuwa alisimamia suala la upatikanaji wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro kwa kujenga hoja kwa Rais wa wakati huo Mhe Benjamin William Mkapa mpaka Mhe Rais akashawishika kuwa ni jambo jema kuanzishwa kwa chuo hicho kwenye majengo ya kilichokuwa Chuo cha Mafunzo cha TANESCO. Kama kuna mtu mmoja ambaye ametoa mchango wa kipekee uliopelekea upatikanaji wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) mtu huyo ni Mzee Kitwana Selemani Kondo. Kwa kuenzi jitihada zake hizo, na kwa kuzingatia Mzee Kondo ni Mwenyekiti mwanzilishi wa Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF), Taasisi ambayo ndiyo Mmiliki wa MUM, nashauri uongozi wa Chuo ubadili jina la kampasi ya Morogoro iitwe Muslim University of Morogoro, Kitwana Kondo Campus.  Natoa rai hiyo kwa kujua kuwa Chuo kina mpango wa kujenga kampasi nyingine Lindi (Kitunda), Kilwa (Mpara), Morogoro (Sangasanga) na Dar es Salaam (Kigamboni). Kwa siku za usoni, Chuo kitakapoanza kutoa Shahada za Uzamivu (PhD), nashauri Mzee Kitwana Kondo atunukiwe PhD (Honoris Causa) posthumously

Kwa kawaida, Shahada ya Uzamivu ya Heshima, yaani PhD (Honoris Causa), ndiyo shahada ya juu zaidi katika Chuo Kikuu chochote. Shahada hii hutolewa kwa watu ambao wanaoheshimika sana na ambao wametoa mchango mkubwa katika jamii kwenye nyanja mbalimbali. Mchango wa Mzee Kondo katika nchi yetu hauna mithali. Aidha Mzee KK alikuwa mwepesi sana wa kuelewa vitu (sharp) na mtu wa mikakati sana. Hakuna alilofanya bila kufikiria nini kinachoweza kutokea usoni na ni namna gani anaweza kuikabili hiyo hali. Nimeyashuhudia hayo wakati akiongoza vikao vya Bodi ya Mamlaka ya Bandari na ushiriki wake katika vikao vya maandalizi ya kuazishwa kwa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro. Kwa wote ambao wamewahi kufanyakazi na Mzee Kondo, watakubaliana nami kuwa staha yake, weledi wake, busara zake na mchango wa katika taifa letu anastahili kutunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima, yaani PhD (Honoris Causa).

Wakati alipokuwa Meya wa Jiji, Mzee Kondo alithamini sana mchango wa watu mbalimbali walioshiriki katika harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika. Ili kuweka kumbukumbu kwa vizazi vijao, Mzee Kondo aliwashawishi madiwani wenziwe kupitisha azimio la kubadili majina ya baadhi ya mitaa ya Dar es Salaam ili ipewe majina ya wazee wetu wa Dar es Salaam walioshiriki kwenye harakati hizo. Utaratibu uliotumika ni kuupa jina la mtaa kwa kila Mzee ambaye alieishi katika mtaa huo. Mifano ya mitaa iliyobadilishwa majina ni mtaa wa Kipata (Kleist Sykes), mtaa wa Tandamti (Mshume Kiyate), mtaa wa Aggrey (Makisi Mbwana), mtaa wa Somali (Omari Londo), mtaa wa Ndanda (John Rupia) na mtaa wa Mwananyamala (MwinyiJuma MwinyiKambi). Jambo la kusikitisha ni kuwa hadi leo baadhi ya mitaa hiyo haijawekwa vibao vya majina mapya. Ili kuendeleza dhamira nzuri ya kuwaenzi wazee wetu waliotoa mchango mkubwa katika nchi yetu naishauri Manispaa ya Ilala ibadili jina la mtaa wa Mtitu ambapo alikuwa anaishi marehemu Mzee Kondo na kuitwa mtaa wa Kitwana Kondo.

