Sunday, 17 September 2017


Wakati nafanya utafiti wa kitabu cha Abdul Sykes nilikutana na matokeo manne ambayo wananchi walijikusanya na kufanya visomo au dua kujikinga na dhulma za ukoloni wa Waingereza. Katika matukio haya manne ya kumuomba Mungu ni tukio moja tu ndilo wafanyaji kisomo walichobainisha kuwa inayosomwa ni ‘’Halal Badr’’ neno ambalo hivi sasa limekuwa maarufu midomoni mwa watu wengi baada ya kuelezwa kuwa kutasomwa Halal Badr makhsusi kufuatia jaribio la kumuua Mbunge wa Singida Mashariki, Mheshimiwa Tundu Lissu.

Nitarudi nyuma kiasi cha nusu karne na zaidi kuangalia nafasi ya visomo katika kutafuta haki. Nitaaanza kwa kueleza mazingira yaliyokuwapo wakati wa ukoloni hadi kusababisha wananchi kumgeukia Mungu na kutaka msaada wake na hivyo kusoma Halal Badr.

Nakuwekea msomaji wangu yale niliyoandika katika kitabu cha Abdul Sykes, kitabu ambacho ndani yake nimejaribu kueleza historia ya uhuru wa  na kuandika kuhusu Halal Badr ili kwa yule ambae ni mgeni katika mambo haya apate picha kamili na Tanganyika ili uweze kuona ilikuwa na kujua ni wakati gani wananchi waliamua kufanya dua iwe Halal Badr au kisomo kingine kama kinga yao dhidi ya nguvu ambayo wao waliona ni Mungu pekee ndiye angeliweza kuwapa nusra.

Labda tujiulize imekuwaje leo baada ya zaidi ya nusu karne wananchi wanarejea katika mbinu ambazo wengi wanaona kuwa kuzirejea tena katika Tanzaia huru ni kitu ambacho kidogo kinashangaza hasa kwa kuwa dini kama inavyoelezwa kuwa haina nafasi katika uendeshaji wa serikali.

Naanza kwa kukuwekea hapo chini mara yangu ya kwanza nilipokutana na huu makakati ambao kwa hakika ulikuwa mpya katika mbinu za kudai haki kwa kukueleza vuguvugu la makuli katika bandari ya Dar es Salaam pale walipoamua kupambana na dhulma za wakoloni kwa kusoma Halal Badr mwaka wa 1947:

‘’…kidogo kidogo Kleist alianza kumkabidhi Abdulwahid kazi za African Association na mara akawa msaidizi wa baba yake katika siasa za Dar es Salaam. Ilikuwa katika kutimiza haya ndipo Abdulwahid akajikuta anahusika na ule mgogoro wa makuli ulioibuka bandarini Dar es Salaam ambao ulikuwa ukichemka pole pole chini kwa chini kwa muda mrefu tangu kumalizika kwa vita. Hatimaye, Abdulwahid alihusika na harakati za siri za wafanyakazi bandarini ambao, wakiwa wamechoshwa na sheria za kazi za ukandamizaji na wakiwa wamechoka kunyonywa na makampuni ya meli, walikuwa wanapanga kuitisha mgomo.

Chama cha African Association ndicho kiliwakilisha maslahi ya wananchi wa Tanganyika na kimya kimya kiliunga mkono zile harakati za chini kwa chini za wafanyakazi katika kutafuta haki zao. Abdulwahid, kijana mdogo mwenye elimu na akiwa karibu zaidi na uongozi wa African Association kuliko Mwafrika yoyote pale mjini, alichaguliwa kuongoza harakati za tabaka la wafanyakazi zilizokuwa zinaibuka. Haya ndiyo mambo serikali ya kikoloni ilihofia na ndiyo ilikuwa sababu ya kumfanyia khiyana asiingie Makerere. Utawala wa kikoloni ulifahamu kuwa msukumo wa Kleist na mwanae aliyeelimika ungeipa Tanganyika uongozi uliokuwa unakosekana Tanganyika na pengine hata ndani ya Al Jamitul Islamiyya.

