Wednesday, 23 May 2018


MCHANGO WA MAANDISHI WA NDG. KABWE ZUBERI RUYAGWA ZITTO, MB KWENYE MAKADIRIO YA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA


Mh. Zitto Kabwe


''Hatuwashi tena mwenge na kuuweka mlimani Kilimanjaro, hatumuliki tena nje ya mipaka yetu, hatuleti tena matumaini pale pasipo na matumaini, hatupeleki tena upendo kule kuliko na chuki, na hatuleti heshima pale palipojaa dharau. Sisi si Tanzania ya Mwalimu Nyerere, sisi sasa ni Tanzania mpya, Tanzania mbaya, Taifa lililokiuka misingi yake, Taifa linalowaacha Wapelestina wakiuawa kinyama, na sasa linalosapoti waonevu.''

1. Sisi si Tanzania ya Nyerere, Ni Tanzania Mpya, Tanzania Mbaya - Inayokalia Kimya Mauaji ya Kinyama ya Wapalestina, na Kusapoti Waonevu.

[Sehemu ya Kwanza na ya Hotuba ya ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto (MB) Juu ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka 2018/19]

Mheshimiwa Spika,
Msimamo wa Tanzania kuhusu mgogoro wa Israel na Palestine unaelezwa vizuri sana na nukuu hii ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa Mwaka 1967 na ndio umekuwa Msingi wa Sera yetu ya Mambo ya Nje kwa miaka mingi kabla ya utawala wa sasa wa CCM mpya:

“[......] Tanzania’s position. We recognize Israel and wish to be friendly with her as well as with the Arab nations. But we cannot condone aggression on any pretext, nor accept victory in war as a justification for the exploitation of other lands, or government over other peoples.”

Kwamba Tanzania inaitambua Israel na inapenda kuwa na urafiki nayo pamoja na urafiki na mataifa mengine ya kiarabu. Lakini hatuwezi kukalia kimya uvamizi kwa namna yeyote ile. Pia ushindi vitani hauhalalishi unyonyaji dhidi ya ardhi ya wengine au dhidi ya Serikali za watu wengine. Msingi huu unaendana kabisa na dhamira  ya sasa ya Sera ya Mambo nje. Hata hivyo hali ni tofauti kabisa. Mambo tunayoyafanya kwenye sera yetu ya Mambo ya Nje yanamfanya Mwalimu Nyerere ageuke huko kaburini kwake. Nitaeleza kwa mifano.

Mheshimiwa Spika,
Oktoba 26, 2016 kulikuwa na kikao cha wajumbe wa Nchi 21 zinazounda ‘Kamati ya Urithi wa Dunia’ ya UNESCO - Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, kupiga kura ya kupitisha makubaliano ya kuridhia kuupa hadhi ya Urithi wa Dunia Mji wa Jerusalem pamoja na moja ya majengo ya mji huo (Temple Mount), na kufungamanishwa na uasili wake na si hali ya sasa inayotokana na uvamizi wa Israel juu ya eneo hilo la lililoko Jerusalem Mashariki (lililovamiwa mwaka 1967 na mpaka leo kutambuliwa na UN kama eneo la Palestina, ambao wanauona ndio Mji Mkuu wa nchi ya Palestina iwapo makubaliano ya ’Two States Solution’ yatafikiwa).

Tanzania ilikuwa ni mjumbe wa Kamati hiyo ya nchi 21, na kwa mshangao wa wengi duniani, ilipiga kura kuzuia Azimio hilo, na kutaka azimio ‘Laini’ zaidi kwa Israel. Nchi marafiki zetu wa asili kule Umoja wa Mataifa (UN) ambazo nazo ni wajumbe wa kamati ile, kama Cuba, Vietnam na Angola zilipiga kura kuunga mkono azimio hilo, zikitushangaa mno kwa utetezi wetu kwa Israel ambao haukutarajiwa, hasa ikiwa msimamo wetu kama nchi siku zote umekuwa ni kutambua Jerusalem Mashariki kama eneo la Wapalestina ili kupata muafaka wa nchi mbili.

Sisi ACT Wazalendo tulihoji juu ya jambo hili linalokwenda kinyume na Sera ya Nje ya Nchi yetu. Msimamo wa Tanzania ni kukubaliana na UN kupinga uvamizi wa eneo hilo uliofanywa na Israel. Serikali ilitoa majibu mepesi tu, tena pembeni, kuwa upigaji kura ule haukuwa msimamo rasmi wa nchi yetu, ni ukiukwaji wa sera yetu ya mambo ya nje, na kuwa ni jambo ambalo Afisa wetu kwenye mkutano ule wa UNESCO alilifanya kwa makosa, na hivyo hatua zingechukuliwa dhidi yake.

Ni dhahiri majibu hayo yalikuwa ni ghiliba tu, matukio ya karibuni yameonyesha kwa uwazi sura mpya ya Taifa letu, pamoja na msimamo mpya wa Sera yetu ya mambo ya nje. Kwenye Diplomasia matendo ya nchi huwa na maana zaidi kuliko maneno ya wanadiplomasia wake. Matendo yetu yafuatayo ya karibuni yameonyesha kuwa Tanzania hatuisapoti tena Palestina:

1. Baada ya kuwaangusha Wapalestina kule Paris kwenye Mkutano wa UNESCO, Serikali iliahidi kuwa ingemchukulia hatua Afisa yule wa Wizara ya Mambo ya Nje aliyekwenda kinyume na Sera yetu ya Mambo ya Nje, hatujafanya hilo, zaidi tumempandisha cheo na kumteua kuwa Balozi wetu wa Ankara, Uturuki. Jambo hilo linaonyesha kuwa tulimtuma Balozi Elizabeth Kiondo apige kura namna ile kule UNESCO, na sasa tumempa cheo zaidi kwa kazi njema aliyoifanya. Jambo hili linaonyesha kuwa kwa sasa tunawaunga mkono Waisrael, na hatuko tena na Wapalestina.

2. Kwa sasa tumeamua kufungua ubalozi wetu Israel, Tel Aviv, kuongeza uchungu kwenye Kidonda, tukachagua wakati huu wa maazimisho ya miaka 70 ya Uvamizi wa Israel katika ardhi ya Taifa la Palestina kuzindua ubalozi wetu huo. Jambo hili linafanyika kukiwa na tuhuma kuwa hata huo Ubalozi unagharamiwa na Israel yenyewe, ndio maana tumepangiwa hata kipindi cha kuufungua. Kidiplomasia kuufungua ubalozi wetu katika wakati huu ni kuazimisha uvamizi wa Israel katika ardhi ya Palestina. Maana tulikuwa na uwezo wa kuchagua wakati mwengine wowote kufanya uzinduzi wa ubalozi wetu, lakini kwa kuwa aliyegharamia uwepo wa ubalozi huo (Israel) alitaka tuufungue wakati huu wa maazimisho ya miaka 70 ya Uvamizi wa Israel kwa Palestina, ilitubidi tufanye hivyo. Jambo hilo limeonyesha kuwa kwa sasa hatuungi mkono tena utu (Palestina) bali tunamtumikia Kila mwenye kitu (Israel).

3. Wakati akiwa ziarani Israel, Balozi Mahiga alifika sehemu ya miji inayokaliwa kimabavu na Israel ambayo inapakana na Ukanda wa Gaza. Na baadaye alihojiwa na Televisheni ya Taifa ya Israel, ambako alionyesha tu masikitiko yake kwa Waisrael wanaokaa maeneo hayo kwa kusumbuliwa na mashambulizi ya Hamas. Lakini hakulaani kabisa uendelezaji wa Israel kujenga makazi kwenye maeneo hayo ya uvamizi kama Wanadiplomasia wengine wa nchi zenye msimamo wa ‘Two States Solution’ kama sisi wanavyofanya. Balozi Mahiga mwanadiplomasia mzoefu na mbobezi, Kutokulaani kwake makazi yale haramu ni jambo la makusudi kabisa, si bahati mbaya. Ni kitendo cha kutuma salamu kwa Wapalestina kuwa tunaunga mkono uendelezaji makazi wa Israel katika maeneo hayo iliyoyavamia.

4. Tanzania imetajwa na vituo mbalimbali vya habari vya Kimataifa kuwa ni katika nchi 33 ambazo zilihudhuria ufunguzi wa ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem, Mei 14, kilele cha maazimisho ya miaka 70 tangu uvamizi wa Israel katika maeneo ya Wapalestina. Chanzo cha taarifa ya Tanzania kuhudhuria ni Serikali ya Israel, ikitaja nchi ilizozialika na zilizohudhuria. Serikali yetu inasema inapinga uwepo wa Ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem, lakini hapo hapo inatajwa kuhudhuria uzinduzi huo. Picha tunayoitoa hapa kwa Wapalestina ni kuwa tunaunga mkono jambo hili la ufunguzi wa ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem.

5. Siku ya uzinduzi huo wa ubalozi wa nchi ya Marekani mjini Jerusalem, Jeshi la Israel liliwaua kwa risasi zaidi ya watu 54 wa Palestina, wakiwemo wanawake, watoto, walemavu na hata wanahabari. Nchi mbalimbali duniani zimelaani mauaji hayo. Nchi ya Afrika ya Kusini imekwenda mbali zaidi kwa kumrudisha nyumbani Balozi wake aliyeko Israel. Sisi Tanzania tulioikomboa Afrika Kusini tumekaa kimya, tumeshindwa hata kutoa kauli ya kulaani mauaji hayo. Kuhudhuria kwetu ufunguzi wa ubalozi na kukaa kimya juu ya mauaji hayo kunaonyesha tumewaacha rasmi Wapalestina.