Sambamba na ujasiri, Mzee KK alikuwa anaipenda sana dini yake na alikuwa mtetezi mkubwa wa Waislamu. Ilikuwa kila ukienda nyumbani kwake ukimtajia Aya kwenye Quran basi haraka huchukua kitabu chake kidogo (note book) na kuiandika ili akaifanyie kazi kwa vitendo au hata kwa kuzungumza kwa wengine. Miongoni mwa Aya ambazo Mzee KK alikuwa akizipenda sana ni Aya ya 10 na ya 11 kwenye Sura ya 61 (As-Saff), pia Aya ya 31 kwenye Sura ya 76 (Al-Insan au kwa jina lingine Dahr). Kwa kumuenzi Mzee KK sitotoa tafsiri ya Aya hizo kwa makusudi ili msomaji upate ushawishi wa kwenda kuzisoma mwenyewe ili nawe upate fadhila za kuisoma Quran. Katika kuonesha mapenzi aliyonayo kwa dini yake, siku zote Mzee Kondo alikuwa mstari wa mbele kuchangia maendeleo ya Waislamu. Moja katika jitihada zake nyingi ni kupatikana kwa kiwanja ambacho kimejengwa Masjid Maamur, Upanga.

Mzee Kondo alijivunia sana Uswahili na Uzaramo wake. Watoto wake wengi aliwapa majina ya Kizaramo kama vile Mtogole, Azimala, Msakuzi nk. Pamoja na nyadhifa mbalimbali alizokuwa nazo Serikalini, kamwe Mzee Kondo hakusahau marafiki zake ambao wengi wao walikuwa ni watu wa kipato cha chini sana. Baadhi yao ni marehemu Mzee Kibiriti, marehemu Mzee Sindano, marehemu Omar AbdulRahman maarufu “Ugundo”, Mzee Gulu, Captain Maliki, marehemu Ramadhani Mangilile, marehemu Ali Abbasi, na marehemu Mapepe. Wengine ni marehemu Hamisi George, marehemu Abbas Mzee, marehemu Saleh Mtumwa, marehemu Maalim Mbegu wote wa Egyptian Musical Club. Hao na wengine wengi wanaofanana na hao ndiyo waliokuwa wazungumzaji wa Mzee KK. Ilikuwa haipiti mwezi bila ya Mzee Kondo kwenda Kariakoo (na haswa klabu ya PAN) kwenda kupiga soga na watu wa mjini wenziwe.

Ukaribu wake na watu wa kawaida umefanya mpaka baadhi ya watu wafikirie kuwa Mzee Kondo hakusoma shule. Nakumbuka mwaka 1996 wakati Mzee Kondo akiwa Mwenyekiti wa Bandari nilikwenda Shirika la Bima ya Taifa (NIC) kufuatilia madai ya gari yangu MUSSO TZH 3336 ambayo ilipata ajali. Nilifika NIC na kuonana na Afisa mhusika wa madai. Katika mazungumzo yetu akabaini kuwa mimi ni Mkurugenzi wa Masoko wa THA. Alinipa pole sana kwa sababu kwa maneno yake mwenyewe, THA tumepata Mwenyekiti ambaye hajui kusoma. Alishangaa Mzee Kondo anawezaje kusoma makabrasha na kuongoza vikao vya Bodi ikiwa hata kuzungumza Kiingereza hawezi. Nikamjibu kuwa Mzee Kondo ni msomi kwani mwaka 1963 alihitimu shahada kwenye “Strategic Studies” kwenye Chuo Kikuu cha Howard Washington DC, Marekani. Aidha Mzee KK amepata mafunzo kwenye nchi kadhaa zikiwemo Ujerumani na Yugoslavia. Yule afisa hakuamini na tukawa na malumbano makali sana. Msingi wa hoja yake ni kuwa mzee KK anaandikwa vibaya sana kwenye gazeti (pamoja ya kuwa kwa sasa gazeti hilo limekufa lakini jina nalihifadhi) na picha inayojitokeza ni kuwa mzee huyu hakusoma kabisa.  

