Showing posts with label historia. Show all posts
Showing posts with label historia. Show all posts

Wednesday, 14 February 2018

Dedan Kimathi
''Minong’ono ilikuwa ikisikika kutoka kanda ya ziwa kuwa kiongozi wa wapiganaji wa Mau Mau, Dedan Kimathi alikuwa anaonekana mjini Mwanza. Wakati ule pale Mwanza kulikuwa na Wakikuyu wengi wakifanya biashara sokoni. Ilivumishwa kuwa Dedan Kimathi alikuwa akiwasiliana na Wakikuyu wenzake na wao walikuwa wakimkusanyia fremu za baiskeli za zamani ili zitumike kutengenezea magobole ili zitumiwe misituni dhidi ya majeshi ya Waingereza. 

Mapigano yalipoonza kati ya Mau Mau na Waingereza kulikuwa na Wakikuyu kama elfu kumi na sita wakiishi na kufanya kazi kaskazini ya Tanganyika. Kama tahadhari, Wakikuyu wachache walioonekana kuunga mkono Mau Mau, walikamatwa na kupelekwa Kenya ambako waliwekwa kizuizini katika kambi mbali mbali. Wakati Budohi na Wakenya wengine walipopita Korogwe wakati wakirudishwa Kenya kupitia Taveta, Ally Sykes, ambaye alikuwa amehamishiwa Korogwe, alikwenda hadi stesheni ya reli kuwaaga. Watuhumiwa hawa wa Mau Mau walikuwa wametiwa katika mabehewa ya kubebea ng'ombe huku wamefungwa minyororo. Dome Budohi na wazalendo wengine waliwekwa kizuizini kwa miaka saba. 

Dome Okochi Budohi TANU kadi no. 6

Kulikuwepo na wazalendo kutoka nchi jirani ya Kenya kama vile Dome Okochi Budohi na Patrick Aoko ambao walikuwa wanajua vyema siasa za walowezi za kupora ardhi za  wananchi. Kutoka kwa wazalendo kama hawa, Abdulwahid alipata usikivu wa mawazo yake ya kuigeuza TAA kuwa chama cha siasa chenye nguvu. Lakini mara tu baada ya kuundwa kwa TANU wazalendo hawa wa Kenya wakakamatwa na serikali. Kwa miezi sita walihojiwa na kuwekwa rumande Central Police Station huku wamefungwa minyororo. Budohi na Aoko walikuwa wakifuatwa na makachero (Special Branch) toka mwaka wa 1952 baada ya hali ya hatari kutangazwa Kenya. Inasemekana Dome Budohi aliponzwa na barua iliyotoka Kenya ambayo ilikamatwa na makachero. Barua hii ilikuwa inamuhusisha Budohi na Mau Mau. Inasemekana Budohi alisalitiwa na Mkenya mwenzake aliyeitwa Martin ambaye alikuwa pamoja naye katika Blackbirds. Martin alikuwa akipuliza tarumbeta.

Askari waliokuwa wakiwalinda kule rumande walitoa habari kwa TANU kuwa kulikuwa na mpango wa kuwapa sumu wafungwa wale, Budohi na mwenzake Aoko. Baadaye wafungwa hawa walihamishiwa Handeni ambako kulikuwa na kambi ya kuwafunga watuhumiwa wa Mau Mau. Kawawa alikuwa amehamishiwa hapo kutoka Dar es Salaam. Baadhi ya wafungwa walikuwa wananachama wa TAA na baada ya kuundwa TANU wakawa wanachama wa TANU. Kawawa alikuwa akifahamiana na wengi kati ya wafungwa wale. Budohi na Aoko waliwahi kuwa  viongozi wa TAA. Kawawa aliwaangalia wafungwa hawa kwa moyo wa huruma akijaribu kupunguza shida zao pale kambini kila alipopata mwanya wa kufanya hivyo.''


***


''Mara tu baada ya kuundwa kwa chama cha TANU Wakenya walikamatwa na kurudishwa Kenya ambako waliwekwa kizuizini Manyani na katika kisiwa cha Lamu. Wazalendo wa Kenya waliokuwa katika harakati nchini Tanganyika hawakuwa na uhusiano na TANU baada ya uhuru na wala chama hakikufanya juhudi kuwasiliana nao. Dome Budohi alijaribu mara nyingi kuomba kukutana na Nyerere alipozuru Nairobi lakini ilishindikana. Budohi hafahamu kama maafisa wa serikali ya Tanzania walimzuia wao tu au walifanya hivyo kwa amri ya Nyerere. Hadi anafariki Dome Budohi hakuwahi kuonana na Nyerere ambae wakati wa enzi za TAA na TANU walikuwa wakifahamiana vizuri.''
(Kutoka kitabu cha Abdul Sykes)


Tuesday, 13 February 2018


Masheikhe wetu: Sayyid Omar Abdalla (Mwinyi Baraka)
Sehemu ya (3)
Na Ben Rijal


Mwinyi Baraka

Makala haya nitamalizia juu ya kusoma kwake, kufanya kazi kwake na misukosuko ya hapa na yapale aliokumbana nayo. Tunaona katika nyakati mbalimbali wasomi wa Kiislamu hupata misukosuko ya kila aina hasa kwa kufanyiwa fitna na wengi wao humalizikia kuwekwa korokoroni na kuonekana kama ndio shahada ya kuwa mlinganiaji wa dini ya Kiislamu. Wengi wao huwekwa korokoroni na Waislamu wenzao. Kuna maandiko yanaonyesha kuwa Sayyid Omar Abdalla kafungwa mara mbili kwa misimamo yake, lakini unapopitia kumbukumbu mbalimbali na kufanya mahojiano na mtu ambaye alibahatika kuwa naye Zanzibar, Uiengereza na kufungwa pamoja naye anathibitisha kuwa kafungwa mara mmoja tu.