Mambo hayo matano yanaonyesha kuwa sisi si tena ile Tanzania ya Mwalimu Julius Nyerere, sisi kwa sasa ni Tanzania Mpya (kama yasemavyo matangazo ya Ikulu yetu) - Tanzania mpya inayosimama na Waonevu wa dunia, Wauaji na Wavunja haki za wanyonge. Sisi si tena Tanzania ya kusimama na wanyonge, bali ni Tanzania ya kusimama na Wanyongaji kwa sababu ya maslahi ya kiuchumi.

Si ile Tanzania iliyoongoza Ukombozi wa Bara la Afrika kutoka kwenye makucha ya Ukoloni, bali ni Tanzania Mpya inayounga mkono na kushabikia ukoloni na Uvamizi. Sisi si ile Tanzania yenye msimamo mkali tuliyolipinga Taifa kubwa la Marekani dhidi ya Uvamizi wake kwa wanyonge wa taifa la Vietnam, bali sasa ni Tanzania mpya ya kuunga mkono Uvamizi wa Taifa onevu la Israel kule Palestina. Sisi si Tanzania ile iliyoitetea China ipate nafasi na kiti chake stahili kule UNO, bali sasa sisi ni Tanzania mpya inayowaacha watu wa Palestina bila utetezi wa hadhi, kiti na nafasi yake stahili kule UNESCO.

Sisi si ile Tanzania huru tena ya Mwalimu Nyerere, iliyowaheshimu watu na mataifa kwa sababu ya Utu wao na kuamini kwamba binaadam wote ni sawa. Sasa sisi ni Tanzania mpya, inayowapa heshima watu kwa sababu ya kitu inachotuhonga, tukiuza usuli wa Utaifa wetu kwa maslahi machache ya kifedha au kiuchumi.

Hatuwashi tena mwenge na kuuweka mlimani Kilimanjaro, hatumuliki tena nje ya mipaka yetu, hatuleti tena matumaini pale pasipo na matumaini, hatupeleki tena upendo kule kuliko na chuki, na hatuleti heshima pale palipojaa dharau. Sisi si Tanzania ya Mwalimu Nyerere, sisi sasa ni Tanzania mpya, Tanzania mbaya, Taifa lililokiuka misingi yake, Taifa linalowaacha Wapelestina wakiuawa kinyama, na sasa linalosapoti waonevu.

2. Kujengewa Uwanja wa Mpira na Msikiti Visiifanye Tanzania Iikumbatie Morocco na Kuacha Kuiunga Mkono Sahara Magharibi

[Sehemu ya Pili ya Hotuba ya ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto (MB) Juu ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka 2018/19]

Mheshimiwa Spika
Bado niko kwenye Sera ya mambo ya nje ya nchi yetu, si hii ya Tanzania mpya, bali ile Tanzania ya tangu wakati wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ya kusimama na wanyonge. Wakati tulipoamua kufuata ‘Diplomasia ya Uchumi’ bado msingi wetu huu wa kusimama na wanyonge ulibaki pale pale. Ndio maana wakati wa Rais Ben Mkapa na Jakaya Kikwete bado tulibaki kuwa ni sauti ya mataifa yanayoonewa kama Cuba (tukipinga vikwazo vya Marekani dhidi yao), Palestina na Sahara Magharibi.

Msingi huo wa kusimama na wanyonge ni muhimu zaidi kwa chama chetu cha ACT Wazalendo, ndio maana tulipinga ujio wa Mfalme wa Morocco hapa nchini Oktoba 23 - 25, 2016. Kwa kuwa Taifa hilo bado linaikalia kimabavu ardhi ya wanyonge wa Sahara Magharibi. Ndio msingi pia wa kutangaza wazi mahusiano yetu rasmi na Chama cha cha siasa na ukombozi wa Taifa hilo cha Polisario kinachopigania Uhuru wa nchi ya Sahara Magharibi.

Umoja wa Afrika (AU) uliamua kukubali ombi la Morocco kurudi bila masharti kwenye jumuiya hiyo. Ikimbukwe kuwa kwa zaidi ya miaka 33 Morocco haikuwa na mahusiano na jumuiya hiyo (tangu OAU mpaka sasa AU) baada ya kujitoa kwa kupinga OAU kuitambua Sahara Magharibi kama Taifa huru na kupewa kiti rasmi ndani ya OAU mwaka 1984.

Uamuzi wa OAU wa kuiruhusu Sahara Magharibi Kuwa mwanachama wa Umoja huo ulitokana na hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (International Court of Justice - ICJ) ya mwaka 1975 iliyopinga madai ya Morocco kuwa ina mahusiano ya kihistoria na kisheria na Sahara Magharibi (na hivyo kuitawala kinguvu) na kutoa haki  ya kujitawala kwa Taifa hilo.

Tunaheshimu maamuzi yale mkutano wa AU wa Januari 2017, ulioirudisha Morocco kwenye AU. Lakini tabia za Taifa hilo onevu bado hazijabadilika, ni muhimu tulieleze bunge masuala yafuatayo ili liweke msimamo wake kwa Serikali juu ya kuminywa kwa watu wa Sahara Magharibi:

1. Kikao cha AU cha Januari 28 - 29, 2018 kiliazimia kuwa Morocco iruhusu Kamati Maalum ya Uangalizi ya AU iende kwenye maeneo ya Sahara Magharibi ambayo inayakalia kimabavu ili kuja kuijulisha AU hali ya mambo ilivyo.

2. Machi 29, 2018 Morocco iliwajulisha UN juu ya kutoruhusu waangalizi wowote wa AU kwenda kwenye maeneo yote ya Sahara Magharibi inayoyakalia.

3. Tangu mwaka 1991 Morocco imetumia mbinu, hila, na uzandiki ili kuzuia Tume ya Umoja wa Mataifa kwaajili ya Kura ya Maoni ya Uhuru wa Sahara Magharibi (MINURSO) kufanya kazi yake kwenye maeneo inayoyakalia kimabavu ya Sahara Magharibi. Siku za karibuni, Umoja wa Mataifa, UN ulipitisha azimio namba 2414 (2018) la kuongeza muda wa mamlaka, uahai na madaraka ya (MINURSO) kwa miezi sita. Morocco imepinga jambo hilo na kutishia kufanya mashambulizi ya kijeshi kwenye maeneo ya Sahara Magharibi ambayo yameshakombolewa (Liberated Zones).

4. Bado Morocco inaendeleza uvunjaji mkubwa wa haki za binaadam kwa watu wote wa Sahara Magharibi wanaodai Uhuru wao.

5. Kurudishwa kwa Morocco kwenye AU kulienda pamoja na Taifa hilo kuridhia ‘AU Constitutive Act’ inayoyataka mataifa ya Afrika kuheshimu maazimio ya AU na hata yale ya UN yanatolewa kwa ushirikiano na AU. Lakini kwa matendo yake tuliyoyaainisha hapo juu ni dhahiri kuwa Morocco haitaki usuluhishi na Sahara Magharibi, bado inataka kuitawala na kuikalia kimabavu, bado Morocco inataka kuendelea kuwa mkoloni. Ndio maana imekataa hata kumpa ushirikiano msuluhishi wa mgogoro huu, ndugu Horst Köhler, Rais wa zamani wa Ujerumani

6. Matendo ya Serikali yetu kwa sasa yanaonyesha hatuna msimamo kwenye mambo ya msingi ya kidiplomasia, namna tulivyoenenda kwenye mahusiano yetu na wanyonge wa Palestina ni mfano hai, sasa tukijali vitu kuliko utu kama ilivyo zamani.

Hivyo basi, nataka kulishawishi Bunge lako litoe muongozo kwa Serikali juu ya kuenenda kwenye hili jambo la Morocco na Sahara Magharibi, ili kuzuia ahadi ya kujengewa Uwanja na Msikiti na Serikali ya Morocco (Vitu) isitufanye tu waache ndugu zetu Wanyonge wa Sahara Magharibi.

Nchi yetu ni kimbilio la Nchi ya Sahara, Serikali yetu chini ya Mwalimu Nyerere ililitambua Taifa la Sahara Magharibi tangu siku za mwanzo kabisa za harakati zao, ndio maana wanao Ubalozi hapa nchini. Kumuenzi baba wa Taifa na kulinda misingi ya Taifa letu ni lazima tusimame na watu wa Sahara Magharibi, na tusiwatupe kama tulivyofanya kwa watu wa Palestina.

Naliomba Bunge liibane Serikali ili itoe ahadi hiyo hapa Bungeni, pamoja na kuitaka Serikali kutumia ushawishi wake kule AU na UN kuibana Morocco iruhusu kura ya maoni ya kuamua mustakabali wa watu wa Sahara Magharibi kama ilivyoridhiwa kwenye Azimio la UN.

Viva Sahara Magharibi
Viva Polisario
Mungu Ibariki Afrika

3. Hakuna Diplomasia Bila Wanadiplomasia: Tuna Uhaba Mkubwa wa Watumishi Kwenye Balozi Zetu

[Sehemu ya Tatu ya Hotuba ya ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto (MB) Juu ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka 2018/19]

Mheshimiwa Spika
Msingi wa tano wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania unatutaka tushirikiane kikamilifu na Nchi, Mashirika pamoja na Taasisi mbalimbali katika nyanja za Diplomasia, Siasa, Uchumi, Utaalam na Teknolojia. Wizara hii ina jukumu la kubuni na kusimami utekelezaji wa misingi yote ya Sera yetu ya Mambo ya Nje.