Nimesema hapo awali kuwa Mzee Kondo alikuwa anajichanganya sana na watu wa aina na rika zote. Nina hakika si wengi wanaofahamu kuwa wakati wa uhai wake Mzee Kondo aliwahi kuwa Katibu wa klabu ya Yanga, Dar es Salaam miaka ya 1950s. Pia mwaka 1962 alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga. Wakati huo Mwenyekiti alikuwa Mzee Mohamed Sultan Mabosti, Katibu Mkuu ni Mzee Jabiri Katundu (alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Mzee Juma Vijiga) na Makamu wake Mzee Juma Shamte. Wote hao wameshatangulia isipokuwa Mzee Jabiri Katundu ambaye anaishi kwenye nyumba yake ile ile iliyopo Ilala mtaa wa Tabora. Tunamwomba Mwenyezi Mungu Ampe Mzee Jabiri umri mrefu na wenye tija ili tuendelee kuvuna busara zake sio tu katika masuala ya mpira bali maisha kwa ujumla.

Kati ya mambo mengi sana ambayo nimejifunza kutoka kwa Mzee KK ni kuwa unapoitwa na mkubwa wako wa kazi iwe ofisini au nyumbani jiandae kwa kujua saa ya kuitwa na sio saa ya kuondoka. Katika hili alinisimulia kisa kimoja wakati akiwa Meya wa Dar es Salaam. Kuna Jumapili moja Mwalimu Nyerere aliwaita viongozi wa Mkoa (akiwemo Mzee KK) nyumbani kwake Msasani saa 4 asubuhi. Ujumbe huo uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa wakati huo. Walipofika Msasani wakakuta Mwalimu ameenda kanisani. Baada ya misa Mwalimu akaenda ofisini Ikulu. Ujumbe ulisubiri Msasani kwa muda mrefu. Ilipofika saa 7 mchana Mkuu wa Mkoa akatoa rai kuwa waondoke na kama kutakuwa na taarifa yoyote watafahamishana. Mzee KK alirudi nyumbani kwake Hill Road Oyster Bay. Haikuchukua muda kapigiwa simu kuwa Mwalimu anamwita Msasani. Alipofika Msasani Mwalimu akataka kujua sababu zilizomfanya Mzee Kondo asiende nyumbani kwake saa 4 asubuhi kama alivyoagiza. Mzee Kondo akajitetea kuwa alikwenda saa 4 kama alivyoagiza na walisubiri hadi saa 7 ndipo kiongozi wa msafara wao Mkuu wa Mkoa akawaruhusu waondoke. Mwalimu akamwambia Mzee Kondo kuwa yeye aliwapa muda wa kufika Msasani saa 4 asubuhi lakini hakuwaambia muda wa kuondoka. Baada ya maneno hayo Mwalimu akamwambia kuwa ameshatengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa na kwamba yeye Mzee Kondo ana bahati kwani yeye ni diwani wa kuchaguliwa kwa hiyo hana namna ya kumfukuza kazi.

Mzee Kondo ameondoka na mambo mengi kifuani mwake. Alikuwa hazina kubwa sana kwa taifa. Mimi binafsi nimejaribu mara kadhaa kumwomba aandike historia yake lakini alikataa kabisa. Pamoja ya kuwa Mzee Kondo alinisikiliza na kukubali ushauri wangu kwenye mambo mengi, lakini hili la kuandika historia yake alikataa kabisa. Mara zote ninapokuwa namkumbusha kuhusu suala hili jibu lake lilikuwa “Bwana Dau, mie mzee, nataka nife huku nimenyooka”. Kwa bahati mbaya sana udhaifu huu wa kutoandika historia zao wanao viongozi wetu wengi. Wamebeba hazina kubwa na wakiondoka wanaondoka nazo bila kutuachia urithi huo adimu. Sisi wazee watarajiwa tusirudie makosa ya wazee wetu. Tujenge utamaduni wa kuandika ili watakaokuja baada ya sisi wanufaike na uzoefu wetu.