Ili kuifanya serikali iwasikilize mahali ambapo hapakuwa na sheria za kazi, ilibidi iwekwe mikakati ambayo ingeifanya serikali iweke sheria hizo katika vitabu vyake. Kamati ndogo ya siri iliundwa na Abdulwahid akatiwa ndani ya kamati hiyo ili kuongoza mgomo uliokusudiwa. Kazi ya kamati hiyo ilikuwa kupanga na kuratibu mikakati ya kuitisha mgomo ambao ungelisaidia katika kuondoa ile dhulma iliyokuwepo. Makuli waliitisha mkutano pembeni kidogo mwa mji, mahali palipokuwa pakijulikana kama ‘’Shamba kwa Mohamed Abeid,’’ katika bonde la Msimbazi. Sehemu hii ilichaguliwa makhususi mbali na macho ya watu ili ipatikane faragha. Makuli walikula kiapo na kusoma, ‘’Ahilil Badr,’’ ili kujikinga na unafiki, usaliti pamoja na shari ya vizabizabina  wangeokataa kugoma. Ubani ulifukizwa na Qur’an ilisomwa. Wakijikinga na kiapo hicho cha mashahidi wa vita vya Badr na huku wakichochewa na ushujaa wa mashahidi waliokufa katika katika  vita vya Badr wakipigana na washirikina wa Makka wakiwa pamoja na Mtume Muhammad (Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu Ziwe Juu Yake), makuli walichagua tarehe 6 Septemba, 1947 kuwa ndiyo siku ya kuanza  mgomo wao.

Mapema asubuhi moja kile kilichoanza kama mipango ya siri dhidi ya  makampuni ya Wazungu bandarini, kililipuka na kuwa mapambano ya dhahiri. Watu katika mitaa jirani ya alipoishi akikaa Abdulwahid walikuwa hawajatoka vitandani mwao alifanjiri moja waliposikia vishindo na makelele vimetanda mtaani. Makuli, baadhi yao wakiwa vidari wazi, walikuwa wameizingira nyumba ya Kleist, wakipiga makelele wakimtaka Abdulwahid atoke nje. Makuli wale walipiga kwata njia nzima kutoka bandarini huku wakitoa maneno ya kupinga ukoloni na  wakiimba kupandisha morali zao. Tukio hili halikuwa na kifani. Ilikuwa ni mara ya kwanza nchini Tanganyika kwa wananchi kushuhudia katika mitaa ya Dar es Salaam uasi wa dhahiri kama huo dhidi ya serikali ya kikoloni. Abdulwahid, wakati ule kijana mdogo kabisa, akichungulia kupitia dirisha la chumba chake alichokuwa amelala, alishangazwa kuona umati mkubwa wa watu nje ya nyumba yao. Aliweza kuwatambua baadhi ya wenzake katika kamati ile ya siri iliyokuwa inapanga mipango ya mgomo. Alipotoka nje kuonana nao makuli wenye hasira walimfahamisha kuwa mgomo ulikuwa umeanza na wasingerudi kazini hadi madai yao yote yamekubaliwa…’’

Kisomo kingine nilichokutana nacho wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika kilifanyika Lindi na kisomo hiki kilifanywa na Sheikh Yusuf Badi lakini kwa kauli ya mpashaji habari wangu kisomo hiki kilikuwa Tawasul na katika waliohudhuria kwa kutajiwa majina yao walikuwa Suleiman Masudi Mnonji na  Bi. Sharifa bint Mzee:

Bi. Shariffa Bint Mzee

‘’Nyerere aliporudi Lindi mwaka 1959, TANU ilikuwa ina nguvu sana na ilikuwa imekumba kila mtu. Wale watumishi wa serikali wengi wao wakiwa Wakristo, walio kuwa wakiibeza  TANU mwaka 1955 kwa sababu ilikuwa ikiongozwa na Waislam ëwasiokuwa na elimu,í ukweli ulikuwa umewadhihirikia na sasa walikuwa wakionyesha heshima kwa chama. Hawakuwa na khiyari na ilibidi waonyeshe heshima kwa sababu bwana mwenyewe, yaani serikali ya kikoloni, ilikuwa na heshima kwa TANU. Serikali ilikuwa imetambua kuwa dhamiri ya watu ya kukataa kutawaliwa haiwezi tena kupuuzwa. Nyerere alikuwa amelihutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa mara mbili, mara ya pili ikiwa mwaka 1957. Ujumbe wa TANU ulikuwa wazi, watu wa Tanganyika walikuwa tayari kujitawala. Kila siku zilivyopita ndivyo TANU ilivyopata nguvu. Rashidi Salum Mpunga, dereva wa lori, aliweza kumshawishi na akafanikiwa kumuingiza TANU mmoja wa masheikh wenye kuheshimiwa sana mjini Lindi na mshairi maarufu, Sheikh Mohamed bin Yusuf Badi. Sheikh Badi alipoingia TANU kwa ajili ya heshima yake na kukubalika na watu, idadi kubwa ya Waislam walimfuata na kukata kadi za TANU. Nyerere alipokuja Lindi kujadili tatizo la kura tatu na uongozi wa Jimbo la Kusini, Sheikh Yusufu Badi alimpokea Nyerere na madras yake, wanafunzi wakimwimbia Nyerere kasda na kumpigia dufu. Kuanzia hapo sasa kila mtu alijiunga na TANU. Si Mponda wala Kanisa lilikuwa na uwezo wa kupambana na TANU kwa wakati ule. Polepole lakini na kwa kwa uhakika, TANU ilingia ndani ya maeneo ya Kikristo huko Songea, Masasi, Tunduru na Newala, nyumbani kwa Yustino  Mponda.
  
Lakini matukio mawili ya kumbukumbu kubwa yalikuwa katika safari ya pili ya Nyerere alipozuru tena Jimbo la Kusini. Kumbukumbu ya kwanza ilikuwa tawaswil aliyosomewa Nyerere na Sheikh Yusuf Badi mwenyewe pamoja na Waislam aliowachagua yeye sheikh mwenyewe maalum kwa hafla hiyo, pamoja na waliochaguliwa na masheikh wengine.’’

Kisomo kingine na hiki ndicho maarufu ni kile kilichofanywa nyumbani kwa Jumbe Tambaza Upanga ambacho Mwalimu Nyerere mwenyewe amekieleza.

Kisomo cha nne kilifanyika Mnyanjani, Tanga mwaka wa 1958 wakati TANU ilipokuwa inakabiliwa na tatizo la Kura Tatu:

‘’Siku kadhaa kabla ya kusafiri kwenda Tabora kwenye ule mkutano mkuu wa mwaka wa TANU, Nyerere na Amos Kissenge, Kaimu Katibu Mwenezi wa TANU, walisafiri kwenda Tanga kushauriana na uongozi wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU Tanga kuhusu matatizo yaliyoletwa na Uchaguzi wa Kura Tatu. Mkutano huu baina ya Nyerere, Kissenge na ule uongozi wa Tanga ulikuwa wa siri sana. Tanga iliwakilishwa na Hamisi Heri, Mwalimu Kihere, Abdallah Rashid Sembe, Ngíanzi Mohamed, Mustafa Shauri na Abdallah Makatta. Nyerere alizungumza waziwazi na kwa ithibati ya moyo wake. Nyerere alikiambia kikao kile kuwa amekuja Tanga kuomba wamuunge mkono kwa sababu ilikuwa ni matakwa yake TANU lazima ishiriki katika ule uchaguzi wa kura tatu uliokuwa unakaribia hata masharti yakiwaje. Nyerere aliuambia uongozi wa Tanga uliokuwa ukimsikiliza kwa makini kuwa alikuwa amekuja kwao kwa sababu watu wa Tanga wanajulikana kwa ufasaha wa lugha na kwa uwezo wao wa kuzungumza vizuri. Nyerere alisema angehitaji hiki kipaji adimu cha watu wa Tanga kuunga mkono msimamo wake huko Tabora. Nyerere alitoa hoja kwamba TANU lazima iingie katika uchaguzi kwa sababu kuususia ni sawasawa na kukipa chama hasimu, UTP ushindi bila jasho kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria. TANU ingedhoofika na hivyo ingekosa sauti katika maamuzi yatakayotolewa na serikali katika  siku zijazo.