Pia Wizara hii pia ina jukumu la kusimamia na kuratibu mahusiano kati ya Tanzania na nchi pamoja na mashirika mbalimbali. Utimizaji wa jambo hilo unafanyika kupitia balozi zetu zilizotapakaa kwenye nchi mbalimbali ulimwenguni. Kwa sasa ufanisi wetu ni mkubwa kwa sababu ya uhaba wa watumishi kwenye balozi zetu mbalimbali duniani.

Kwa wastani ukimuondoa Balozi, kila kituo cha Ubalozi wetu nje ya nchi kinapaswa kuwa na Mhasibu, mtu wa TISS na pamoja na Mwanadiplomasia (FSO). Vituo vingi vya balozi zetu havina kabisa Maafisa wa Diplomasia (FSO’s). Wale wachache waliokuwepo awali walirudishwa nchini kwa sababu mbalimbali (ikiwemo kumaliza muda wao wa utumishi Nje ya Nchi). Tumerudisha watu bila kupeleka mbadala wao.

Kwenye balozi zetu mbalimbali watendaji hasa wa kazi za Kibalozi na kidiplomasia ni hawa maafisa wa Diplomasia (FSO’s). Sasa kwa uhaba huu tunawezaje kufanya Diplomasia ya nchi yetu? Hiyo Diplomasia ya Uchumi tunafanyaje bila kuwa na hao Wanadiplomasia?

Nitatoa tu mfano wa balozi zetu chache ulimwenguni. China, nchi ambayo ni mshirika wetu mkubwa kidiplomasia na kiuchumi, hatuna kabisa FSO huko, labda ndio sababu mauzo yetu kwenda China yameshuka mno, maana biashara ya nje ni Diplomasia, sasa wakati Spika unamtaka ndugu yangu Mwijage asafiri, ni nani atakayemuandalia hiyo mikutano ya kupata wawekezaji huko China kama hatuna FSO hata mmoja? Wenzetu Uganda wana FSO’s 8 huko China, Kenya na Sudan wao wanao 9 Kila mmoja.

Nchi nyengine ambayo hatuna kabisa FSO ni Ethiopia - Makao Makuu ya AU, utaona tunavyodharau nafasi yetu katika Afrika. Pia hatuna FSO Afrika Kusini, nchi rafiki na moja ya zenye uchumi mkubwa Afrika, hatuna kabisa FSO Ujerumani - Nchi kubwa zaidi kiuchumi katika Umoja wa Ulaya (EU). Hata India ambako tangu Bunge lianze wabunge tunalalamikia kukosa soko la mbaazi kutoka huko nako hatuna FSO hata mmoja. Tumeufanya kuwa ubalozi wa kupokea wagonjwa tu.

Nchi za Brics (ukiondoa China, India na Afrika Kusini ambazo hatuna kabisa FSO’s) zilizobaki, Brazil na Urusi tuna FSO mmoja mmoja tu. Hata DRC Congo - Nchi ambayo zaidi ya theluthi moja ya mizigo ya Transit inayopita kwenye bandari ya Dar inatoka, nayo tuna FSO mmoja tu tofauti na watatu ilivyozoeleka. Kenya - Nchi ya Afrika Mashariki tunayofanya nayo biashara zaidi nayo ina FSO mmoja tu.

Hali iko hivyo karibu katika balozi zetu nyingi ulimwenguni. FSO’s ndio maafisa hasa waliofundwa na kupikwa kutekeleza Sera yetu ya mambo ya Nje. Foreign Service Officers (FSO’s) ndio diplomats (wanadiplomasia wetu). Kama hawapo vituoni, na hatuwatumii maana yake hatufanyi diplomasia, na kwa kuangalia mbali tunaua diplomasia yetu.

Mimi sitapitisha bajeti hii mpaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa itakaponihakikishia kuwa itapeleka Maafisa wa Diplomasia (FSO’s) katika vituo ambavyo hatuna kabisa na pia kuwaongeza katika vile vituo ambavyo wako wachache.

Tunasimama na Iran na Qatar, Uonevu Dhidi Yao Si Sawa - Tanzania Tusaidie Amani ya Ulimwengu.
Tunasimama na Iran na Qatar - Uonevu Dhidi Yao Si Sawa. Tanzania Tusaidie Amani ya Ulimwengu.

[Sehemu ya Nne na ya Mwisho ya Hotuba ya ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto (MB) Juu ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka 2018/19]

Mheshimiwa Spika
Jambo la mwisho kwenye mchango wangu ni juu ya hali ya ulinzi na usalama duniani. Usiku wa kuamkia Disemba 9, 2017, tulipoteza askari wetu 14 na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa huko DRC Congo, wakiwa kwenye Jeshi la kulinda Amani la Umoja wa Mataifa. Nachukua nafasi hii kuwaombea kwa Mola awalaze pema, pamoja na kutoa pole kwa familia zao na kwa Jeshi zima la JWTZ.

Taifa letu linachangia pakubwa katika kulinda amani ya ulimwengu, wanajeshi wetu wakaiwa karibu katika nchi nane duniani. Naamini tunao wajibu kama Taifa kusaidia uwepo wa amani Ulimwenguni ili kuzuia nchi zilizo kwenye machafuko kama DRC Congo kuongezeka na askari wetu wa kulinda amani kupotea.

Tayari, katika siku za karibuni, dunia imeshughudia maafa makubwa ya vita nchini Libya (ambako Rais Kikwete ni msuluhishi), Iraq, Afghanistan, Somalia, Syria, Sudan Kusini na Yemen. Mwenendo wa migogoro na uonevu unofanyika Qatar na unaotaka kufanyika Iran unapaswa kukemewa mapema ili kuchochea amani ulimwenguni, hasa eneo la mashariki ya kati ambalo tayari limeharibiwa na vita.
Hotuba ya Waziri ya Bajeti ya Wizara hii kwa mwaka 2016/17 ilibeba pongezi kwa nchi za Iran, Marekani, China, Urusi, UN na Umoja wa Ulaya (hasa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani) kwa makubaliano ya Nyuklia ya yaliyoiondolea vikwazo Iran kwa masharti ya kutoendeleza urutubishaji wa nyuklia. Makubaliano yale ni muhimu kwa kuwa iliondoa hali ya mashaka iliyokuwa imetanda duniani.

Tumeona Marekani imejitoa kwenye makubaliano hayo, na kutishia kuweka vikwazo vipya kwa Iran. Huku wajumbe wengine wa wakiendelea kubaki kwa kuwa bado Iran imeendelea kutekeleza makubaliano husika, na kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki, IAEA ni kuwa bado Iran inafuata masharti ya makubaliano husika.

Uamuzi huu wa Marekani si mzuri, unarudisha hali ya mashaka kwenye eneo la mashariki ya kati, ni uonevu dhidi ya Iran, hasa kwa kuwa IAEA imethibitisha kuwa Iran haina makosa. Ni maamuzi ya uonevu tu na usiochochea amani, ni uamuzi unaopaswa kupingwa. Serikali yetu iitumie nafasi yake kule UN kupinga uamuzi huu, na kuitaka Marekani kurudi kwenye makubaliano haya ili kudumisha amani.

Pia Julai 26, 2017 Wizara hii ilitoa taarifa yake juu ya mgogoro wa nchi za Ghuba (GCC), baada ya hatua ya nchi nne za Saudi Arabia, UAE, Bahrain na Misri kuiwekea vikwazo vya anga, bahari na ardhini nchi ya Qatar. Msimamo wa Serikali ni kuunga mkono upatanishi unaongozwa na Amir wa Kuwait, Sheikh Sabah Al-Jaber, tunaunga mkono msimamo huo.

Lakini bado pia sisi ACT Wazalendo tunasimamia tamko letu la kupinga uonevu dhidi ya Qatar tulilolitoa July 24, 2017. Kwa karibu miezi 10 sasa watu wa Qatar wamewekewa vikwazo vya kiuchumi na kiusafiri, kwenye anga, ardhi na bahari na nchi hizo nne jirani, jambo hilo si sawa, hasa kwa kuwa masharti yaliyotolewa ili kuondoa vikwazo hivyo yanaingilia uhuru wa nchi hiyo.
Tunaitaka Serikali yetu, pamoja na kusapoti usuluhishi huu wa Kuwait, itumie nafasi yake pia kule UN kuhakikisha inachangia usuluhishi wa jambo hili ili mashaka yaliyoko na vikwazo kwa Qatar viondoshwe.

Ahsanteni kwa Kunisikiliza. Naomba Kuwasilisha
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge, Kigoma Mjini
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Bungeni Dodoma
Mei 23, 2018

Monday, 21 May 2018


Shajara ya Mwana Mzizima:
HISTORIA NDEFU YA MNAZI MMOJA DAR
Na Alhaji Abdallah Tambaza


ENEO la Mnazi Mmoja hapa jijini, lina historia ndefu pengine kama ilivyo historia ya jiji lenyewe la Dar es Salaam liloanza na Mzizima zaidi ya miaka 150 iliyopita.

Hakuna maelezo sahihi yaliyorekodiwa yanayoelezea hasa ni kwa vipi eneo hilo likaitwa Mnazi Mmoja; lakini itoshe tu kusema kwamba majina kama hayo hupewa maeneo, ama kwa kuwepo kwa mti kama huo mahala hapo huko nyuma; na baadaye, pengine kwa sababu yoyote ile, labda ukakatwa usiwepo tena, lakini jina likawa limebakia.