Yapo mengi sana ya kuandika kuhusu Mzee KK lakini nafasi hapa haitoshi. Kwa kumalizia, kwa wale wasiofahamu, Mzee KK alikuwa mpenda sana mashairi. Miongoni mwa mashairi yake aliyokuwa akiyapenda ni shairi la Muyaka bin Ghassany wa Mombasa. Alipoanza kuumwa kiasi miaka 3 iliyopita ilikuwa kila nikienda kumjulia hali huwa namsomea shairi la Muyaka. Pamoja na kutokuwa na fahamu lakini nikianza tu kumsomea shairi la Muyaka hufungua macho na kunitazama kisha akatokwa na machozi na baadae kufunga macho. Kwa kumuenzi Mzee Kitwana Kondo, nimeamua kulinukuu shairi ambalo wakati wa uhai wake, alikuwa analisoma ghibu.

Akutendeae Mema, Kushukuru ni lazima
Jaza ya mema ni mema, Maovu kutoyatia

Mbona umeghafilika? Kwa jambo lisilo shaka?
Shetani umemshika, Na kumuacha Nabia?

Unajifanya Mtesi, Kwa Mola wako Mkwasi
Unavitupa viasi, Sina la kukwambia

Silaha zote ni Zake, Wala na riziki Zake
Unakunywa maji Yake, Mbona umekosa haya?
Vita vyako fahamu, Havimdhuru Karimu
Ila wewe Bahaimu, Jijue Utaumia

Itunze yako fikara, Uwafikiri mabora
Wenye ngome na minara, Na panga za kuchinjia

Yatafakari mauti, Yeyote hayamuachi
Wala hayana wakati, Ghafla hukujilia

Yu wapi Firauni, Yu wapi Karuni
Na Shadadi maluuni, Wote wameangamia

Zao zilipokwisha, Ziraili kawafisha
Wameyawacha makasha, Na mambo haya na haya

Waimefika akhera, Madhalili mafukara
Uwapi wao bora, Wote umewakimbia

Kaburi zimewakaza, Hapana la kupumbaza
Kote kumefunga kiza, Adhabu kuwashukia

Adhabu hiyo ni kuu, Tena motoni kuwa juu
Majuto ni mjukuu, Tahadhari na dunia

Wapita na Siratini, Kuwangukia motoni
Kuteketea maini, Maisha kuteketea

Na yote ninayoyasema, Yatakufika lazima
Safari mbele na nyuma, Wengine hutangulia


Kitwana Kondo alipokuwa Meya wa Dar es Salaam
Naam ni kweli kabisa safari ni mbele na nyuma wengine hutangulia. Mzee KK ametangulia. Kwa kuondokewa na Mzee Kitwana Selemani Kondo, Dar es Salaam imepwaya sana. Jiji limegubikwa na simanzi na ukiwa na hasa ukizingatia kuwa tokea mwaka huu uanze Dar es Salaa imeondokewa na Kamanda Dr. Mohamed Awadh (Chiko), Mzee Iddi Sungura, Mzee Issa Ausi (“Smart Boy”) na hivi karibuni Ali “Bob” wa Cosmopolitan. Maskini Dar es Salaam, imeondokewa na kubaki mkiwa.

Mwenyezi Mungu Amlipe mema na azipe uzito amali za Mzee Kitwana Kondo ziwe na mizani ya juu kuliko mapungufu yoyote ya kibinaadamu ambayo alikuwa nayo. In-ShaAllah Mwenyezi Mungu Amruzuku Pepo na In-ShaAllah Atukutanishe Peponi Firdaus, Ameen.


Wednesday, 24 May 2017


Hotuba ya Mh. Kitwana Kondo (MB) aliyoitoa Bungeni Dodoma, 1999


Annur Na.187- Feb.5-11, 1999
Hotuba ya Mh. Kitwana Kondo (MB) aliyoitoa Bungeni Dodoma


Kitwana Selemani Kondo
Mh. Kitwana S. Kondo: Mheshimiwa Spika, naomba nikushuru sana.  