          Katika makala iliopita nilijaribu kuonyesha kusoma kwake na tumeona kuwa Sayyid Omar Abdalla kwanza alikwenda kusoma Chuo cha SOAS na kupata shahada ya Diploma ambayo ndio aliokuja nayo na kuwa sasa kishakuwa msomi anayotakiwa kuwa anaongoza Chuo cha Kiislamu “Muslim Academy” ingawa mwenyewe alikuwa akiona kuwepo na pengo na kuwa hajaaelimika atakavyo.
          Bada ya kurudi masomoni na kuwa anashirikiana na watawala katika kuweza kukiendeleza Chuo cha Muslim Academy, Sayyid Omar alihudhuria mikutano mingi na hata ikajiri afike Nigeria kwenda kuweza kuangalia namna wao wanavyoendesha masomo ya Kiislamu katika nchi ambayo Kiengereza kinatawala na kipo juu.
          Unapopitia nyaraka mbalimbali saa nyengine unahangaishwa kufahamu mtawala Muiengereza katika utawala wake namna ambavyo alivokuwa anaziangalia dini kuu mbili na kuhakikisha kuwa hazipishani na wakati huo huo anakuja na upendeleo kwa upande mmoja halafu upendeleo huo unakuja unafichwa na kuonyeshwa juhudi za kuwaweka waumini wa dini kuu mbili Afrika ukiwa Uislamu na Ukiristo kuwa upo sawa.
          Muiengereza alikuwa amejaribu katika nchi ya India, Sudan na Nigeria kuweka mtaala wa elimu ya dini ya Kiislamu ambao unafahamika na utaweza kutumika unavyostahiki, aidha alifanya katika nchi hizo kuwa na Makadhi pamoja na Mahakama zake ambazo Waislamu hawatakuwa na shida na ili kuweza kuyatolea ithibati hayo, utayaona katika kumbukumbu za kuanzishwa kwa Muslim School mkolini alijaribu kukaa na viongozi mbalimbali wa dini na wasomi wa kuiweka Ofisi ya Kadhi na Mahkama yake, na akahakikisha kuwa wale wasomi wanaofahamika na wenye ujuzi ndio wakupewa nafasi ya kuongoza kuanzia Kadhi na watendaji wake.
          India na Sudan walifanya vizuri sana katika kujipanga kwa mitala ya dini ya Kiislamu,  utaona hadi leo Sudan wana taratibu nzuri ya kuwanisha baina ya uongozi wa dunia na akhera.
          Sayyid Omar bin Abdalla alipata fursa yakwenda Nigeria na alivutiwa kuona mpangilio wa mitala ya Madrasa namna ilivyopangiliwa namna walimu walivyofunzwa namna ya kumsomesha mtoto kujua kusoma Qur’an na Sheria na hapo hapo kufunzwa msingi wa mwanzo wa lugha ya kiarabu, kujua vitu mbalimbali vinaitwaje kwa Kiarabu hasa vile vilivyomzunguka, haya yalimvutia sana Sayyid Omar Abdalla na safari yake hio ya Nigeria ilikuwa akipenda kuielezea katika mihadhara yake na kuanza kuandaa mipango ya utekelezaji kwa Zanzibar na Afrika ya Mashariki kwa jumla.
          Sayyid Omar aliporudi Ulaya akawa anasoemsha dini katika Skuli ya Teacher Training na akaja kuwa mwalimu Mkuu wa Skuli ya Muslim Academy kwa hakika alikuwa anaposemesha dini mara zote akipenda kuingiza na taaluma yake alioipata Chuo cha Makerere College ikiwa elimu ya viumbe (Biology).
          Ilipofika mwanzo wa miaka ya 60 Sayyid Omar Abdalla alifanikiwa kupata Scholarship nyengine kwenda Uiengereza. Wakati huo akiwa Muiengereza akijua makoloni yanamtoka lakini alianza kujisafisha na kuweka nidhamu ambayo kila mwaka akijaribu kuhakikisha wanafunzi wangapi wanakwenda nje kusoma masomo ya juu na Zanzibar kwa wakati wake ikiwa na idadi ya watu 300,000 ukichukua na asilimia na uwastani wake ilikuwa na wanafunzi wasiopungua 400 wakiwa wapo nchi za kigeni wanasoma, wengi wao walikuwepo Misri kwa program ya Gamal Abdulnasir na wengine wakiwepo Uiengereza, Iraq, Marekani, India na kwengineko.
          Sayyid Omar Abdalla alijiunga na Chuo Kikuu cha Oriel College, Oxford na safari hii akafanya shahada ya Masters ambayo somo lake lilikuwa juu ya Falsafa na hapa ndipo mkanganyiko nitajaribu kuweka sawa na haya ninayosema nasema kwa kupitia Faili lake na mazungumzo nna  murid wake Sheikh Ahmed ambaye kawa naye hapa Zanzibar kama katika wanaohudhuria mihadahara yake na kuwa naye kwenye rubaa za kheri na wakawa pamoja Uiengereza na wakafungwa jela pamoja.
          Katika Chuo cha Oxford Sayyid Omar Abdalla alisoma somo la Falsafa (Philosophy) alipokuwa anajifunza somo hili alionyesha maajabu mengi namna alivyokuwa akiweza kuona wana Falsafa watangulizi wa Kiyunani kina Aristotle na wengineo walivyokuja kuwa athiri wasomi wa Kiislamu kama Ibn Sinna (Avicenna) na kuweza kuwafahamu wana falsafa wa Kiislamu ambao wengine hata roho walikua wakielezea katika kitu chengine ambacho kitabaki na kuondoka na kurejea kwa njia nyengine.
          Sayyid Omar alivutiwa na Mwanafalsafa Ibn Bajja na Imam Ghazali na unaposoma Risala yake ya mwisho Chuwomi Oxford (Thesis) alioipa jina “Some Felicity in Medieval, Islamic Philosophy” ndio utapofahamu kwanini alishikana na Ibn Bajja akawa tafauti na Ibn Rushd, hawa kina Ibn Rushd na Ibn Sinna waliuweka pembeni Uungu na wakenda katika nadharia ambayo mwanadamu ameiasisi.
          Sayyid Omar alivutiwa zaidi na Imam Ghazali ambaye akiweza yeye kumfahamu zaidi, Imam Ghazali alianza kuzama na nadharia za kina Aristotle, kisha akazama kuona Uungu na umoja yaani sii umoja huu lakini upweke wa Allah kuwa hakuna mwengine wa kuabudiwa ila ni yeye tu katika mamlaka yake na uongozi wake.
          Leo katika elimu ya Ikolojia (Ecology) kunazungumzwa juu ya mwindaji na  mwindwaji na haya Imam Ghazali katika kitabu chake cha Ihya Ulumu Deen anagusia na utafahamu utapomsikia Sayyid Omar Abdalla alivomfahamu Imam Ghazali, naye kuwa na uelewa wa somo la ilimu ya viumbe.