Aidha, jina hilo pia hutolewa kwa sababu ya harakati za mahala hapo kufanana na zile za ki-mnazi mmoja hivi—liko eneo linaitwa Mnazi Mmoja kule Unguja ambako pirikapirika zake zinalingana na hizi za hapa Dar es Salaam. 

Eneo la Mnazi Mmoja ya Dar es Salaam, kiasilia linaanzia mwanzo wa Barabara ya Lumumba (zamani New Street)/Morogoro Road na kuelekea mpaka mwisho wa Lumumba kule Gerezani; halafu ikutane na Bibi Titi Mohammed, na kuja hadi Morogoro Road tena. Mzunguko huo na vilivyomo ndani yake, hasa vile viwanja, ndio Mnazi Mmoja yenyewe.

Kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja pale barabara ya New Street siku hizo, mikutano mikubwa sana ya kihistoria ilifanyika ambayo ilikuja kubadili historia ya nchi ya Tanganyika wakati huo wa utawala dhalimu wa Serikali ya Malkia Elizabeth wa Ulaya Ingereza.

Iliyokuwa Ofisi ya African Association 1929, TANU 1954
na CCM 1977,New Street (Lumumba Avenue)

Mikutano hiyo ni pamoja na ule mashuhuri ulioitishwa na Chama cha TANU siku hizo kuja kuwaelezea wananchi kusudio la kumpeleka Mwalimu Nyerere Umoja wa Mataifa (UNO), kwenda kulieleza baraza lile kwamba, ‘wakati umefika sasa Watanganyika wanataka uhuru wao ili wajitawale wenyewe’.

Julius Nyerere alienda  UNO na kurejea nchini Machi 19, 1955 na siku iliyofuata Jumapili, Machi 20,1955, TANU ilifanya mkutano mkubwa sana ambao unakisiwa ulihudhuriwa na watu wasiopungua 40,000 waliokuja kutoka pande zote za nchi hii kusikiliza matokeo ya safari ile ya kihistoria, iliyokuja kubadili kabisa taaswira na mtizamo wa Watanganyika kwa nchi yao.

“Mikutano ya mwanzo kabisa ya TANU ya siku za mwanzo ilifanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja mbele ya Princess Hotel. Kwenye jukwaa kubwa lililojengwa kwa miti walikuwa wakikaa wale viongozi wa mstari wa mbele ndani ya TANU, Bibi Titi Mohammed, John Rupia na Clement Mtamila,” anaandika Mohammed Said kwenye kitabu chake mashuhuri cha Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes, ukurasa 191.

Kulia Sheikh Bi. Titi Mohamed, Clement Mtamila, Sheikh Suleiman
Takadir, Julius Nyerere, Mnazi Mmoja, 1955

Mkutano mwengine mkubwa alioufanya Mwalimu Nyerere kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja ni pamoja na ule aliouita kulielezea taifa kutoroka nchini kwa aliyekuwa Waziri wake wa Mambo ya Nje, Oscar Salathiel Kambona. 

Waziri Oscar Kambona, alikimbilia Uingereza baada ya kukosana na Mwalimu Nyerere siku hizo kuhusiana na Azimio la Arusha, ambalo yeye aligoma kuwa muumini wake. Alipopata fununu za kwamba labda angetiwa mbaroni, akakimbilia Kenya na baadaye kuishia London, Uingereza kama mkimbizi wa kisiasa.     

Nyerere, katika mkutano huo, alimshambulia hadharani aliyepata kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Masuala ya Muungano, Abdallah Kassim Hanga, ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa Oscar Kambona, na ambaye wakati huo alihusishwa na masuala ya uhaini kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika mkutano huo, Hanga, ambaye aliletwa kutoka kizuizini Ukonga, alitukanwa na kufokewa kama mtoto mdogo mbele ya kadamnasi ya watu. Baada ya tukio hilo, Hanga hakuonekana tena na hajulikani mahala alipo mpaka leo hii. Kambona yeye alishambuliwa ‘ghaibu’ (hakuwepo alikuwa yuko London akila ‘bata’).

Mama yetu mpendwa Bibi Titi Mohammed, pia alifanya ule mkutano wake mashuhuri wa mwanzo kabisa uliomjenga kisiasa kwenye viwanja hivyo hivyo vya Mnazi Mmoja, pale alipoweza kuwahamasisha wanawake wenzake kujiunga kwa wingi kwenye harakati za ukombozi wa taifa hili. Huo ukawa ndio mwanzo wa safari ndefu ya kisiasa ya Bibi Titi Mohammed, ambaye jina lake lilivuma na kuvuka mipaka mpaka kwenye nchi jirani za Kenya, Uganda, Zambia na Malawi.

Viwanja hivyo pia, vilikuwa maarufu na mahsusi kwa shughuli za kidini hasa ya Kiislamu wakati huo, kwani ndipo mahala ambapo sherehe za Maulid ya Mfungo Sita (mazazi ya Mtume Muhammad SAW) kwa jiji la Dar es Salaam na Mzizima, zilipokuwa zikifanyika na kuhudhuriwa na Gavana mwenyewe.

Pia, sala za Eid zote zote mbili zilikuwa zikisaliwa viwanjani hapo huku misikiti yote ya jijini, ukiacha michache sana, ilikuwa ikifungwa ili watu waweze kujumuika pamoja kwenye sala na sherehe hizo za sikukuu ya Eid.

Sala ya Eid Mnazi Mmoja 2006
Mnazi Mmoja nyuma ni iliyokuja kuwa Titi Street 1966

Sherehe hizo zote zilikuwa zikipangwa na kuratibiwa na kamati maalumu iliyoshirikisha madhehebu zote za dini ya Kiislamu (Sunni, Bohra, Shia, Ibadhi, Ismailia n.k) iliyojulikana kama Maulid Committee na mwenyekiti wake kwa muda mrefu alikuwa Ismailia mmoja aliyeitwa Aziz Khaki. Hakukuwa na Bakwata siku hizo, ambayo kimtazamo inaonekana kama ni ya Waislamu Waafrika au weusi.

Kwa siku za sikukuu ya Eid, viwanja vya Mnazi Mmoja ilikuwa ndipo panapofanyika sherehe zote kwa kuandaliwa mambo mbalimbali ya kufurahisha, hasa kwa watoto kupata burudani ya michezo mbalimbali ya kubembea na vichekesho pamoja na vyakula vyenye kufurahisha nyoyo kama vile sharbati, askirimu, gubiti na mishikaki. Ngoma za asili pia hupigwa hapo kuwaburidisha watu kwa muda wa takriban siku tatu mpaka nne kila jioni. Zile zilikuwa ni siku za kukumbukwa kweli, kwani mambo kama yale sasa hayapo tena sijui yamepotelea wapi.

Sasa kwa siku nyingine za kawaida, viwanja vya Mnazi Mmoja vilikuwa ni kimbilio la wakazi wengi wa hapa mjini kuja kushuhudia mechi mbalimbali za mpira wa miguu zilizokuwa zikichezwa hapo kwa kushirikisha timu mbalimbali za hapa mjini kuwania ama vikombe au kucheza kirafiki tu pamoja.

Mjini hapa siku hizo, ukiacha Sunderland (sasa Simba) na Yanga, kulikuwapo na vilabu vingine maeneo ya Kariakoo, Ilala na Magomeni vilivyokuwa vikitoa burudani tosha kabisa katika medani ya soka kwa wenyeji wa jijini.

Eneo la Gerezani kulikuwa na timu kali sana ikiitwa Victoria, ambapo inapopambana na New Take Time ya Kariakoo, basi huwa patashika kweli kweli. Klabu ya Kahe ya Kariakoo inapomenyana na Rover Fire ya Msimbazi Center pale Ilala, huwa ni kama vile ‘asiye na mwana aeleke jiwe’. Hali kadhalika klabu ya New Port ilipokuwa ikicheza na Young Boys, basi siku hiyo macho yote huelekezwa Mnazi Mmoja au kwa jina jengine viwanja hivyo vikijulikana kama ‘Tua Tugawe’.

Tua Tugawe, ni jina pia la eneo hilo la asili kwa vile pale mbele, ambapo kwa sasa imejengwa ile Shule ya Msingi ya Mnazi Mmoja, kulikuwa na mbuyu mkubwa uliojulikana kwa jina ‘Mbuyu wa Simbamwene’. Simbamwene alikuwa ni mzee mmoja ‘babubabu’ hivi, ambaye kutwa alikuwa akishinda kwenye mbuyu huo. Mara nyingi jijini Dar, mibuyu huwa na majina ya watu. Kwa mfano mbuyu ule uliopo pale St. Peters, Oysterbay, ulikuwa ukiitwa ‘Mbuyu wa Kigwe’, jina la kiasili hilo ambalo limekufa kabisa. Kigwe ni moja ya majina makubwa ya wazawa wa Msasani kule baharini.

Sasa, mahala pale kwenye mbuyu wa Simbamwene kulikuwa na wahuni wakishinda hapo kuwasumbua watu wanaopita njia hiyo kuelekea Kisutu, Stesheni au Gerezani. Kama itatokea wewe mpita njia ukawa umebeba kitu, basi ghafla hukutokea na kukutisha wakikwambia “tuwa hicho ulichonacho tugawe!” Wanyonge wao mara nyingi huwa ni akina mama ambao walikuwa wakiitumia njia hiyo kwenda hospitali ya Sewa Haji iliyokuwapo maeneo ya kule Polisi Kati (Central Police Station) jijini, wakiwa wamebeba chakula kuwapelekea wagonjwa. Kadhia hiyo pia iliwakumba wasafiri kutoka mikoani ambao walikuwa wakitoka Stesheni ya Treni, ambayo haiko mbali na ‘Tua Tugawe.’