Sheiikh Abdallah Rashid Sembe

Kufichuka kwa msimamo wa Nyerere wa kutaka TANU iingie kaatika kura tatu kulishtua uongozi wa Tanga. Majadiliano makali yalifuata uongozi wa Tanga ukionyesha upinzani wao kwa msimamo wa Nyerere. Baada ya majadiliano ya muda mrefu Nyerere alifanikiwa kuwashawishi wote wawili, Hamisi Heri na Mwalimu Kihere ambao ndiyo walikuwa wapinzani wakubwa wa msimamo wa Nyerere na uchaguzi wa kura tatu. Nyerere aliutahadharisha uongozi wa Tanga kuwa agenda ya kura tatu itakapokuja anatabiri kupata upinzani mkali kutoka katika majimbo. Huko Tanga kwenyewe, TANU ilikuwa ikikabiliwa na upinzani mkali kutoka UTP na serikali. Matawi kadhaa yalikuwa yamepigwa marufuku.   UTP ilikuwa na nguvu Tanga kwa sababu wanachama wake wengi walikuwa wakimiliki mashamba ya mkonge katika jimbo hilo. Kwa ajili hii chama kilikuwa kinaelemewa na mashambulizi kutoka wa wapinzani. Wakati huo Tanga ilikuwa imetoa viongozi wenye uwezo lakini wote walikuwa wamehamishiwa makao makuu mjini Dar es Salaam. Wapangaji mikakati wazuri kama Peter Mhando alikuwa amehamishiwa Dar es Salaam na kutoka hapo alipelekwa Tabora ambako si muda mrefu akafa. Elias Kissenge vilevile alihamishiwa makao makuu kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa TANU baada ya Oscar Kambona aliyekuwa ameshika nafasi hiyo kwenda Uingereza kwa ajili ya masomo. Uongozi wa TANU Tanga hata baada ya kujadili mbinu waliyopanga na huku Nyerere akielekeza mikakati ambayo Mwalimu Kihere na Abdallah Rashid Sembe wataitekeleza Tabora, bado uongozi ule ulikuwa na wasiwasi wa mafanikio ya mpango huo. Kwa ajili ya wasiwasi huu, viongozi wa TANU wa Tanga walimuomba Nyerere wawe pamoja ili ifanywe tawaswil waombe msaada wa Allah awape ushindi dhidi yaa vitimbi vya Waingereza. 

Maili tatu kutoka Tanga kipo kijiji cha Mnyanjani ambako kulikuwako na tawi la TANU lililokuwa na nguvu sana likiongozwa na Mmaka Omari kama mwenyekiti na Akida Boramimi bin Dai akiwa katibu. Mmaka alikuwa kijana aliyekuwa akiendesha mgahawa pale kijijini na Akida bin Dai alikuwa mwashi. Akida aliongoza tawi la vijana wa TANU ambalo baadae lilikuja kujulikana kama Tanga Volunteer Corps (TVC). TVC ilikuwa sawasawa na Bantu Group, ambayo wakati huo ilikuwa imekwishaanzishwa huko Dar es Salaam na Tabora. Vikundi hivi mbali na kufanya shughuli za propaganda na kuhamasisha wananchi halikadhalika viliifanyia TANU ujasusi. Nyerere na Kissenge walichukuliwa hadi Mnyanjani na tawaswil ikasomwa. Waliohudhuria kisomo hicho  walikuwa Abdallah Rashid Sembe, Sheikh Dhikr bin Said, Mzee Zonga, Hemed Anzwan, Salehe Kibwana aliyekuwa mshairi maarufu, Akida Boramimi bin Dai na Mmaka Omari. Aliyechaguliwa kusoma Quran Tukufu alikuwa mjomba wa Mwalimu Kihere, Sheikh Ali Kombora…’’


Mwalimu Kihere

Kipo kisomo kilifanywa na wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo mwaka wa 1954/55 wakimnuia Town Clerk Mwingereza ambae alikuja Kariakoo Market kukamata kadi za TANU ambazo Abdul Sykes alikuwa kaziweka ofisini kwake na akiziuza pale sokoni. Ilikuwa Abdul apoteze kazi yake kama Market Master. 