          Imam Ghazali akifahamisha namna ya ndege Allah alivyomjaalia kuwa kila saa awe anakula kisha anakitoa chakula kama kinyesi, anakula tena na kurudia kula, Imam Ghazali anaeleza kuwa kuumbwa kwa ndege kuwa na umbo dogo w ni kwasababu awe yupo natunaendelea kuwaona kwa dahar, lakini kuweza kubakia kwake ndege kuepukana na maadui awe kila akila akikaa awe hashibi bada ya muda mdogo anataka kula tena na hio inamfanya kuwa kwa udogo wake angekuwa anakula na kushiba basi maadui wake kina nyoka na wengine wangewamaliza kirahisi, hapa ndipo kunakazi kufahamu na inataka malinganisho ya ilimu ya dunia na akhera.
          Katika somo la Ikolojia  haya maingiliaano wanayaita “Predator prey relation) na Sayyid Omar Abdalla nilimsikia anamuelezea Imam Ghazali kwa wigo wa Ikolojia na namna wanyama wanavyopotea kutoonekana tena (Extinct) ni namna Allah alivyopanga vipi viumbe viweze kupambana na wengine na kujihami na kuendelea kukuwepo, Falsafa ya Imam Ghazali ilimvaa vya kutosha na Sayyid Omar Abdalla alifika hadi hawezi kutoa mhadhara bada ya kutoa aya chache na kuja na hadithi za Mtume Muhammad (SAW) asimgusie Imam Ghazali.           Bahati nzuri hii risala yake ya Oxford imechapishwa na vyema ukaipata ukaisoma.
          Sayyid Omar Abdalla alirejea Zanzibar mwaka wa 1963 bada ya kumaliza masomo yake hapo Oxford na alifika kuwa na kasi kubwa ya kutoa mihadhara na akipata nafasi iwe kwenye hitima, majlisi, radio au popote pale akichukua nafasi hio kuweza kutoa mawaidha mazito ambayo ni zaidi yalikuwa ulinganisho wa dini ya Kiislamu na Kikiristo.
          Yalipotokea Mapinduzi ya 1964 alikuwa ni mwalimu bado hakuyapa kisogo aliendelea kufanya kazi na kwenda sambamba na mabadiliko yaliotokea, ithibati ya hio ni hio picha ya ujenzi wa uwanja wa Amani, akiwa yumo katika ujenzi wa taifa na huku ana shoka anachanja mnazi.
Sayyid Omar Abdalla na Maalim Zubeir Rijal katika ujenzi wa taifa
          Matokeo machache juu ya Sheikhe huyu: Sayyid Omar Abdalla ilikuwa kila siku ya Ijumaa akipenda kuwa na rubaa na wenzake ya kumuomba Mungu katika zile taratibu ambazo Mola anasema “Niombeni nikujibuni” yeye na wenzake  waliweka taratibu ya kuleta maombi au tuite Nyiradi siku za Alkhamisi na Ijumaa, katika mwaka wa 1968 alikamatwa na wenzake kama 25 kwa kuambiwa wanapanga njama ya kupindua Serikali, akawekwa korokoroni kwa mwezi mmoja badaye ilikuja  kuelekweka kuwa ilikuwa ni fitna tu, tena hapo Mzee Abeid Amani Karume akaamua kuwachia, afya yake iliathirika sana kwani akisumbuliwa na kisukari na akawa hapati dawa ya kupiga shindano ya Insulin. Sayyid Omar bada ya kutolewa jela alikuwa akiishi na khofu akaona asije akafungwa tena akaamua kuhama Zanzibar huku  tayari kapatiwa nafasi ya kurudi Uiengereza lakini aliona vyema kwenda kusihi katika visiwa vya Comoro ambavyo ana nasaba navyo.
          Safari mmoja akiwa anasafiri kutokea Kenya anaelekea Ulaya, amesimama kwenye foleni, binti wa Kikenya alio katika kupima mizizigo na kutoa namba ya viti kwenye ndege kumuona mzee na majuba na kashika bakora akamshika kumwambia “eeh muzee nenda kwenye foleni ile ya kwenu Mombasa, ndege itakukimbia.” Sayyid Omar alikaa kimya lakini jeuri ya kitoto ikazidi kwa kumtaka mmoja ya wafanyakazi kumtoa kwenye Foleni, Sayyid Omar akatoa Pasi ya kusafiria ikiwa na hadhi ya kidiplomasia na mrundo wa tiketi, mpaka akaiona tiketi yake anayokwenda Ulaya, aliyotumwa akamjibu yupo pahali sawa, binti akasema haiwezi kuwa, akawa anajipanga sasa kwenda kumtoanyeye mwenyewe kilichomudhi hakifahamiki, lakawa anamuhudumia msafiri wa Kifaransa ambaye hajui Kiengereza, ikawa vuta ni kuvute na wakati unakwenda Sayyid Omar akamsogelea yule bibi wa Kifaransa na kumuamikia kwa Kifaransa na kutaka kujua nini shida yake, akawa Sayyid Omar sasa anatafsiri kutoka Kifaransa anapeleka kwa Kiengereza kwa mratibu wa Tiketi, binti wa Kikenya hakuamini, alivyoyasuluhisha binti akataka kujua wapi aliposoma kujua Kiengereza na Kifaransa, Sayyid Omar Abdalla akamwambia “You better asked Kibaki, he knows me better, we were together at Makerere College” Binti wa Kikenya  alitahayari bali aliogopa asije kushtakiwan kwa wakubwa wake na Sayyid Omar alipomuona anatetemeka huku hana raha akamwabia “Jitahidi kuwaona watu wote ni sawa.”
          Alifika Chuo Kikuu cha DaresSalaam akatoa uwaidh juu ya umuhimu wa kujiendeleza kiroho kwa kuwa na dini, wakati wa masuala kijana akaona aaah, huyu mzee ndio watu wa kizamani Wakoloni waliwafundisha lugha ndio katuhutubia kwa Kiengereza, akamvaa akamwambia unajua nini Karl Marx kasema? “Religion is the opium of the mass” kwa maana ya kuwa “Dini ni kasumba kwa umma.” Sayyid Omar Abdalla kwa mshangao wa wengi aliusoma ukurasa mzima wa Das Capital juu ya maneno hayo na kusema ukurasa gani upo wenye manerno hayo ambayo aliyasoma  kwa ghibu, na akamtaka kijana huyo amsome Maurice Bucaile katika kitabu “What is the Origin of man na The Qur’an, The Science and the Bible.” Kijana badala ya kutaka kumshushua Sheikhe alijikuta kajishusha hadhi na kujuta aliyotaka kuyafanya.
          Sayyid Omar Abdalla akipenda kuurejea na kurejea msemo wa mwana sayansi wa Fizikia maarufu kwa jina la Albert Einstein usemayo “Science without religion is lame, religion without science is blind.” Somo la sayansi pasi kujuwa dini ni sawa na kilema na sayansi pasi kujuwa dini ni mithili ya kipofu.” Sheikhe huyu alikuwa na elimu zote mbili hizo na akiweza kufahamisha na kutowa ujumbe kwa watu wa rika zote wakiwa wasomi na wale wasiokuwa wasomi.
          Yapo mengi ambayo ningeweza kumzungumza Sheikhe huyu, nategemea haya machache yanatosha, fatwana na mie wiki ijayo umjua Sheikh Abubakar Bakathir. Tumuombe Allah nasi tufwate nyayo za Sayyid Omar Abdalla (Mwinyi Baraka), Ameen.