Jirani na Tua Tugawe na Mbuyu wa Simbamwene, ndipo ilipoasisiwa Madrassa maarufu jijini ya Maalim Ramadhan Abbas, ambapo wakazi wengi wa asili ya jiji hili walipitia kupata elimu yao ya Dini ya Kiislamu. Madrassa ya Abbasiya, kwa sasa imehamia maeneo ya Kariakoo jirani na Msikiti wa Idrissa. Miongoni mwa wanafunzi mashuhuri ni pamoja na Sheikh Zubeir Yahya wa Msikiti wa Mtoro, Sheikh Ali Azan wa Msasani na hayati Maalim Badi Ali, aliyepata kuwa mchezaji na kocha wa timu ya mpira ya Yanga ya Dar es Salaam.

Sasa, pamoja na mambo yote mazuri hayo yaliyopo eneo la Mnazi Mmoja hapa jijini; Mnazi Mmoja ndipo ilipoasisiwa TAA, TANU na baadaye CCM (chama kikuu cha siasa nchini) ambayo ilikuwa na makao yake makuu pale New Street/Lumumba kabla kuhamia Dodoma.

Mkabala na Ofisi za CCM, inapatikana shule maarufu ya Msingi ya Mnazi Mmoja, iliyojengwa mwaka 1957 kuja kuisaidia shule pekee ya msingi ya Mchikichini kusomesha Waafrika wajue kusoma na kuandika waje kusaidiana na watawala kweye kazi za daraja la chini—hasa hasa kuhesabu magunia na marobota ya bidhaa. Watu wengi walipitia hapo kwa elimu hiyo, akiwamo mwandishi huyu.

Wengine ni pamoja na Balozi Asha Rose Migiro, Alhaji Ramadhani Madabida aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Dar es Salaam, Wendo Mwapachu mfanyabiashara mashuhuri jijini Dar es Salaam na Alhaji Mussa Shaggow Mweka Fedha wa Klabu ya Saigon ya Dar es Salaam.

Historia ya Mnazi Mmoja haikuishia hapo, kwani kule upande wa pili inapatikana hospitali pekee iliyokuwa ikihudumia watu weusi wakati huo wa ukoloni uliogubikwa na ubaguzi wa rangi kwenye kila jambo. Hospitali ya Mnazi Mmoja ilikuwa inatibia magonjwa madogo madogo sana kama homa, kukohoa, kufunga vidonda na labda majipu na mapunye uliokuwa ugonjwa mkubwa kwa watoto majumbani.

Magonjwa mengine ni kichocho na kisonono ambayo yalikuwa yakiwakumba watoto mashuleni kwa sababu sera ya serikali ya kikoloni wakati huo ni kwenda shule ‘pekupeku’ (hakuna ruhusa kuvaa viatu shuleni), hivyo wanafunzi walikuwa wakiambukizana magonjwa hayo kwa sababu ya kukanyaga uchafu vyooni.

Jumba la Sukita na lile la Ushirika pale Lumumba ni majengo yenye historia ya kipekee kabisa kwenye miaka hiyo ya nyuma hasa kabla ya uhuru na mwanzoni mwa miaka ya 1960s mara tulipoanza kujitawala wenyewe.
Jumba la Ushirika Lumumba Avenue

Msomaji, amini usiamini lile Jumba la Ushirika ndilo lilokuwa jumba la kwanza refu hapa Dar es Salam likiyapita majengo yote mengine. Wachoraji ramani na wajenzi walitokea nchini Israel.

Hii inaweza ikawa ni kichekesho kwa watu wengi, lakini ukweli unabakia kwamba jumba lile lilipotangazwa kwamba litafunguliwa rasmi kwa kukamilika ujenzi wake, wakazi wengi walisikika wakilalamika ‘inakuwaje linafunguliwa bila kupigwa rangi nje; hawajui kujenga hao!’ Watu kwa mara ya kwanza tulishuhudia nyumba zikiwa na rangi ile ya cementi nje ili kupunguza vumbi, kwani baada ya jengo hilo likafuatia lile la Kilimanjaro Hotel nalo likafunguliwa bila kupigwa rangi nje. Mambo yakawa yaleyale, ‘ujenzi gani huu, nyumba zinapigwa lipu tu bila rangi!’

Jumba la Sukita, wakati huo likijulikana kama Jengo la Elimu ya Watu Wazima kwenye miaka ya 1960s, ndipo kilipoanzia Chuo Kikuu cha mwanzo Tanganyika kabla majengo ya kule UDSM Mlimani hayajajengwa. Nchi hii, kabla ya kupatikana uhuru hakukuwa na elimu ya shahada inayotolewa. Wazungu kwa miaka yote waliyokaa hapa hilo hawakulitaka litokee, maana shahada huzalisha watu wajanja na werevu ambao wangekuwa hatari kwa utawala wao. Udini na uchifu ndio uliowaibua na kuwapaisha akina Nyerere, Mareale, Fundikira, Kunambi na Kidaha Makwaia; ingawa hawakusomeshwa waje wadai uhuru baadaye.

Kushoto ni Mnazi Mmoja 2010

Msomaji historia ya Mnazi Mmoja ni pana sana kuelezeka kwa kikamilifu. Kwa hiyo naona kwa kumalizia nizungumzie sakata la kutaka kuibadilisha Mnazi Mmoja ili ichukue sura ya mpya ya kupendeza zaidi kulikoanzishwa na serikali ya Nyerere na chama chake cha TANU pale uhuru ulipopatikana.

Kwa nia nzuri tu, Mwalimu na viongozi wenzake waandamizi kwenye ile miaka ya mwanzo ya kujitawala walipanga kujenga jengo kubwa la chama chao cha TANU pale Lumumba; kujenga jengo jipya la Bunge pamoja na majengo mengine ya serikali yasambae kwenye eneo lile la Mnazi Mmoja na mitaa ya jirani.

Mpango huo ulikuwa utekelezwe kwa kuvunjwa nyumba nyingi sana mahala pale ukiwamo na Msikiti maarufu wa Manyema. Walipofuatwa kutakiwa kuvunja msikiti wao kupisha ujenzi mpya, wazee wa Kimanyema jijini waligoma kabisa wakasema wao hawawezi kuvunja nyumba ya Mwenyezi Mungu.

Mazungumzo mbalimbali ya kutaka wabadili msimamo yalishindikana hata pale Mwalimu mwenyewe alipoingilia kati kushawishi jambo hilo. Bado walikataa wakasema labda yeye kama rais wa nchi anaweza kutoa amri hiyo.

Nyerere alikasirika sana kupita kiasi; na hapo ndipo alipoanza mikakati ya kuhamisha kabisa makao makuu ya serikali kuhamia Dodoma. Haikuwa kwa kufuata mji wa katikati wala nini. Alijua Dar es Salaam angepata changamoto nyingi bora akaanze upya mahala pengine kama Dodoma, ambako wakazi wangelipokea kwa mikono miwili jambo hilo. Hivyo ndivyo ilivyokuwa serikali kuhamia Dodoma kwa kinyongo!

Basi tukutane juma lijalo. Alamsiki!
Simu: 0715808864

Sunday, 20 May 2018

ASANTERABI MALIMA:  MTANZANIA ATAKAYEOKOA DUNIA
AUG 21, 2014by RAIA MWEMAin HABARI

Asanterabi Malima


UMEPATA kusikia jina la Dk. Asanterabi Malima?

Jambo moja ambalo wanafunzi waliosoma naye nchini Tanzania hawabishani kuhusu Malima ni ukweli kwamba alikuwa ni mwanafunzi mwenye akili nyingi darasani.

Shafii Dauda ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Azania jijini Dar es Salaam, anamkumbuka Asanterabi kama mwanafunzi mwenye akili aliyefanya vizuri sana katika masomo yake ya kumaliza kidato cha nne.

Shafii, ambaye sasa ni miongoni mwa watangazaji na wachambuzi maarufu wa mchezo wa soka hapa nchini alikuwa kidato cha kwanza wakati Malima alikuwa kidato cha nne.

Akili ile ya Malima imemfikisha nchini Marekani ambako sasa amefanya ugunduzi wa kidude chenye saizi ya pini ndogo (milimita 0.250) kinachoweza kubaini magonjwa ya kuambukiza, kansa na moyo katika hatua ya awali kabisa.

Ugunduzi huu, utakapofika mwisho wake, unaweza kuokoa maisha ya watu wengi duniani. Fikiria tu kwamba unakuwa na kifaa ambacho mojawapo ya magonjwa hayo yakikuanza unaubaini mapema na kwenda kutibiwa. 

Mamilioni ya watu wataokolewa maisha yao na kijana huyu wa Kitanzania.

“Siku zote nimekuwa na ndoto za kugundua kitu ambacho kitaweza kuokoa maisha ya watu. Baba yangu alifariki kwa ugonjwa wa moyo ambao ungegundulika mapema kama kungekuwa na kifaa kama hiki. 

“Kwa sasa sitaweza kuokoa maisha ya baba yangu lakini ninaweza kuokoa maisha ya wazazi au watoto wa watu wengine kutokana na ugunduzi huu nilioufanya. Nafurahi kwamba ndoto yangu imetimia.