Mheshimiwa Spika, naomba na mimi nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake aliyoitoa tarehe 4 Novemba, 1998 hapa Bungeni. Hotuba hii Mheshimiwa Spika ina ukweli, ina usahihi na pia ina uungwana. (Makofi). 

Mimi nataka ninukuu vifungu viwili katika hotuba hii, navyo ni vifungu vya mwisho. Lakini kabla sijafanya hivyo, nataka nimwambie rafiki yangu, mpenzi wangu Dr. Msina kwa manung’uniko yake ya mambo aliyofanyiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, mimi ninazo habari na sio mimi tu, watu wengi wanazo habari kwamba Wasukuma na Mkuu wa Mkoa wa Tabora ni Msukuma na Wanyamwezi na kidogo Wadigo wana tabia ya wizi. Kwa hiyo yaliyomkuta ni mahali pake. (Kicheko/Makofi) 

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ningependa sasa niende kwenye vile vifungu nilivyosema kuwa nitavinukuu. Katika hotuba hii ya Mheshimiwa Rais, mwisho inasema hivi, "Mheshimiwa Spika, baada ya miaka mitatu ya Urais, nathubutu kubadili maneno ya msanii mashuhuri wa visiwani, Siti bint Said na kusema Tanzania ni njema atakaye na aje. Nchi yetu Mwenyezi Mungu ameibariki sana. Ni nchi ya umoja, amani, upendo, bashasha, ukarimu uliopindukia. Ni nchi ya wapenda usawa na haki. Umoja wetu wa Kitaifa unatokana na imani yetu ya dhati juu ya usawa wa binadamu mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya sheria. Umoja unaoimarishwa na sera sahihi za kujenga jamii na kuandaa mazingira ya maendeleo ya haki, amani na utulivu kwa wote". (Makofi) 

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, Mheshimiwa Rais anaendelea. Anasema hivi, "Umoja unaotahadhari sera, kauli, tabia na vitendo vinavyoweza kupanda mbegu za mfarakano, chuki na kutoaminiana miongoni mwa Watanzania". Ningependa niyarudie maneno haya. "Umoja unaotahadhari sera, kauli, tabia na vitendo vinavyoweza kupanda mbegu za mfarakano, chuki na kutoaminiana miongoni mwa Watanzania. Umoja unaolindwa kwa vita vya kudumu dhidi ya ukabila, udini, ubaguzi wa rangi, jinsia au majimbo". 

Mheshimiwa Spika, miaka mingi iliyopita, kwenye 1658 A.D. Mtu mmoja Galileo alisema, "Dunia ni mviringo". Makuhani wakamwambia huyu anakufuru, akashitakiwa akahukumiwa kuuawa na akachomwa moto. Leo Galileo amekuwa Vindicated. Kwa bahati mbaya Galileo mwenyewe hayupo kujua kwamba amepata Vindication. (Makofi) 

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema ni hiki cha umoja unaotadhari sera, kauli, tabia na vitendo vinavyoweza kupanda mbegu za mfarakano. Nimesema mara nyingi hapa kwako. Mheshimiwa Rais, hivi karibuni aliwahutubia Waislamu kwenye Baraza la Idd, akawaambia kwamba manung’uniko yao na malalamiko yao yote atayatazama na atayashughulikia akishirikiana na Baraza lake la Mawaziri. 

Sasa nina mambo mawili au matatu ambayo nataka kuyasema ambayo yanaweza kuleta mfarakano. Yanapandwa na serikali. Moja, karibuni hivi katika mwezi wa Ramadhani, mwezi wa Ramadhani kwa Waislamu ni mwezi Mtukufu, ni mwezi wa toba. 

Wale jamaa zangu wasiojua toba ni mwezi wa kurudi kwa Mungu. Wakati wa ukoloni na mimi nilisoma wakati wa Ukoloni mwezi wa Ramadhani shughuli zote zinafungwa, baadaye kwenye serikali yetu wenyewe shule hazifungwi. Lakini baada ya muda wanaachiwa watoto kurudi majumbani kwao au kwenda kwenye mabweni. Lakini mwaka jana na mwaka huu serikali ikaamua kuwa mitihani ya watoto wa kidato cha nne ifanywe mwezi wa Ramadhani na iendelee mpaka siku za Idd. Hiyo ni moja ya cheche za mifarakano. 