Sunday, 11 February 2018


Masheikhe wetu: Sayyid Omar Abdalla (Mwinyi Baraka)
Sehemu ya (2)
Na Ben Rijal
Katika makala haya ya leo yatamuangalia Sayyid Omar Abdalla katika kuendelea kusoma na kazi alizozifanya alipokuwa bado yupo Zanzibar, sio kitu cha kawaida katika Wasomi wengi wa Kiislamu kwenda nazo sambamba elimu ya dunia na elimu ya dini. Sayyid Omar Abdalla alielimika na elimu zote mbili hizo aidha alikuwa akijisomea vitabu mbalimbali na majarida katika kuendeleza uwezo wake kielimu.

            Katika makala ya wiki iliopita nilianza kwa kunukuu misitari miwili mitatu ya Kiengereza kwa yule aliojuwana na Sayyid Omar Abdalla na leo aidha nitaanza hivyo hivyo na mistari miwili mitatu alioyaandika yeye mwenye Sayyid Omar Abdalla.
            Dear Mr. Harvey, I have just received your circular in connection with Religious Teaching in School. Thank you very much. During the last vacation I resumed my discussion with the Chief Kadhi and at the end we arrived to a definite conclusion which I am sure you would like to hear. Since the beginning of the term I have been trying to come and see you at your office but in vain, as I am very busy throughout the week including Saturday. Could you kindly therefore fix me up on any one convenient Sunday so that I might come to see you in your home? Your sincerely, Omar Abdalla (Kumbukumbu  ZNA AD 3/8). Tafsiri ya juu juu kutokana na Faili lake lenye nambari ZNA 3/8  akimuandikia Mkurugenzi wa elimu Mr. Harvey akimwambia, “Nashukuu  kuwa nimepata chapisho ulionitumia kuhusu usomeshwaji wa masomo ya dini katika maskuli. Katika mapumziko yangu bada ya mhula wa masomo  nilishafanya mazungumzo juu ya masaala hayo na Kadhi Mkuu ambaye tulifikia makubaliano,  imani yangu kuwa wewe Mkurugenzi wa Elimu utapenda kusikia juu ya mazungumzo hayo. Nilijitahidi kupiga hodi kwenye ofisi yako pasi mafanikio, ikiwa na mie nimebanwa na mashughuli kwa wiki nzima pamoja na Ijumamosi yake, nitaomba uitenge siku ya Ijumapili tuweze kuonana.  Wako mtiifu. Omar Abdalla.”
            Nitapenda kugusia jambo mmoja muhimu sana ambalo katika utawala wa Muiengereza uliweza kusaidia sana katika uwekaji wa kumbukumbu. Ilikuwa Maofisa wote wa Serikali wakitakiwa taarifa zao kuhifadhiwa katika mafaili maalumu kisha kuwekwa kwenye ofisi ya nyaraka (Archives).
            Ilikuwa ofisa yoyote akipandishwa cheo, akiongezwa mshahara, akipata uhamisho barua atakayopewa lazima ikawekwe kwenye faili lake huko ofisi ya nyaraka na mpelekaji wa taarifa hizo ni tarishi ambaye kila mtu akimjua kama ni tarishi au kwajina hilo la zama hizo akiitwa Ofisi boi, kwani akivaa shati na surula ya khaki na baskeli yake nyekundu.
            Ofisi boi akijivunia kazi hio kwani ilikuwa siku hizo ukiwa mfanya kazi wa Serikali basi maisha yako utayaweza kutokana na mshahara unaolipwa. Taarifa nyingi za waliopita tunaweza kuzipata kwa njia hio ambazo kwa leo ni kitu kigumu kuweza kuzipata taarifa za wafanya kazi mbalimbali.
            Aidha katika sehemu hio ya kumbukumbu utaweza kupata taarifa za kila aina, hata zile za magazeti yaliopita ambayo kila nakala iliokuwa ikitolewa hupelekwa hapo na kuwekwa.
Sayyid Omar Abdalla akiwa na Masheikhe na walimu mbalimbali hapo Ukutani
            Sayyid Omar Abdalla akiwa amerudi kusoma Makerere College huku anasomesha, alikuwa ansubiri nafasi ya kwenda kuongeza masomo kwa hamu huko nchi za nje, kama nilivyokwisha kueleza kabla  kuwa Sayyid Omar alikuwa kati ya wanafunzi wa mwanzo kusoma masomo ya Sekondari viiswani Zanzibar aidha alikuwa kati ya wanafunzi wa mwanzo wa kwenda kusoma masomo ya juu katika Chuo cha Makerere.
            Ilipofika mwaka wa 1951 Sayyid Omar Abdalla na Abdalla Jahadhmi walikuwa wanafunzi wawili waliopata fursa ya kwenda Uiengereza kwa masomo ya juu. Sayyid Omar Abdalla alikwenda chuo cha SOAS kufanya masomo ya Ulinganisho wa dini pamoja na Kiarabu.
            Kuna mapendekezo mengi ambayo watawala wa Kiengereza walikuwa wakijadiliana katika uongozi wa elimu pamoja na mahusiano ya mambo ya nje juu ya kumsomesha Sayyid Omar Abdalla ili aweze kuja kuwa Mwalimu Mkuu wa Chuo cha Kiislamu ambacho kilikuwa katika katika mataarisho ya kufunguliwa mwisho wa miaka ya 40.
            Sayyid Omar Abdalla alikuwa akitamani kwenda kusoma nchi za Kiarabu lakini fursa ilipomuangukia ya kusoma Uiengereza kufanya masomo ya Ulinganisho wa dini ngazi ya Shahada ya Diploma hakusita akakubali, huku akijuwa kuwa atakuwa na pengo katika kuzungumza Kiarabu, ingawa akizungumza Kiarabu lakini sivyo namna alivyokuwa akitamani mwenyewe kukimudu hicho Kiarabu. Wengi wa watu wa visiwani siku hizo katika maisha yao ya kujifunza Msikitini tangu utotoni hadi utuzimani mwao walikuwa wakizungumza Kiarabu lakini wenyewe wakikiita Kiarabu cha Msikitini.
Ahlil Darsa wa Msikiti wa Ijumaa mdogo
            Alipokuwa anafanya masomo yake hayo hapo Uiengereza alipewa magwiji wawili ambao kazi yao ilikuwa kuhakikisha analifikia lengo lilokusudiwa, akisimamiwa na mjuzi wa elimu ya Ulinganisho wa dini David Cowan (al Dundawi) na R. B. Serjeant inagawa msimamizi mwengine alimkataa kumsimamia na kujiunga na chuo hicho alikuwa  ni J.N.D Anderson.
            Akiwa anasoma huko Uingereza alikuwa akiwasiliana na wanafunzi wa maeneo mbalimbali kuweza kupata kwenda kujiendeleza bada ya kukamilsiha masomo yake na khasa alilenga kuweza kupata fursa ya kwenda kujiendeleza katika nchi za Kiarabu na za Kiislamu.
            Ilipofika mwaka wa 1953 akiwa bado yupo Uiengereza alifanya safari ya kwenda Marekani na kuhudhuria mafunzo ya nyakati za kiangazi, masomo ya muda mfupi, huku akiwa amefanya aridhilhali ya kupata kwenda kusoma masomo ya Kiarabu.
            Hakuchoka kuandika na kuwataka Waiengereza wamlipie masomo yake katika nchi za Kiarabu kitu ambacho katika siku zake za utuzimani bada ya kuondoka Zanzibar hakuwa ni mtu wa kushikilia jambo analolitaka ila akipenda kuona ajiachie na aone upepo utavyomchukua utakavyo.


Sayyid Umar bin Sumayt na Sayyid Omar Abdalla
             Akiwa bado yupo huko Uiengereza na kiu chake kutaka kujiendeleza masomo yake katika nchi za Kiarabu, hakuona tabu kukamata kalamu na kuandikia Wizara ya elimu, aliandika lugha nzito yenye ufasaha na unapoisoma barua hii utaona namna alivyokuwa akikimudu Kiengereza.
            “Sir, you may be pleased to hear that I have done well in my examination, and next year I hope to complete my course. I must thank the government for affording me the unique opportunity, being the first and the only student in the course. I am becoming a learned man. But you will agree that however high the standard   of knowledge I get here, I shall not be really competent to hold any post involving the use of Arabic or Islamic law unless I spend some time in a country where Arabic is the language, and where Islam form the background of the people. Here, there is no proper atmosphere. My stay in Arabia will be a shield against those who criticize my coming to London. It will give me a greater confidence, and I confess that I shall not completely qualified for a responsible position without actual living in Arabia” (kumbukumbu ANA AB 86/47, barua alioiandika tarehe 30.6.1953)
            Kwa kifupi aliandika barua kusema kuwa amemaliza masomo yake na amefanya vizuri ni vyema sasa wakampatia fursa ya kwenda kuongeza msomo yake katika nchi za Kiarabu, kufanya hivyo kutawafunga midomo wale watakao bwabwaja kuwa elimu yake kaipata Ulaya, ila tu kukosa kwenda kufanya mafunzo katika nchi za Kiarabu zenye utamaduni wa Kiislamu basi hatokuwa na uwezo wa kukamata nyadhifa kubwa za kitaaluma.
            Katika mwaka wa 1954 Sayyid Omar Abdalla aliandika barua ya kukumbusha azma yake ya kupata fursa ya kuendelea kusoma katika nchi za Kiarabu na Kiislamu na alitaka kuwa akiwa anarudi kutoka Uiengereza apewe ruksa ya kwenda Kuhiji Makka kisha apite Hadharmout huko Yemen akae kidogo ajifunze kwa Kiarabu masomo aliokwisha kuyasoma kisha ndio arudi nyumbani, alikubaliwa hilo na safari yake alilipiwa na Serikali.
            Kuna kumbukumbu ambayo sijaipata lakini niliisikia kuwa alipokwenda Makka na kupita Hadahrmout alichelewa kwa siku 2 kurudi Zanzibar kwahio alikatwa mshahara wa siku 2 lakini hapo hapo kutokana na kufanya vizuri masomo yake alipandishwa cheo na kupatiwa nyongeza ya mshahara.
Sayyid Omar Abdalla akiwa na Masheikhe na walimu mbalimbali hapo Ukutani

          Fatwana na mie katika makala inayofwata kumuangalia Sayyid Omar Abdalla akiwa amerudi masomoni kazi zake na kuhama Zanzibar kuhamia visiwa vya Comoro.  