“Kansa, baadhi ya magonjwa ya kuambukizwa na magonjwa ya moyo huwa yanachelewa sana kugundulika. Watu wengi hupoteza maisha, na kwa nchi zilizoendelea hutumia pesa nyingi sana kuwatibu waathirika.

“Kifaa nilichogundua ni kidude cha ukubwa wa pini (0.250mm) kinachoweza kupima na kugundua hayo magonjwa mapema. Ili, yaweze kutibika kirahisi, kuokoa maisha na kupunguza gharama,” anasema Asanterabi katika mazungumzo yake na Raia Mwema yaliyofanyika kwa njia ya mtandao juzi Jumatatu.

Asanterabi ni mtoto wa aliyepata kuwa waziri wa fedha wa Tanzania, Profesa Kighoma Ali Malima, aliyefariki dunia Agosti 6, 1995 jijini London, Uingereza, katika mojawapo ya vifo vya kushtusha katika historia ya Tanzania.

Kifaa alichokigundia kijana huyu wa Kitanzania kinafahamika kwa jina la Biolom na ugunduzi huu aliufanya akishirikiana na wanafunzi wenzake wawili wa Chuo Kikuu cha Northeastern kilichopo Boston; Cihan Yilmaz na Jaydev Upponi.

Pamoja na udogo wake, kipini hicho kina jumla ya maeneo manne –yote yenye kazi maalumu, na ubunifu huo tayari umetambuliwa na Serikali ya Marekani. 

Katika mazungumzo yake na vyombo vya habari vya Marekani, Asanterabi alipata kusema kwamba vifaa vingi vya kisasa hubaini magonjwa; kwa mfano kansa, katika wakati ambapo ni vigumu mtu kupata tiba na kupona.

“Kazi yetu hii itakapokamilika, tutaweza kubaini magonjwa haraka zaidi na mapema zaidi na hivyo watu watapata tiba mapema na kuokoa maisha.

“Nchini kwangu (Tanzania), akinamama wengi hufariki dunia kwa sababu ya kuugua ugonjwa wa kansa ya kizazi, kifaa hiki kitaweza kusaidia watu wengi kupona kutoka katika matatizo yao,” alisema.

Kidude hicho ni kidogo sana kwa umbo na namuuliza kama wameamua iwapo mtu anaweza kukinunua na kubaki nacho nyumbani akijitazama mwenyewe au ni lazima aende hospitali.

“Dhamira yetu hapo ni kipimo kitumike mtu akienda hospitali au kliniki (for annual check-up). Lakini japokuwa kinafanya kazi, kupata ruhusa kwa kukiingiza kama pini ni vigumu. Tunafanya vipimo (test) kwa kupima damu iliyotoka kwa mgonjwa,” anasema.

Asanterabi ni zao la mfumo wa masomo wa kawaida uliokuwepo hapa nchini miaka michache iliyopita (kabla ya ujio wa hizi za kata na ‘academy’).

Alisoma katika Shule ya Sekondari ya Tambaza jijini Dar es Salaam kwa mwaka mmoja kabla ya kuhamia Azania.

Miaka 20 iliyopita, hizi zilikuwa ni shule zilizokuwa zikichukua watoto waliofaulu vizuri kimasomo miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi za Mkoa wa Dar es Salaam. 

“Tambaza nilisoma mwaka mmoja tu lakini kutokana na fujo zilizokuwapo nikahamishwa na wazazi na ndipo nikaenda Azania nilikosoma mpaka kumaliza kidato cha nne. Nashukuru kwamba nilifaulu vizuri kwa kupata daraja la kwanza. Kimsingi, nilipata alama A katika masomo yangu yote,” anasema.

Pamoja na muda wote alioutumia Marekani na umaarufu ambao ameupata kama mmoja wa vijana wenye bongo zinazochemka nchini humo, Asanterabi bado hajasahau maisha ya hapa nchini na, hususan, maisha ya shule. 

Kimsingi, Asanterabi anasikitishwa sana na matokeo mabovu ambayo baadhi ya shule alizosoma katika miaka ya nyuma zimekuwa zikiyapata katika miaka ya karibuni.

“Kwa kweli nakumbuka sana walimu wangu. Pale Tambaza, kwa mfano, namkumbuka sana mwalimu mmoja alikuwa anaitwa Mama Msuya, huyu nadhani ndiye alikuwa mwalimu bora kuliko wote pale. Huyu alikuwa anafundisha Jiografia.

“Katika shule ya Azania, namkumbuka sana Mama Shija ambaye naye alikuwa akitufundisha somo la Kemia. Mzizima namkumbuka sana mwalimu mmoja alikuwa anaitwa Thind – best mathematician ever (mwana hisabati bora kuliko wote niliowahi kufundishwa nao).

“Elimu ni sehemu nyingine ambao inanisisimua mno. Nimefuatilia katika tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ( moe.org.tz ) kuwa mwaka 2011, karibu asilimia 50 ya wanafunzi walipata alama sifuri. Tambaza, Forodhani, Kibasila na Azania zilikuwa na watu wenye akili kuliko wote, pengine Tanzania nzima.

“Niko sasa nafanya kazi na vichwa vya bongo huku Marekani tuone tunaweza kufanya nini kutoa mchango kwa "online video learning" (mafunzo kwa njia ya mtandao maana wengi wetu tulisoma bure tu na huo utakuwa sehemu ya mchango wetu kwa Taifa,” anasema.

Kutokana na ubunifu huo alioufanya na wenzake hao, Malima sasa anatakiwa kuanzisha kampuni ambayo itafanya biashara ya ubunifu huo utakaoleta mapinduzi katika sekta ya afya duniani kote. 

Haya ni mabadiliko makubwa katika maisha ya Asanterabi ambaye aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari vya Marekani akisema kwamba siasa iko kwenye damu ya familia yao.

Baba yake alikuwa mwanasiasa na msomi maarufu nchini na kaka wa Asanterabi, Adam, sasa ni Naibu Waziri wa Fedha katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete. Pia ndiye Mbunge wa Jimbo la Mkuranga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

“Kusema kweli mimi sijawahi kujiona kama mjasiriamali (mfanyabiashara). Watu wengi walijua kwamba nitakapokuwa mkubwa nitafuata tu nyayo za wazee wangu. Lakini leo niko hapa.

“Kwenye maisha yangu, sikutaraji kwamba ipo siku nitakuja kufanya ubunifu kama huu. Baada ya kufika hapa nilipofika, sasa naamini kwamba naweza kupiga hatua zaidi,” anasema. 

Ingawa fedha si msukumo mkubwa katika maisha ya Asanterabi, ugunduzi huu unaweza kumfanya kuwa mmoja wa Watanzania matajiri endapo kidude hiki kitaanza kuuzwa.

Hesabu zake ziko hivi. 

“Tunafikiri kitakapokuwa tayari, kidude kimoja kinaweza kuuzwa kwa wastani wa dola moja hivi ya Marekani (Shilingi 1650) kama tukiweza kufanya uzalishaji mkubwa.

“Gharama ya kupimwa inaweza kugharimu kiasi cha kati ya dola 10-15. Mahospitali huwa wanachaji hela nyingi mno kama daktari ndio atafanya vipimo na maamuzi. Ila kama ni nesi gharama si kubwa,” anasema. 

Katika dunia yenye watu zaidi ya bilioni sita, uwezekano wa kuuza pini hizo milioni mia moja kwa mwaka ni mkubwa na kwa kiasi hicho pekee, mauzo ya zaidi ya dola milioni 100 kwa mwaka (zaidi ya shilingi bilioni 165) yanawezekana. 

Asanterabi na wenzake watakuwa na mgawo wao hapo na ifahamike kwa sababu ya sheria kali za hatimiliki nchini Marekani, hizi ni fedha ambazo familia ya wagunduzi watakula hadi kwa wajukuu, vitukuu na kuendelea. 

Safari ya Asanterabi kutoka Tanzania kwenda Marekani haikuwa rahisa namna hiyo. Ikumbukwe kwamba alifiwa na baba yake wakati ndiyo kwanza akiwa na umri wa miaka 15 tu. 

Ni msiba ambao nusura ubadili kabisa maisha ya kijana huyu ambaye baadhi ya wanafunzi waliowahi kusoma naye wanamtambua kwa jina la “Mzaramo wa Chole.” 

Chole ni miongoni mwa mitaa maarufu ya eneo la Oysterbay jijini Dar es Salaam ambako Asanterabi alikulia. Pengine, jina hilo linatokana na ukweli kwamba kuna watu wachache wa kabila la Wazaramo analotoka Malima wanaoishi huko. 

Majina ya namna hii hayakuwa na maana ya ubaguzi wa kikabila lakini ni sehemu ya utani wa kikabila uliokuwa Tanzania wakati huu. 

Utafiti na ubunifu huu wa Asanterabi si habari kubwa hapa Tanzania pekee kwani inaonekana kwamba hata Marekani nako ameanza kutambulika. 

Juni mwaka huu, wakati wa sherehe za maadhimisho ya Wiki ya Afrika katika Jimbo la Massachussets uliko mji wa Boston, Gavana wa Jimbo hilo, Deval Patrick, alimpa Asanterabi tuzo maalumu ya Ujasiriamali akimpongeza kwa ubunifu wake huo utakaosababisha nafuu kwa maisha ya wanadamu na pia ukuaji wa uchumi wa eneo hilo. 