Kwa Rehema ya Mungu Alhamdulillah, baada ya kunung’unika Waislamu, Waziri wa Elimu na Utamaduni alitoa maelezo. Maelezo yale yakawaridhisha Waislamu na Mheshimiwa Rais akakubali kwa siku za Iddi, watoto wasifanye mitihani na haikufanywa mitihani. (Makofi) 

Lakini mimi ninalouliza ile sababu ya kuamua mwezi wa Ramadhani ifanywe mitihani ni nini? Ni Insensitivity, ni jeuri, ni kiburi, kwa sababu kuna wengine ambao ni wazito tuliwasikia wakisema, wakitaka kufanya mtihani na wafanye hawataki basi. Mimi nasema watu kama hao ndiyo watu wasioitakia kheri nchi hii. Siyo sisi tunakuja kusema hapa hadharani. Hao wanaosema wakitaka kufanya na wafanye na hawataki kufanya basi. Hao ndio wasioitakia kheri nchi hii. (Makofi) 

La pili, linaloweza kuleta mfarakano ni tabia ya serikali ya kuchelewesha makusudi kuandikisha taasisi za Kiislamu. Taasisi yoyote ya Kiislamu ikitaka kuandikishwa serikalini itachukua miaka miwili au mitatu. Sababu hazitolewi, hata kama kuna uchunguzi, watu waende wakatafute habari kwa nini inachukua miaka miwili, miaka mitatu? 

Mheshimiwa Spika, nilipata kusema hapa kwamba mimi ni mlezi wa Baraza la Maimamu Tanzania. Tumeomba Baraza la Maimamu kuandikishwa, sasa ni miaka mitatu, sababu haijulikani. Wengine kila wakiomba wanasema lazima kipatikane kibali toka BAKWATA. Leo ningependa nijue ipo sheria inayosema hivyo? Au ni matakwa tu ya wakubwa? Hilo la pili. (Makofi) 

Mheshimiwa Spika, la tatu, Sura ya 33 Aya ya 30 na ya 31 ya Qur’an inamtaka mwanamke akifika umri wa miaka 9 avae hijabu. Hijab maana yake avae nguo ya mikono mirefu, avae shungi, avae gwanda zuri na avae suruali inayoficha mapaja na mpaka magoti. Mimi najua ya kwamba serikali imetoa agizo kwa watoto wa shule kwamba wafanyiwe hivyo wale wa Kiislamu wanaotaka, sheria zote zinavunjwa. Dini ya Kiislamu inakataza pombe, Waislamu wanakunywa pombe. Sasa hilo anafanya mwenyewe. 

Lakini ninajua pia ya kwamba kuna shule nchini huku, kuna viongozi wa Idara ya elimu ambao wanakataa kutekeleza sheria hii au agizo hili na serikali imekaa kimya, nataka nijue ni kwa sababu gani? Tujue ni kwa nini. Hii ni amri ya Mwenyezi Mungu na serikali, Rais anasema tusifanye chochote kinachoweza kuleta mifarakano. 

Mheshimiwa Spika, lingine ni kwamba huu mwaka wa 30 wa uhuru. Siku ya Ijumaa ni siku muhimu kwa Waislamu kama ilivyo kwa siku ya Jumamosi ni siku muhimu kwa Wasabato kama ilivyokuwa siku ya Jumapili ni siku muhimu kwa Wakristo wengine. Lakini siku ya Ijumaa ingawa kuna agizo la serikali kwamba Waislamu waachiwe waende wakasali. Kuna viongozi siku ile ndiyo siku ya kufanya Board Meeting, ili kumzuia Mkurugenzi ambaye ni Muislamu ambaye anapenda kazi yake aogope. Shule zinafungwa saa 7. Jumapili vitoto vidogo vidogo vya Kikristo vinakwenda kusali. Jumamosi vitoto vidogo vidogo vya Kikristo vinakwenda kusali. Siku hizi vitoto vidogo vidogo vya Kiislamu vinataka kwenda na wazazi wao. Naomba utaratibu ufanywe wa dhamiri kabisa kwamba Ijumaa saa 6 kazi basi kwa Waislamu. Wale wanaofanya Board Meeting waache wafanye saa 8, wafanye saa 9 na shule zote za Primary na Secondary zifungwe saa 6 ili kuwapa nafasi watoto wa Kiislamu waende wakasali. 