Saturday, 10 February 2018

Mwinyi Baraka
Sayyid Omar bin Abdalla

Sayyid Omar bin Abdalla ni kati ya wasomi wachache aliosoma katika vyuo vikuu mbalimbali akapata shahada ya elimu zote mbili za dunia na akhera. Alianza masomo yake ya juu katika Chuo cha Makerere, kisha akenda kusoma Uiengereza Cho cha Oxford na kusoma katika baadhi ya nchi za Kiarabu kwa kuendelea kusoma. Alikuwa mhubiri mkubwa wa dini ya Kiislamu duniani kote aidha alipohama visiwani Zanzibar alipewa hadhi ya kuiwakilisha kisiwa cha Comoro katika masuala ya dini nchi za nje na mwishowe alikuwa ni mwakilishi wa Jumuia ya Kiislamu ya Saudi Arabia hadi anafariki. Nitaanza na maneno haya ya kimombo “In the popular mind love is usually linked with romance and sex. I never imagined that the first person I would fall madly in love with would be a short, flamboyant, erudite, bespectacled, snaggletoothed black man from Zanzibar who spilled things, wore long coats over a sarong, spoke in rich Edwardian English, had infection laugh and walked with a cane.” 

Maneno hayo yamesemwa na Michael Sugich katika kitabu Sign on the HorizonsMeeting with Men of Knowledge and Illumination. Tafsirii ya juu juu mapenzi ya mtu kwa mtu mwengine huwa ya kijinsia lakini Michael Sugich ni kinyume anasema hajakutana na mtu akafikia kuwa anampenda kuwa naye kama Sayyid Omar bin Abdalla, msomi ambaye amebobea, mwenye kuvaa kanzu na majuba, mzee wa Kiafrika kutoka visiwa vya Zanzibar ambaye huzungumza mombo lilokamilika la mtindo wa Edwardian. Sayyid Omar bin Abdaala (Mwinyi Baraka). Unapotaka kuwalinginisha Sayyid Omar bin Abdalla na Sheikh Abdalla Saleh Farsy kuna sehemu wanakutana na kuna sehemu wanaachana. Wote wawili walibobea katika elimu ya dini na historia, Sheikh Abdalla Saleh Farsy kaandika na kutoa mawaidha, Sayyid Omar bin Abdalla hakuandika ila sehemu ndogo kabisa ya makala kama kwenye Jarida la Mazungumzo ya Walimu Jarida ambalo walimu wa visiwani Zanzibar wakiandika na kutoa maoni yao na maelezo mbalimbali. Sayyid Omar Abdalla kenda kusoma katika vyuo Vikuu, Sheikh Abdalla Saleh Farsy amesoma kwa Masheikhe mbalimbali, wote walipata kuwa walimu wakuu katika chuo cha Kiislamu kiitwacho Muslim Academy, wote wawili wakitoa mawaidha ya wiki katika radio ya Sauti ya Zanzibar. Sheikh Abdalla Saleh Farsy alikuwa Kadhi alipokuwa Visiwani Zanzibar na Mombasa Kenya, Sayyid Omar bin Abdalla yeye alikuwa Balozi na Dai mkubwa wa kuzunguka dunia nzima katika mabara yote katika kulingania Uislamu amesafiri zaidi ya nchi 80 duniani kote. 

Jina kamili la Sayyid Omar bin Abdalla ni Sayyid Omar Abdalla Abi Bakr bin Salim, mzaliwa wa visiwani Zanzibar ingawa wengine huelezea kuwa amezaliwa katika visiwa vya Comoro akiwa yatima alipelekwa visiwani Zanzibar katika mwaka wa 1923 na kukulia na kusoma Unguja. Kumbukumbu katika faili lake binafsi katika Ofisi za Nyaraka (ZNA AB 86/47) linathibitisha kuwa kazaliwa Zanzibar katika mwaka wa 1918 na aliwahi kuthibitisha mwenyewe kuwa amezaliwa Zanzibar katika mahojiano na Shirika la TV ya Kenya, KBC. Ameanza masomo yake ya Qur‟an akiwa kijana mdogo alipojiunga na chuo cha Maalim Abd al-Fatah Jamal al-Leyl maarufu Sharif Aboud. Mwalimu huyu alikuwa akifundisha wanafunzi wake kuhifadhi Qu‟ran kwa kadri wawezavyo na baadhi ya wanafunzi waliopita hapo waliweza kuhifadhi Mshafu mzima katika kipindi cha baina ya miaka 3 na 5. Shariff Abbud alimuingiza Sayyid Omar Abdalla ambaye kwa jina jengine akiitwa Mwinyi Baraka kujifunza Usufi na kujifunza juu ya Tarika ya Qadiriyya. Kama ilivyopata kuwa dasturi ya watoto wa visiwani baina ya sala ya Magharibi na Isha huwenda kujifunza elimu mbalimbali juu ya Uislamu kwenye uga wa Fiqhi, Tafsiri, lugha ya Kiarabu, Hadithi za Mtume Muhammad (SAW), Sira na fani nyenginezo, Sayyid Omar bin Abdalla alikwenda katika Misikiti mbalimbali akiwa kijana mwenye umri mdogo kwenda kusoma fani mbalimbali. Alikuwa akipenda kujua mashairi ya Kiarabu na kujifunza kusomna Maulidi. Alionyesha uwezo mkubwa wa kudhibiti alivyosomeshwa na haya yalikuja kuoenekana hata ukubwani mwake uwezo wake wa kuhifadhi ulikuwa mkubwa sana na nafasi yake ya kusoma ilikuwa ndogo mno na alikuwa akipenda kulala sana, ndipo wakati mmoja alipoulizwa na Michael Sugich kwanini akipenda kulala sana akamjibu kwa mkato “Unapolala huwa unaepukana na dhambi kwani huwa huna ulitendalo.” 

Sayyid Omar akipenda maneno ya mkato na kukufanya upende kumuuliza ili upate maneno ya ufasaha na jawabu muwafaka. Alipofika umri wa kijana alisogea kwa Sayyid Omar bin Sumayt wengine wanaelezea alijifunza Tariqa ya Shadhiliya kwa Bin Sumayt. Katika mwaka wa 1928 alisoma GCS ikiwa ni Government Central School ambapo alimalizia darasa la 8 kisha akaendelea masomo ya sekondari GSS ikiwa ni Government Secondary School, alikuwa kati ya wanafunzi wa mwanzo kuingia skuli ya sekondari chini ya mwalimu Hollingsworth na kote alikosoma alikuwa ni mwanafunzi anayofanya vizuri katika masomo yake, alisoma kwa miaka 3 masomo ya sekondari ingawa kwengine kunaonyesha kuwa alisoma kwa miaka 4 hadi mwaka wa wa 1936. Alielekea kusoma masomo ya Diploma katika Chuo Kikuu cha Makerere kiliopo Uganda katika mwaka wa 1939, alianza kusomea uwalimu kwa miaka 2 na mwaka wa mwisho ukiwa mwaka wa 3 alitakhasusi na somo la elimu ya viumbe (Biology), Sheikhe huyu ndio aliokuwa mwanafunzi wa mwanzo wa visiwani kupata shahada ya somo la ''Biology” na elimu hio ilikuja kumsaidia sana katika kutoa mawaidha hasa akielezea elimu ya uzazi, suala la kutoamini Mwenye-enziMungu, mabadiliko ya viumbe (evolution) na mwanzowake n.k. 