“Si kwamba ugunduzi huu utabadili maisha ya wengi na uchumi kwa wakazi wa Marekani pekee, lakini ugunduzi huu utasaidia sana kuokoa maisha ya mamilioni ya wananchi katika nchi anakotoka Malima ya Tanzania,” alisema Gavana huyo. 

Miaka michache iliyopita, Asanterabi alikuwa akijipanga kuwa mmoja wa waajiriwa katika mojawapo ya kampuni kubwa duniani ya Toshiba, lakini sasa ugunduzi huu umemfanya kujiandaa kuwa mmoja wa viongozi wa kampuni muhimu hapa duniani. 

Pamoja na umbali mkubwa uliopo sasa, baadhi ya watu wanaomfahamu Asanterabi wanamkumbuka kama kijana mpole ambaye hakuharibiwa na ukubwa wa jina la baba yake. 

“Mzaramo wa Chole alikuwa mpole sana kipindi kile anasoma Azania na kwa kweli hakuwa na mambo mengi kama walivyo watoto wengi wa wakubwa,” anasema Mintanga Malulu aliyesoma katika shule hiyo wakati mmoja na Asanterabi. 

Jambo zuri kuhusu Asanterabi ni kwamba ni mzalendo na anayependa nchi yake. Katika mazungumzo yake na Raia Mwema, alisema kwamba kwa namna yoyote ile ugunduzi wake huo utaifaidisha Tanzania. 

Tayari Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (Costech) imetangaza kuvutiwa na mafanikio ya Asanterabi katika nyanja hiyo ya sayansi. 

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Flora Tibazarwa, inasema ingawa utafiti huo bado haujafikia katika hatua ya mwisho, matumaini ni makubwa. 

“Tuna taarifa kuhusu ugunduzi wa Dk. Malima lakini hatuwezi kusema chochote kwa sasa kwa vile bado uko katika hatua za awali na haujapita katika vipimo vyote. Jambo zuri ni kwamba dalili za kufanikiwa ni kubwa,” ilisema taarifa hiyo. 

Ni safari ndefu, ndefu sana kutoka Tanzania hadi Marekani. Lakini, kama mwisho wake ni kama ule wa Asanterabi, safari inakuwa njema.

Wakati tukiagana baada ya kumaliza mazungumzo yetu, bado alionyesha kusikitishwa na matokeo katika shule za sekondari maarufu; Hivi, kuna nini kinatokea huko kwa Azania na Tambaza? 

Sikuwa na majibu. Labda nitapata kama nitafanya utafiti. Labda, itabidi Asanterabi agundue kidude kingine kitakachotoa majibu kuhusu kushuka kwa elimu hapa nchini. 

Swali moja kubwa ambalo nimejiuliza baada ya mazungumzo yangu na Asanterabi ni moja tu; Hivi kweli Taifa hili litakuja kutoa akina Asanterabi wengine katika miaka 20 ijayo  katika mfumo wetu wa elimu tulionao sasa?


Friday, 18 May 2018Balozi Mwapachu akikitambulisha kitabu chake
''Tanzania in the Age of Change and Transfomation''
Mgeni wa Heshima Prof. Mark Mwandosya
Balozi Ali Mchumu


Balozi Juma Mwapachu akitia sahihi yake katika kitabu cha
msomaji Mzee Khamisi Salum

I have been reading Balozi Juma Volta Mwapachu from our early life. Our first encounter was in Tukuyu, former Rungwe District, during the late 1950s.

He came to Tukuyu along with his father, Kibwana Bakari Mwapachu (RIP), one of the first African district officers.

The District Commissioner was Mzee Yessaya Nkata.

Balozi Juma Mwapachu had an early potential for authorship.

At Mpuguso Middle School, he excelled in English debates; challenging peers and seniors alike.

Excellent essay writing skills and discourse, has placed him in good stead to write. 

Talk of life drama, Balozi Mwapachu has always impressed. 

I fondly recall his involvement, along with Cleveland Nkata, Francis Louis and my young brother, Balozi Emmanuel Mwambulukutu, innocent truancy swimming in the forbidden then Rungwe Botanical Garden.

They had to face the cane at the instigation of angry parents, the DC and DO.

This early dramatic life partly helps explain how Balozi Mwapachu morphed into a bona fide author.

The proof of the pudding is in the eating: his latest title: Tanzania in the Age of Transformation is only a sequel to his acclaimed book: ‘’Challenging the Frontiers of African Integration.’’ (November 2012).

These two books, relevant and must reads, ought to read along with his prolific writings. 
Congratulations Balozi Juma Mwapachu.

Ulli K. Mwambulukutu

Monday, 14 May 2018


Shajara ya Mwana Mzizima:
WAJUE WANA SAIGON CLUB WA MZIZIMA
Na Alhaji Abdallah Tambaza

Saigon Khitma  Jumapili 13 May 2018
Raia Mwema 14 - 15 May 2018

JUMA hili, shajara imeonelea ichepuke kidogo kutoka kwenye siasa na kuangalia mambo ya kijamii kidogo ili wasomaji wasichoshwe na historia ya siasa peke yake;   leo tutaangazia habari nyengine kutoka katika jamii tunamoishi.

Vijijini kule tunakotoka, ukitaja neno ‘klabu’ au klabuni, basi moja kwa moja hiyo inamaanisha kwamba umekusudia mahala ambapo watu – wanawake kwa wanaume—watakuwa wamejazana wakinywa ‘mapombe’ yale ya kienyeji yaliyovunda na kutoa harufu mbaya kabisa.

Mijini hali kadhalika, ukisema ‘nakwenda klabu’ maana yake ni kwamba unakusudia klabu cha usiku (Night Club), ili pia ukalewe na, au kukesha huko ukicheza muziki na mambo mengine ya anasa kama kucheza kamari na kuvinjari na warembo wa mjini hapo. Klabu pia inaweza kuwa kama vile klabu za mpira za Simba, Azam na Yanga ili kwenda kujumuika na wapenzi na marafiki mzungumzie masuala ya soka na michezo mengine kama tenisi na gofu (Gymkhana) na Leaders Club (Klabu ya Viongozi pale Barabara ya Ali Hassan Mwinyi), siasa na biashara—basi hakuna zaidi.

Jijini Dar es Salaam, hususan maeneo ya katikati ya Kariakoo, inapatikana klabu moja mashuhuri sana inayojulikana kama Saigon Club, yenye maskani yake pale Mtaa wa Narung’ombe na Livingstone. Ni klabu kongwe ambayo umaarufu wake umezagaa kila pembe, ambapo hakuna mwenyeji wa jiji hili, atasema haijui au hajawahi kuisikia. Saigon kabla ya kuhamia Mtaa wa Narung’ombe na Livingstone ilikuwa Mtaa wa Sikukuu na Narung’ombe.

Madhumuni ya klabu hiyo—‘raison d’etre’— ni tofauti kabisa na vilabu vingine vyote tulivyovizoea katika maisha ya kawaida. Hapo hapachezwi mpira (ingawa wanachama wake labda kwa kiasi fulani ni wapenzi wa mpira), wala mchezo wa aina yoyote ile kama karata, drafti na dhumna. Hii siyo kusema kuwa Saigon haikuwa klabu ya mpira. Saigon ilianza kama klub ya mpira ya watoto wadogo wa shule za msingi na wakakua nayo hadi ukubwani na walipokuwa sasa hawawezi tena kucheza mpira Saigon ikabaki kama barza, mahali wanakutana kwa mazungumzo.

Klabu hii ya kupigiwa mfano au yenye mfano wa kuigwa, ni mahala ambapo watu huenda jioni na kuzungumza mambo mbali mbali ya kijamii na namna ya kuyatafutia ufumbuzi wa haraka kwa mustakabali wa jiji la Dar es Salaam na watu wake.

Orodha ya wanachama wake imekusanya watu kutoka katika kada mbalimbali wakiwamo kwanza hao wanamichezo, wapenzi wa michezo, masheikh, maimamu, walimu wa skuli na madrassa; pamoja na wanasiasa waandamizi wakiwamo mpaka marais, mawaziri, wabunge na madiwani.

Wamo pia wanajeshi la Ulinzi, Polisi, Usalama wa Taifa, Madaktari na wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa mjini Dar es Salaam wa jinsia zote.

Klabu ya Saigon ina madhumuni tofauti na vilabu vyengine na mambo yanayofanyika pale ni aghlabu kuyakuta kwenye vilabu vya kawaida tulivyovielezea hapo awali.

Kwanza, uanachama wake hauangalii umri, jinsia, dini, kabila, itikadi ya vyama vya siasa, cheo, na mambo kama hayo. Utanzania wako ndiyo kigezo kikuu cha kuwa mwanachama ingawa klabu ni ya watu wa Dar es Salaam.

Katika kalenda yake ya mwaka, Klabu ya Saigon huadhimisha mambo makubwa  matatu hivi.Kwanza, ni kuandaa shughuli kubwa siku chache kabla ya kuingia mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kuwaalika watu mashuhuri kuja kujumuika na jamii ya kawaida kuja kuwaombea dua wanachama wa klabu hiyo waliotangulia mbele ya haki, pamoja na wakazi wa jiji hili ambao maisha na matendo yao walipokuwa hai, yaliacha athari na kumbukumbu kwa watu wa jiji hili.

Kushoto Brigadier General Mstaafu Simba Waziri, Mwinyi Mangara
na Boi Risasi katika futari ya mwaka wa 2010
Hao ni pamoja na wasanii wa fani mbalimbali; mashekhe na walimu wakubwa; wazee mashuhuri pamoja na viongozi waliopata kushika nyadhifa mbalimbali jijini Dar es Salaam na kugusa nyoyo za watu.
 