Wazee wa pale sokoni walisoma Halal Badr. 
In Shaa Allah iko siku nitakieleza hiki kisa.

Shariff Abdallah Attas na Mzee Kisaka waliokuwa wakifanya kazi chini ya Abdul Sykes walikifahamu vizuri kia hiki.

Wednesday, 13 September 2017


TAAZIA: DR. BUYUNI JAHAZIDr. Jahazi amefariki mchana huu leo tarehe 13 September, 2017.
Kwake tumetoka na Kwake ni marejeo yetu.

Iko siku mwaka wa 1993 na ulikuwa mwezi wa Ramadhani nilikuwa nasafIri na ndege ya Air Tanzania Corporation (ATC) kuelekea Harare kwenye kozi ya Masoko ya Huduma yaani, ‘’Marketing of Services.’’ Wakati ule nilikuwa nikifanya kazi Bandarini Idara ya Masoko.

Ndege ilikuwa ya alfajir na kwa bahati nzuri Dr. Jahazi na yeye alikuwa anasafiri na ndege hiyo hiyo kuelekea Harare kwenye mkutano wa Madaktari. Wakati ule Dr. Jahazi alikuwa akisomesha pale Muhimbili Faculty of Medicine.

Basi nikamkuta Dr. Jahazi pale uwanjani amesimama anasubiri ATC wafungue ‘’desk,’’ lao abiria waanze mchakato wa ku -‘’check in,’’ abiria ili wapatiwe, ‘’boarding pass,’’ waelekee, ‘’departure lounge,’’ na kuingia katika ndege tayari kuwa kuruka.

Dr. Jahazi alikuwa amevaa kanzu nyeupe na amepiga kilemba cha tabligh.

Ukitamtazama picha ya haraka itakayokujia ni kuwa huyo ni sheikh wa tabligh siyo Mhadhiri wa Chuo Kikuu.

Siku zile ilikuwa hakuna, ‘’security check,’’ kama hizi za siku hizi za kupitisha watu na mizigo katika, ‘’metal detector,’’ ambazo kwa sasa ziko kila mahali kuanzia viwanja vya ndege hadi katika mahoteli makubwa.

Wakati nasalimiana na Dr. Jahazi tukiubiri ATC wafungue, mara akatokea Balozi Ami Mpungwe wakati ule akifanyakazi Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje kama Balozi na Mkurugenzi wa Afrika na Mashariki ya Kati.

Ami akaja pale tulipokuwa tumesimama na akatusalimu.

Dr. Jahazi akamuuliza kama na yeye ni msafiri. Ami akajibu akasema yeye amekuja kuwasindikiza wageni wa serikali na alikuwa kawaingiza VIP Lounge na alikuwa anaondoka ndipo alipotuona akaona aje atusalimu.

Dr. Jahazi akamfahamisha Ami kuwa sisi tulikuwa tunakwenda Harare.

Dr. Jahazi alikuwa mkononi ameshika, ‘’briefcase,’’ na katika ile, ‘’briefcase,’’ alikuwa amefunga kidumu cha lita tano chenye maji.

Ami akawa kashangazwa na kile kidumu cha maji, akamuuliza Dr. Jahazi, ‘’Dr. haya maji ya nini?’’

Dr. Jahazi akajibu akasema, ‘’Haya maji natembea nayo kwa ajili ya kuchukua udhu isije wakati wa sala umeingia na mimi sina maji ya kutawadha.’’