Alipokuwa ansoma Chuo Kikuu cha Makerere huko Uganda, Sayyid Omar Abdalla akicheza mchezo wa mpira na cricket na alikuwa na darsa akisomesha wanafunzi wenzake wakati huo wakikuwepo kina Chief Abdalla Fundikira, Marehemu Idrissa Abdul Wakil aliokuwa Rais wa awamu ya 4 wa Zanzibar, Spika wa mwanzo wa Baraza la Wakilishi Zanzibar Ali Khamisi, Sheikh Ali Muhsin Barwany, Maalim Zubeir Rijal, Mwalimu Abdulrasul Khako na wengineo, baadhi ya wanafunzi wake katika darsa hizo wakimfanyia mzaha wakimwambia watamkimbia kwani walipokuwa nyumbani walibanwa kutoweza kujifaragua na ujana wao na wapo huko naye anawabana upande wake, Sayyid Omar akiwajibu „ujana ni sehemu ndogo ya maisha, musipende kuendekeza.” Sayyid Omar Abdalla katika Ujenzi wa Taifa, Ujenzi wa Uwanja wa Amani Sayyid Omar Abdalla na walimu wenzake wa Muslim Academy. Aliporudi masomoni katika mwaka wa 1943 alianza kusomesha katika skuli ya Dole wakati huo zikiitwa Rural Middle School (RMS) hapo alisomesha vijana wengi ambao badaye walikuja kushika sehemu muhimu katika Serikali ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla, alimfundisha katika skuli ya Dole, Rais mstaafu wa wamu ya pili ya Tanzania, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi aidha akifundisha darsa katika Msikiti wa Shariff Aboud. 

Fatwana na mie na sehemu ya pili ya msomi huyu katika toleo lijalo... 

Friday, 9 February 2018

JOHN KETO
HISTORIA YANGU KUHUSU ELIMU YANGU NA UZOEFU 
KATIKA KAZI ZA KUJENGA TAIFA
(Kwa hisani ya Dr. Nzige)

Waliosimama wa nne kulia ni John Keto University of Edinburgh 1953
Nilizaliwa Misozwe katika Wilaya ya Muheza  Mkoani Tanga (wakati ule ukiitwa  Jimbo la Tanga  tarehe 15/08/1917.

Kwa kuwa baba yangu alikuwa mwalimu nilipata bahati ya   ya kuanza elimu katika shule  ya misheni  ya U.M.C.A (University  Mission to Central Africa)pale  Misozwe mwaka 1922.
Baba  alipohamia  Magila Msalabani kwa ajili ya kusomea kazi ya ushemasi,ikabidi  nihamie  huko na kuendelea  na masomo yangu ya shule  ya msingi  kwenye  shule  ya St. Martins (zamani  ikiitwa  Hemvumo).

Mwaka  1928 (baba wakati  huo akiwa  Padre) nilihamia  shule ya central  school kiwanda kwa kuwa   baba  alihamishiwa kutoka  Magila   kwenda  kuwa Padre wa Mtaa  wa Kizara.

Hapo kiwanda  nilisoma  na kupata  cheti  cha Territorial  St x (central  school  leaving  certificate) mwaka 1932; na  mwaka  uliof uata  (1933)  nilikwenda minaki kusomea kazi ya ualimu. Nilipokuwa hapo  minaki  nilisomea   kwanza cheti cha  ualimu  wa grade  I na kufaulu , mwaka huohuo  nikajaribu mtihani wa kwenda  Makerere  na nikafaulu. Kwa hiyo  badala ya  kupelekwa kufundisha  nilipata  nafasi ya kuendelea  na masomo zaidi ya Diploma in Educationb kule Makerere.

Mwaka 1940 nilifaulu kupata cheti change cha Diploma in Education pamoja na Cambridge   School Certificate na kurudi Tanzania ili kuanza  kazi yangu ya Ualimu.

Shule yangu ya kwanza kufundisha  ni U.M.C.A Korogwe Middle   School ambapo  nilianzishwa St. VII. Nilifundishwa  Korogwe  kwa miaka miwili  1940  na 1941 nikiwa mwalimu mkuu, na mwaka 1942 nikahamishiwa  kwenda  kufundisha  Minaki.

Wakati nikifundisha    Minaki  nilijiandikisha  katika Woolssey Hall   College  ya London, Uingereza  ili kupata  masomo kwa njia  ya Posta . Masomo  hayo pamoja na cheti  nilichopata cha London  Matriculation ndivvyo  vilivyoniwezesha  kukuballiwa kupata  Scholarship Ya British Council   mwaka 1950 kwenda kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh, Scotland, Uingereza.

Huko Edinburgh nilisoma  kwa miaka  mitatu na kupata degree yangu ya M.A katika  masomo yafuatayo:- Political Economy,Economy History,British History,Constitutional Law, Botanical Science,Moral Philosophy na  English Literature. Mwaka 1954 nikarudi nyumbani na kwenda  Minaki kuendelea  kufundisha wakati huo nikiwa makamu wa mkuu wa chuo.

Niliporudi mwaka 1954 nilikuta  chama cha siasa cha TANU (Tanganyika  African National Union) kimekwisha  kuanzishwa, kwa hiyo nikajiunga  nacho na nikachaguliwa  kuwa  mwenyekiti wa Tawi la TANU Wilaya ya Kisarawe.

Nilijitahidi  kuongoza TANU katika Uzaramo hadi mwaka 1958 wakati nilipoteuliwa na chama kuwa mgombea Mwafrika  wa kiti cha ubunge  wa Jimbo  la Tanga. Nilifaulu na ikabidi kufanya   shughuli  za ubunge huku nikiendelea na kazi ya  ya kufundisha  Minaki, baada ya kuafikiana  na mkuu wangu wa Chuo (Fr. Nash) kuwa itanilazimu kwenda Tanga ikiwa  kkutakuwa na jambo lolote la kisiasa litakalonihitaji jimboni kwangu.

Kwa bahati mbaya  kanuni za TANU hazikuruhusu mwanachama kupokea mshahara zaidi ya mmoja ikiimaanisha kuwa mtu kama mimi kupokea mshahara  wa ualimu na malipo ya ubunge.   Kwa hiyo  ilipofika awamu  ya  pili ya uchaguzi mwaka 1960 sikuweza  kugombea tena ubunge, kwa kuwa nilikataa kuacha kazi yangu ya ualimu kwa sababu ambazo nilimweleza Rais Nyerere na akanikubalia.

Mwaka  1961 tulipopata uhuru wetu  Rais Nyerere aliniita  ofisini  kwake  Dar es salaam akaniuliza  kama niko tayari kwenda   Dar es salaam ili kuwa mwenyekiti wa Public Service Commission. Nilimpa sababu  zangu  nilizopata kupampa huko nyuma  zikiwamo uhaba wa walimu kwenye shule yangu ya Minaki, Yeye allinijibu kwamba atanisaidia kuondoa hilo tatizo  kwa kutuletea  walimu wawili wazungu badala yangu. Kwa hiyo  tuliafikiana na nikahama kwenda Dar es Salaam.
Mfumo wa Huduma  za pamoja  za mawasilano  wa Africa ya Mashariki ulipotengenezwa upya. Tanganyika ilipewa huduma  ya Posta kwa hiyo mwaka 1964 Rais Nyerere alimtuma  waziri Amir Jamal kuja kuniomba  niende Nairobi kushika wadhifa wa Postmaster General wa Africa nilikuwa  pia mwenyekiti wa kampuni ya Posta na Simu( Post & Telecommunicationb Company Ltd).