Katikati Abdallah Tambaza mwandishi wa makala hii na kulia
Mussa Shagow na kushoto ni Mwinyikhamis Mwinyimadi

Shughuli hiyo ya khitma, husababisha kufungwa kwa matumizi ya kawaida, barabara yote ya Narung’ombe kuanzia Sikukuu mpaka ile ya Livingstone. Idadi ya wahudhuriaji huwa zaidi ya watu elfu 4000 mpaka 5000. Vyakula vya aina mbalimbali hupikwa kwa wingi sana siku hiyo na vinywaji baridi na matunda hutolewa kwa wageni.

Sherehe hii, ambayo huwa si ya kukosa kuhudhuria kwa wenyeji, hufana sana maana huwa imepangiliwa kwa ustadi mkubwa kuanzia madua na visomo mbalimbali, pamoja na wazungumzaji wa kutoa nasaha zenye mazingatio kwa waalikwa.

Kila mwaka huwa inaushinda mwaka uliotangulia kwa ubora. Huwa ni hadhara ya aina yake iliyojaa vicheko, utani na vitimbi mbalimbali vya Usimba na Uyanga kwa watu kupigana vijembe vya upendo.

Pili, ni kuandaa futari maalumu katika siku moja ya Ramadhani na kufuturisha watu wa jiji hili bila ubaguzi, hata kama mtu hukufunga au si Mwislamu huwa anakaribishwa kujumuika. Kitendo hicho, si tu kinajenga udugu miongoni mwa wanachama, bali hutoa fursa kwa watu mbalimbali kukutana na kula pamoja futari hiyo katika hali ya furaha na upendo.

Daima kwenye futari hizo za kimrima, waandaaji huhakikisha vile vitu vyote vizuri vinakuwamo sahanini, siniani na vyanoni—iwe ndizi mzuzu na mihogo kwa papa; tambi, kaiamati na maandazi; mikate ya kusukuma na ya kumimina; bajia, sambusa na kachori pia huwamo. Uji wa pilipili manga na ‘chai za zatari’ huhanikiza kwa harufu nzuri mahala hapo. Waandaji huweka pia makombe (mabakuli makubwa) ya michuzi ya kuku, maini na mbuzi pia. Vitu huwa vimekamilika kisawasawa vyenye kutamanisha machoni na mdomoni!    

Wazalendo hawa wa Saigon huwa hawaishii hapo, bali pia huandaa sherehe ya usiku mmoja ya kasida za Mtume Muhammad, kwa ajili ya mahujaji wa jijini ambao walibahatika kwenda kufanya Ibada ya Hija na kurejea salama. Hii nayo hupendeza kwelikweli, maana hutoa fursa kwa mahujaji, wakiwa kwenye kanzu zao nzuri zenye kumeremeta, kuja kuelezea waliyoyaona na kuyadiriki walipokuwa kule kwenye miji mitukufu ya Makkah na Madina katika Hijja na Umra kwa kuwaburudisha kwa kasida zinazoimbwa na kughaniwa kwa sauti nyororo.

Hii huwa ni nafasi nzuri kwa wasiobahatika kuwenda Hijja ya kuombewa dua na watu wale watukufu siku za mwanzo kabisa, kwani imesemwa kwamba dua za mahujaji kabla ya siku 40 kwisha huwa mustajaba (hukubaliwa na anayeombwa).

Saigon Sports Club, hapo mwanzoni iliundwa na vijana wadogo wa skuli za Mchikichini na Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, mwaka 1966, ikiwa kama klabu ya mtaani kwa madhumuni ya kucheza mpira na watoto wenzao wa mitaa mingine.

Kwa mujibu wa Alhaji Mussa Mohammed Shaggow, mwanachama mwandamizi, waanzilishi wachache wa mwanzo wa klabu hii wakati huo ikijulikana kama Everton ni pamoja na Mussa Shaggow mwenyewe, Harudiki Kabunju, Yaakub Mbamba, Atika Kombo, Abdu Shiba, Dachi na Salum Khalil akiwa Golikipa wa mwanzo klabuni.


Kulia Atika Kombo, Harudiki Kabunju na Sunday Kayuni
wakijikinga mvua katika khiyma ya mwaka wa 2017

Kushoto Abdu Shiba na Mohamed Said

Timu nyingine za watoto wa mitaani siku hizo hapa Kariakoo, ni pamoja na iliyokuwa jirani yao, Cuba Rovers, New Take Time, New Port (mwandishi huyu alikuwa mwanachama), Dundee, Young Kenya na Young Boys. Zote hizo ziliundwa na vijana wadogo wa umri wa wastani wa miaka 14 wa maeneo ya Kariakoo, ili kutoa ushindani wa kimpira.

Sasa kadri miaka ilivyokuwa inakwenda mbele na vijana wale kuondoka kutoka utoto na kwenda ukubwani, wakabadilisha madhumuni ya klabu yao na kuwa haya sasa ili kudumisha udugu wao pamoja na kuwapokea wanachama wapya wakiwamo wanawake na wazee pia.

Kwa sasa, Saigon mpya yenye malengo mapya na maono mapya, inaongozwa na Mahmoud Mbarak kama Mwenyekiti, akisaidiwa na Juma Abeid ‘Spencer’. Boi Juma ni Katibu wa Klabu akisaidiwa na Mohammed Msitu na Alhaji Mussa Shaggow Mweka Hazina akisaidiana na Abdul Risasi. Kwenye orodha ya wajumbe yumo Muharram Mkamba, Mohammed Tall, R. Sultan na wanawake Hamida Simba na Awena Kitama.

Iddi Simba, mwanasiasa mkongwe na aliyewahi kugombea urais wa nchi hii, kupitia CCM ndiye mlezi wa Saigon ambaye kila mara amekuwa mstari wa mbele kuitetea na kuihami pale inapotaka kutetereka au kwenda kombo, kwani klabu hii ni kioo cha uzalendo uliotutuka kwa kufanya mambo makubwa ambayo wengi wamejaribu kuyaiga lakini wameshindwa vibaya.

Dr. Gharib Bilal akitoa nasaha katika Khitma ya Saigon
Kushoto Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi na mwisho kulia Idd Simba

Wamo pia katika wanachama na wapenzi wakubwa wa Klabu ya Saigon, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu wake Dk. Mohammed Gharib Bilal. Wengine ni Mwanasiasa mashuhuri wa nchi hii hayati Ali Sykes na nduguye Balozi Abbas Sykes pamoja na watoto wao Kleist Sykes (sasa marehemu), Abraham na Ayoub Sykes. Yumo pia Mussa Azzan Zungu, Mbunge wa Ilala, na marehemu Balozi Abdul Cisco Mtiro na ACP Kamanda Mohammed Chico (sasa marehemu).


Kulia Ally Sykes, Sheikh Issa ''Smart Boy'' Ausi, mwisho
kushoto Juma ''Spencer'' Abeid

Kulia marehemu Balozi Cisco Mtiro, Mrehemu Sheikh Hussein, Sheikh
Shomari na Abraham Sykes katika Khitma ya Saigon
   
Mheshimiwa Mussa Zungu katikati akifuturu

Madhumuni mapya ya uwepo wa Klabu hiyo, pamoja na hayo niliyaeleza hapo juu ni pamoja na kusaidiana kwa shida; kufa na kuzikana. Saigon pia imekuwa kimbilio kubwa la wanasiasa wakubwa na wadogo wanaowania nafasi za uongozi katika ngazi mbali mbali hapa nchini ili kupata kuungwa (endorsement).

Hivyo basi kutokana na kuwa na wanachama wa rika na kada mbalimbali inakuwa rahisi kwa mgombea kukubalika jijini kama watu wa Saigon watamridhia na ‘kumpigia debe’ tiketi yake. Hiyo imethibitika mara nyingi na hivyo kuwa na ulazima wa kujitambulisha mapema kwa wana Saigon pale mgombea anapotangaza nia. Cha ajabu ni kwamba, hiyo si kwa wanasiasa peke yao bali hata wale wanaogombea kwenye vilabu vya mpira vya Simba na Yanga na kwenye ofisi za TFF za Taifa—Saigon wana mkono mrefu na nguvu kote huko. Fitna za siasa na mpira wanajua kuzicheza.

Lakini basi pamoja na mafanikio yote hayo mazuri, klabu ya Saigon imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimesababisha kuwepo na makundi mawili hasimu yasiyoiva pamoja. Jitihada mbalimbali zimefanywa kuwarudisha pamoja kwa faida ya watu wa Dar es Salaam, mpaka leo hazijazaa matunda. Hivyo ni jukumu letu kuzidi kumwomba Allah (SWT) aipeperushe fitna hii kwa mbali na amani nzuri irejee pale Saigon ili Dar es Salaam yetu iendelee kustawi. Wahenga walisema; ‘wengi huitwa wale na mmoja huitwa yule!’

Hiyo ndiyo Saigon Club, yenye kuunganisha watu kwa namna ya kipekee ambayo haijapata kufanywa, kuwepo au kutokea mfano wake hapa Tanzania katika huu umri wa miaka 60 wa kujitawala.

Jana tarehe 13 May 2018 Saigon walifanya khitma ambayo juu ya kuwa ilinyesha mvua kubwa wengi walihudhuria.
Alamsiki!
Simu: 0715808864
atambaza@yahoo.com