Mheshimiwa Spika, nina mengi lakini nitakuambia mwisho. La mwisho, Rais aliwaambia Waislamu wote pale Dar es Salaam kwamba atalishughulikia suala la elimu. Lakini akawashauri kwamba wale wafadhili ambao hivi sasa wanatujengea Misikiti wajenge pia shule. Hilo jambo zuri, na Waislamu wamelisikia na ninajua ya kwamba Waislamu wanataka hivi karibuni kumwendea Rais kwenda kumshukuru. Ila nina jambo moja, natoa mfano wa Dar es Salaam, Waislamu wanafikia asilimia 70 au zaidi. Kwenye magereza Dar es Salaam wengi kuliko Wakristo au watu wengine. Hawa wengi, hawana kazi, jela watakuwa wengi. (Kicheko) 

Lakini tuende kielimu. Ninayo ripoti ya mwaka huu. Waliofanya mtihani wa darasa la saba kuingia darasa la tisa, asilimia 71 Waislamu. Asilimia 29 ni wengine. Walioshinda katika wale asilimia 71 ni asilimia 21. Katika wale 29 walioshinda tena sema mwenyewe. Katika asilimia 29 waliokwenda shuleni ni asilimia 79. Katika asilimia 71 waliokwenda darasa la tisa ni asilimia 21. 

Sasa kuna moja, ama Waislamu wajinga ama akili yao haifanyi kazi, ama mtu ukiwa Muislamu wewe huna kitu, ama kuna kitu. Sasa namwomba Waziri anayehusika, anaposema aseme ya kwamba kwa hali ilivyo Waislamu wameumbwa wajinga. Au kwa hali ilivyo kuna sababu kadha, kadha. Mwalimu Nyerere alisema zamani ifanywe bidii ya kuwanyanyua waliokuwa chini. Sasa bidii hii siyo ya kuwanyanyua waliokuwa chini. Bidii hii ni ya kuwakandamiza waliokuwa chini. 

Mheshimiwa Spika, Rais Mkapa anawasaidia Waislamu. Tulimwendea, mimi mmojawapo kwa mambo mengi ambayo ameyashughulikia. Nina hakika ya kwamba mambo haya tuliyoyasema na aliyoambiwa na viongozi wa Kiislamu kule bungeni atayashughulikia. Lakini ninaamini kabisa ya kwamba hataweza peke yake bila ya msaada wa viongozi wangu hao walioko hapa. Wakisema hawa kwamba ndiyo kawaida yao hiyo. Atapata tabu Rais wangu. 

Mheshimiwa Spika, kengele ya pili imelia. Nashukuru sana. Lakini nataka niseme kwamba haya niliyoyasema, nasema kwa sababu najua mimi kwamba suala hili la mfarakano ni suala kubwa. Penye mfarakano hakuna maendeleo. Penye mfarakano hakuna cha uchumi. Kwenye mfarakano kuna ghasia. Kwa kuwa Rais ameomba tufanye kila jambo mfarakano usiwepo, basi serikali imsaidie Rais katika kutekeleza wajibu wake kwa makundi yote ili pawepo na usawa. (Makofi)  


Kitwana Selemani Kondo akifanya kipindi cha televisheni (TV Imaan) ''Walioacha Alama Katika Historia,''
nyumbani kwake Upanga tarehe 12 Septemba, 2012 akihojiwa na Mohamed Said