Mwaka 1969 baada ya kuundwa  kwa Jumuiya  ya Africa Mashariki 1967, Makao makuu ya Posta  yalihamishwa kwenda Kampala Uganda, Ambako nilikaa mpaka nilipostaafu mwaka 1976 na kurudi nyumbani Tanzania.

Niliporudi nyumbani kwangu Korogwe, Kwamba mwaka 1977 nilikuta  Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekwis ha  kuanzishwa   kwa hiyo nikajiunga na wanachama wengine wa kijiji katika kuhimiza  vikao vya chama   na   kuendesha miradi ya siasa ya kujitegemea  kwa mujibu wa miongozo ya  Chama. Nilikuwa pia mwanachama wa ushirika wa uzalishaji mali vijijini.

Mwaka 1978 nikapata ujumbe  kkutoka magila Muheza kuniomba nikawe mkuu wa Shule  ya Hegongo (iliyoitwa  Muheza Secondary School hapo awali) badala ya  Mw. Stephene Mhando. Nilianzia kazi hiyo tarehe 1/06/1978 nikiwa 1985 nilipostaafu na kurudi Korogwe.

Kwa sasa  nipo hapa Majengo nikiwa mwenyekiti  wa sehemu ya Wazee wa CCM na mwanachama wa kikundi cha mradi wa kufuga  nyuki wa TASAF.

Mungu  Uibariki Afrika
Mungu Uibariki Tanzania

…………………..
Majengo Korogwe
10/05/2012


CURRICULUM VITAE
OF
MR. JOHN KETO
1.    Date and   place  of Birth
Born on 15th August, 1917, at Misozwe in Muheza District of Tanga Region.
Married (now widow) with six children, two of them now dead

2.   Education
i.     At Kiwanda  Central School and Minaki
Teacher Training College (1928 – 1937)
Awarded Grade II and Grade I Teachers Certificates
ii.   At Makerere College, Uganda(1938 – 1940)
Awarded Cambridge school certificate and Diploma in Education
iii.  At Edinburgh University, Scotlad (Oct 1950 – July 1954) awarded M.A degree in following subjects.
·         Political  History : Constitutional law
·         Botanical Science: Moral Philosophy
·         English Literature
3.      Career
i.                    Teacher at Korogwe Middle School(1941)
ii.                  Teacher at Minaki (1942 to Sept 1950) and again 1954 to 1961
iii.                Chairman Public Service Commission Tanzania 1961 – 1964
iv.                 Postmaster General, East Africa 1964 to 1968
v.                   Director General E.A.P and T. Corporation    1968 TO 1976
vi.                 Chairman  E.A. External Telecoms 1964 to 1976
vii.               Headmaster Hegongo Secondary School 1978 to 1985

4.    Part Time  Activities
a.                   Member of Council University College
Dar es Salaam
b.                  Member, East  Africa (Swahili) Literature
c.                   Diwani Muheza and Korogwe District Council
d.                  Member of Legislative Council

Prepared by Mwalimu John Keto, Majengo Korogwe

John Keto katika kitabu cha Abdul Sykes: 
''Ilikuwa chini ya hali ya hewa ya kisiasa kama hii ndipo TANU iliingia kwenye uchaguzi wake wa kwanza katika Tanganyika. Tanga ambako UTP ilikuwa imara TANU iliwachagua John Keto, B. Krishna na R. N. Donaldson kama wagombea wake. John Keto akiwa miongoni mwa walimu wa St. Maryís School, Minaki na alikuwa amefanya kazi kubwa katika siku za mwanzo kufungua matawi ya TANU huko Kisarawe. TANU iliamua kumteua Keto kusimama Tanga ambako ndiyo kulikuwa kwao. Katika uchaguzi huu serikali iliacha uandikishaji wa wapiga kura kwa vyama vyenyewe. Mzee Makoko Rashid, mwanasiasa wa makamo mwenye msimamo thabiti wa chama na kijana Mmaka Omari walikuwa maofisa waandikishaji wa wapiga kura katika  wa TANU mjini Tanga. Makoko na Mmaka walikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la kuwaandikisha watu ambao hawakutimiza masharti yaliyoelezwa na ilani ya uchaguzi. Katika ghera yao kwa TANU kushinda ule uchaguzi muhimu, Mzee Makoko alimsajili Mwafrika yoyote aliyetaka kuipigia kura TANU bila kujali sifa zake. Bhoke Munanka alikamatwa vilevile kule Mwanza kwa kosa hilo hilo. Hakukuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya Mmaka Omari kwa hiyo aliachiwa huru mara tu baada ya kukamatwa kwake. Mzee Makoko Rashid alipatikana na hatia na alihukumiwa kufungwa jela.  Adhabu ya kifungo ilidhoofisha sana afya yake na mara baada ya kufunguliwa kutoka gereza baya sana la Maweni Mzee Makoko alifariki.''

Moja ya barua za John Keto:
(John Keto kwa J. D. Turner, D. C. Kisarawe, 11 Novemba, 1955 TNA/57/A.6/23).