Jibu lili lilimtosheleza Ami hata na mie pia kwani nami nilikuwa najiuliza yale maji yalikuwa ya nini ila tu sikupata fahamu ya kuuliza.

Ndani ya ndege tulikaa pamoja na ilikuwa safari nzuri sana kwangu.

Dr. Jahazi aliniwaidhi kuhusu utukufu wa Allah na Mtume Wake na akaniambia kuwa endapo nitaishika kamba ya Allah nitafanikiwa hapa duniani na akhera.

Siku ile tukiwa angani tukielekea Zimbabwe ndiyo kwa mara yangu ya kwanza nilipolisikia jina la Prince Badru Kakunguru wa Uganda.

Dr. Jahazi alipobaini kuwa mimi sikuwa namjua Prince Badru Kakunguru alianza kunieleza historia ya Uislam Uganda na vipi Prince Badru Kakunguru alivyofanya juhudi katika kuuepeleka Uislam mbele Uganda.

Nilishangaa sana kwani sikujua kuwa Dr. Jahazi juu ya kuwa Bingwa wa Micro Bio-Chemistry Uganga wenyewe alikuwa pia ni mjuzi wa historia.

Niliona safari ni fupi sana katika ya Dar na Harare.

Mimi nilikuwa sijafika Harare lakini yeye Dr. Jahazi alinifahamisha kuwa alikuwa akienda huko mara nyingi kwa shughuli za mikutano na makangamano ya kitaaluma.

Basi nikamuomba Dr. Jahazi anifahamishe hoteli nzuri ya mimi kwenda kukaa.

Ilikuwa kozi ya takriban mwezi mzima na nilitaka nikae mahali pazuri.

Dr. Jahazi alinitazama usoni akaniambia, ‘’Sikiliza mdogo wangu Mohamed, mimi sikai hoteli, mimi nalala msikitini.’’

Ukweli ni kuwa nilishtuka na kushangaa sana.

Juu ya mshtuko wangu sikusema kitu nilinyamaza kimya.

Wakati tunatoka nje ya uwanja wa ndege wa Harare mie nikawa nimemganda Dr. Jahazi niko ubavuni kwake. Mara tu tulipokuwa tushapita, ‘’Customs,’’ kundi la vijana wa kila rangi nikaona wamemvamia Dr. Jahazi wakimpokea mizigo yake na kutokana na mazungumzo yao nikajua hawa ni madaktari wanataaluma wanzake.

Ghafla Dr. Jahazi akawa kageuka si yule aliyekuwa na mimi ndani ya ndege. Hapa alikuwa Dr. Jahazi ‘’Lecturer,’’ yuko darasani anasomesha.

Mara atamjibu huyu hiki mara atamjibu huyu kile kwa Kiingereza kilichonyooka kisawasawa. Hakika wale jamaa ilionyesha walikuwa wanamuusudu Dr. Jahazi na walikuwa wamengoja kwa hamu.

Yalikuyokuwa yanazunguzwa pale mie sikuambulia hata moja.

Baada ya kutulia tukaingia katika gari kuelekea mjini na akanambia kuwa atanipeleka Ambassador Hotel iko katikati ya mji na akamwambia dereva apite barabara fulani ili anionyeshe msikiti nitakaokuja kuswali tarweh.

Nakumbuka kichekesho kimoja.

Dr. Jahazi aliposema neno, ‘’mosque,’’ yule dereva akawa hajui lina maana gani.

Dr. Jahazi alipomfahamisha dereva kuwa ni ‘’msikiti,’’ yule bwana akajibu akasema, ‘’Oh! You mean Muslim church.’’

Dr. Jahazi alikuwa rafiki kipenzi wa kaka yangu Prof. Mgone toka wote wakiwa wanafunzi pale Muhimbili na nilikuwa nafurahishwa na kitu kimoja kila tunapokutana.

Ingawa sasa mimi ni mtu mzima lakini yeye hakuacha kuniangalia mimi kama, ‘’bwana mdogo,’’ wake na katika mazunguzo yetu siku zote hiki kikijitokeza na mimi nilikuwa siachi kutanguliza, ‘’kaka,’’ kila ninapozungumza na yeye.