Tuesday, 6 February 2018

Uhuru, Jumanne Februari 6, 2018
ALLY KLEIST SYKES
Mpigania uhuru aliyempokea Nyerere Dar es Salaam
L Alimkabidhi kadi namba moja ya TANU
L Mwandishi wa karatasi zilizowakera Wakoloni
NA MUSSA YUSUPH
UHURU wa Tanganyika haukuwa kazi rahisi kupatikana kama ambavyo wengi wanadhania.
Ili kuwa ni shughuli pevu iliyohitaji kujitoa kwa hali na mali ili kuhakikisha Waafrika kutoka Tanganyika ambalo lilikuwa koloni la Uingereza, wanajitawala.
Jitihada hizo zilifanywa na wapigania uhuru mbalimbali waliounganishwa kupitia chama cha Tanganyika National Unioni (TANU), kilichoundwa na na watu waliojawa na shauku la kujitoa kwenye makucha ya kikoloni.
Ally Kleist Sykes mzaliwa wa Mtaa wa Gerezani, Kariakoo Dar es Salaam, ni miongoni mwa waasisi waliopigania uhuru wa Tanganyika ambaye ana mengi ya kukumbukwa.
Mzee huyo aliyezaliwa Oktoba 10 mwaka 1926 kisha kufariki Dunia Mei 19 mwaka 2013 alikuwa mzalendo aliyeanza harakati za kisiasa kwenye miaka ya 1950.
Ally Sykes ndiye aliyemwandikia na kumkabidhi Hayati Mwalimu Julius Nyerere kadi ya TANU namba moja.
Pia alikuwa miongoni mwa waasisi wa TANU, kati ya wazee watu saba waliokuwa katika kamati ya TAA iliyounda TANU.
Alikuwa miongoni mwa wafadhili wakuu wa TANU, huku akiwa tegemeo la chama hicho katika kutekeleza mikakati hatari dhidi ya utawala wa Uingereza.
Katika siasa za sasa Mzee Ally Sykes anaweza akaelezewa kama "Mzee wa fitna" kwani alikuwa majukumu ya kuwagombanisha wananchi dhidi ya serikali ya kikoloni.
Majukumu hayo aliyatelekeza kwa kuchapa karatasi ambayo Waingereza waliyaita ya kuchochea ghasia kwani majasusi wa serikali ya kikoloni walimfahamu kwa uhodari wa kutengeneza mambo.
Waingereza walipata wakati mgumu kumkabili kwani licha ya uhodari wa kisiasa aliokuwa nao, Ally Sykes pia alikuwa na medali ya mlenga shabaha mahiri, aliyopata kwenye Vita Kuu vya Pili ya Dunia.
Kwenye vita hiyo Ally Sykes alikuwa kwenye bataliani ya sita (Battalion 6 Burma Infantry) King's African Rifles (KAR) 
Hakika Ally Sykes alikuwa mzalendo, mweledi wa mambo na miongoni mwa waasisi muhimu wa TANU ambaye sahihi yake ndio iko katika kadi ya TANU ya Mwalimu Nyerere.
Umaarufu wake ni kama aliurithi kutoka kwa Baba yake Mzee Kleist Sykes aliyekuwa watu mashuhuri  Dar es Salaam katika miaka ya 1900 hadi alipofariki mwaka 1949.
Baba yake alikuwa maarufu kwa kuwa alilelewa na Affande Plantan aliyekuwa askari kiongozi katika jeshi la Wajerumani lilokuja Tanganyika na Herman Von Wissman.
Kleist alikuwa ndiye katibu muasisi wa African Association mwaka 1929 chama kilichokuja baadae kujibadili na kuwa TANU ambacho Ally Sykes akiwa mmoja wa waasisi.
Pia baba yake aliasisi Al Jamiatul Islamiyya Fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika) na kupitia jumuia hiyo akajenga shule ya kwanza ya Kiiislam Dar es Salaam, ambayo ilisomesha Qur’an pamoja na elimu ya kimagharibi.
Jumuiya hiyo ilichangia vijana wengi wa kiislamu kuingia kwenye siasa za TAA na TANU katika harakati za kudai uhuru.
AKUTANA NA NYERERE
Ally Sykes na kaka yake Abdulwahid Sykes ndio watu wa mwanzo kumpokea Mwalimu Nyerere alipokuja Dar es Salaam mwaka 1952.
Nyerere alifika nyumbani kwa akina Sykes na ilijenga urafiki ambao ulipitiliza na kuwa udugu mkubwa wa mapenzi ya dhati si baina yao tu bali hata kwa wake na mama zao.
Mama yake Nyerere, Bi. Mugaya mara kwa mara alipenda kumtembelea nyumbani Bi Mruguru biti Mussa ambaye ndiye mama wa Sykes.
Pia Mama Maria Nyerere alikuwa mwenye urafiki wa karibu na Bi. Zainab ambaye ni mke wa Ally Sykes aliyekuwa akiishi Mtaa wa Kipata.
Wakati huo harakati za kuanzisha TANU zilikuwa zimepamba moto huku fitna za Waingereza kuwatokomeza viongozi shupavu wa TAA kama Hamza Mwapachu, Dk. Vedast Kyaruzi, Dk. Wilbard Mwanjisi, zilikivunja nguvu chama hicho.
Ndio maana TANU ilipokuja kuasisiwa mwaka 1954 Ally Sykes kadi yake ya TANU ikawa namba mbili, Nyerere namba moja, Abdulwahid Sykes kadi yake namba tatu, Dossa Aziz kadi namba nne na John Rupia kadi yake ilikuwa namba saba.
Kipindi hicho Ally Sykes alikuwa Katibu wa Tanganyika African Government Servants Association (TAGSA) na vilevile alikuwa mwakilishi wa chama hicho katika Kamati ya Uajiri ya Serikali (Government Establishment Committee).
Thomas Marealle ndiye alikuwa rais wa TAGSA na Rashid Kawawa alikuwa mwanakamati.
Wanasiasa hao walijipa jina la ‘’Wednesday Tea Club’’ wakikutana kila siku ya Jumatano kunywa chai pamoja na kupanga mikakati ya kuwang’oa Waingereza katika ardhi ya Tanganyika.
Kupitia Ally, Abdulwahid na Dossa Aziz, Nyerere aliweza kujuana na wenyeji wa Dar es Salaam maarufu baadhi yao ni Sheikh Hassan bin Amir, Mshume Kiyate, Jumbe Tambaza, Sheikh Suleiman Takadir, Clement Mtamila, Titi Mohamed na Tatu biti Mzee.
NYARAKA ZA HISTORIA YAKE
Baadhi ya nyaraka za historia alizozitunza nyumbani pake na kumpatia Mohamed Said, mpaka Ally Sykes, anafariki dunia zinadaiwa bado zilikuwa kwenye mikono ya Mohamed Said.
Ally Sykes aliwahi kumlalamikia kuwa nyaraka hizo ni mali ya taifa na lazima azikabidhi serikalini kwa kuhifadhiwa na kuwekwa kama urithi wa kizazi kijacho.
Inadaiwa kuwa nyaraka za Ally Sykes zinakwenda zimeelezea historia tangu babu yake Sykes Mbuwane alipoingia Tanganyika kutoka meli ya kivitia ya Wajerumani iliyotia nanga Pangani akitokea Msumbiji.
Nyaraka hizo zinadaiwa kuwa na barua za wanasiasa wa mwanzo katika Tanganyika mbali historia ya baba yake.
Inasemekama zimeelezea habari kuhusu wazalendo na machifu, wanasiasa wenye asili ya Kiasia na Waingereza wenyewe waliokuwa watawala.
Ally Sykes ameelezea harakati za Dk Joseph Mutahangarwa, Chifu Abdieli Shangali wa Machame, Paramount Chief Thomas Marealle wa Marangu, Chifu Adam Sapi Mkwawa wa Wahehe, Chifu Harun Msabila Lugusha na Dk. Wilbard Mwanjisi.
Wengine ni Abdulkarim Karimjee, Dk. Vedas Kyaruzi, Liwali Juma Mwindadi, H.K. Viran, Stephen Mhando, Dossa Aziz, Ivor Bayldon, Yustino Mponda, Ivor Bayldon, Rashid Mfaume Kawawa, Bhoke Munanka, Rashid Kheri Baghdelleh na  Robert Makange.
Wanasiasa wengine aliowaelezea ni Saadani Abdu Kandoro, Malkia Elizabeth, Chief Secretary Bruce Hutt, Gavana Edward Twining, Gavana Ronald Cameron, Mwalimu Thomas Plantan na ndugu zake Schneider Abdillah Plantan na Ramadhani Plantan.
Pia wapo wakina Mwalimu Mdachi Shariff, Mwalimu Nicodemus Ubwe, Kassela Bantu, John Rupia, Hamza Kibwana Mwapachu, Othman Chande, Leonard Bakuname, Stephen Mhando, Oscar Kambona, Peter Colmore, Albert Rothschild, Ali Mwinyi Tambwe, Alexander Thobias, Japhet Kirilo, Joseph Kimalando, Ian Smith, Roy Welensky, Jim Bailey na Kenneth Kaunda.
Ally Sykes kwenye nyaraka hizo zinadaiwa amewaelezea wakina, Meida Springer, John Hatch, Gretton Bailey, Brig. Scupham, Dome Okochi Budohi, Annur Kassum, Nesmo Eliufoo, Yusuf Olotu, Joseph Kimalando na Mwalimu Julius Nyerere kwa nyadhifa walizokuja kuzishika kwenye Tanganyika huru.
xxxx