Miezi michache iliyopita tulikuwa sote tukaachana Msikiti wa Shadhly baada ya kuzungumza njia nzima.

Mwaka wa 2002 Tanzania ilipopitisha Sheria ya Ugaidi, Dr. Jahazi alivamiwa nyumbani kwake na kutiwa nguvuni kwa kushukiwa kuwa ni gaidi. Wapelelezi walipekuea nyumba yake chini juu juu chini kutafuta ushahidi wa ugaidi lakini walichokutananacho katika nyumba na maktaba yake ni mavolumu na mavolumu ya majarida na mabuku na mabuku ya taaluma yake ya udaktari.

Kosa lake Dr. Jahazi ilikuwa ni yake mapenzi yake katika dini yake na kuenzi kivazi chake cha kanzu na kilemba hata anapokuwa darasani Chuo Kikuu Muhimbili akihadhiri.

Allah ampe kaka yangu Dr. Jahazi kauli thabit na amweke mahali pema peponi.

Amin.

Jeneza likitoka Msikiti wa Shadhly

Maziko ya Dr. Jahazi Makaburi ya Kisutu
Tuesday, 5 September 2017Rijal Hamzah: Shukran. Hollingsworth huyu ni Father of Education, Zanzibar lakini watawala hata kumzungumza hawataki, au hawajui au hawapendi siwezi kufahamu.

Alipoanzisha Journal la Mazungumzo ya Walimu alikuwa Editor, kisha Sheikh Abdalla Saleh Farsy kati ya wanafunzi wake akaja kuwa Editor. Hollingsworth akifanya Tuition kwa wanafunzi wake na kutomtoza hata Cent mwanafunzi. Wanasema alikuwa anaamini kila mwanafunzi anafahamu ila tu wanapishana katika ufahamu, ndio lile bench la mwanzo kwenda Makerere ilikuwa ni product yake na walionyesha kishindo kikubwa kilichomshtua Director wa Education hapo Makerere.

Baadhi ya hao waliokuwemo katika hio picha wanakuja kuwa walimu wazuri watu kama Maalim Ibrahim Kassim aliokuja kuwa bingwa wa Arithmetic. Utakuta kuna mchanganyiko wa wanafunzi hapo mtu kama Sheikh Hassan Sheikh, Sheikh Abdalla Saleh Farsy, Saleh Mbamba.

Dr. Said Mahfoudh ni daktari wa mwanzo mzalendo na yupo hapo Dr. Said Aboud, maina hayo yalivuma sana wakiwa ndio madaktari wazalendo, hakuna asiomjua Maalim Amour Ali Ameir anakuja kuwa Director wa mwanzo mzalendo, alikuwa na command  kubwa ya Kiengereza na Kiarabu na kabla ya kuhajiri Zanzibar, alipokuja ziara Rais wa Misri Jamal Abdele Naseer yeye alikuwa ndio Mkalimani katika Mkutano wa hadhara uliofanywa Syd Khalifa Hall ilipo TVZ sasa ZBC.

Mohamed Said Jinja anatarekhe kubwa na anaweza kuandikwa kitabu kizima, katika vijana wa wakati huo waliokwenda England kusoma, wanasema uwezo wake wa Kiengereza ulikuwa hauna kifani na hata akizungumza kama hujamuona utasema aliokuwemo huko ndani anazungumza ni Muiengereza.

Bahati nzuri taarifa zao baadhi yao ni rahisi kuweza kuzipata pale Archives. Tutoe Shukurani alioivumbua hii picha na shuurani kwa aliojitahidi kuweka majina yalioweza kupatikana. Nakumbuka wazee wakipenda kutoa credit kwa wenzao kwa yale waliokuwa nayo na ndio kina sisi kwa mbali tumepata kuwajua. Wengi wao wengekuwa hai wangekuwa na age ya miaka mia na, kwani Syd Omar bin Abdalla Mwinyi Baraka mwakani ataadhimishwa kufikia umri wa miaka 100. 

Baada ya hapa sina tena la kuongeza tuwape wengine nafasi watuelimishe.

Mwinyi Baraka  katika Darsa yake mmoja nikiwa nimehudhuria alimzungumza Hollingsworth namna alivyokuwa na hima ya kusomesha, akaazimia akenda England akamzuru na akabahatika kufika alipokaa, alistaajabu Mwinyi alipogonga akichungulia akikaa ground floor hapo hapo alisema kwa Kiswahili ''Mwiny nani kakuongoza kufika hapa, faraja kwangu, ingaw aupweke umenizunguka bada ya kufiwa na mke wangu'' Mwinyi anasema alilia kumsikia mwalimu wake namna anavyozungumza na neno Upweke kulitumia, leo katika lugha yetu inayobatizwa kila kukicha ni nadra kumsikia mtu anatumia neno Upweke.  

Thursday, 31 August 2017

Mzee Mshume Kiyate na Baba wa Taifa, 1964

Jina la Mshume Kiyate kwa sasa si geni tena katika historia ya TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.

Mzee Mshume alikuwa katika Baraza la Wazee wa TANU kuanzia lilipoundwa 1955.

Mshume Kiyate alikuwa kiishi Mtaa wa Tandamti na akifanya biashara Soko la Kariakoo toka miaka ya 1950. Yeye ndiye aliyekuwa dalali wa samaki wote walioletwa pale sokoni. Kazi hii ilimtajirisha kwa kiwango cha nyakati zile na yeye alitumia fedha zake nyingi katika harakati za kuijenga TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.

Kubwa ambalo lilimpambanua Mzee Mshume katika historia ya uhuru ni kule yeye kujitolea kubeba jukumu la chakula cha nyumba ya Baba wa Taifa kuanzia miaka ya mwanzo ya TANU hadi uhuru unapatikana mwaka wa 1961 na kuendelea kufanya hivyo hata pale Baba wa Taifa alipomwambia, ‘’Mzee Mshume sasa basi hivi vikapu vyako vya chakula, mimi sasa nalishwa na serikali.’’

Jibu la Mzee Mshume lilikuwa, ‘’Hapana Mheshimiwa sitoacha kuleta chakuka nyumbani kwako kwani nataka wewe na watoto wako ule chakula hiki na hicho cha serikali wape wageni wako.’’

Huyu ndiye mzalendo mpigania uhuru wa Tanganyika na rafiki kipenzi cha Baba wa Taifa, Mzee Mshume Kiyate.

Miaka takriban 20 iliyopita aliyekuwa Meya wa Jiji ;a Dar es Salaam marehemu Kitwana Selamani Kondo katika kutambua mchango wa Mzee Mshume Kiyate alibadili jina la Mtaa wa Tandamti kuwa, ‘’Mtaa wa Mshume Kiyate.’’
Hadi hivi ninavyoandika na nimepita mtaa huu leo nimekuta kibao kipya kimewekwa lakini jina ni lile lile la zamani.


Hii nini maana yake?
Dharau, khiyana au nini? Picha hiyo hapo juu ilipigwa mwaka wa 1964 baada ya maasi ya wanajeshi na Baba wa Taifa kurejeshwa madarakani na Jeshi la Waingereza. TANU ilifanya mkutano mkubwa sana Jangwani na Mzee Mshume Kiyate siku ile alimvisha Baba wa Taifa kitambi kama ishara ya kuonyesha kuwa Wazee wa Dar es Salaam wale waliompokea na kuwa na yeye bega kwa bega kupigania uhuru wa Tanganyika bado wako nyuma yake na wanamuunga mkono. 

Huyu ndiye Mzee Mshume Kiyate.


Waliosimama wa pili kulia ni Mzee Mshume Kiyate
Mshume Kiyate wa kwanza kulia aliyemshika mkono Baba wa Taifa na
pembeni kwa Baba wa Taifa ni Mzee Max Mbwana akifuatiwa na Mzee
Mwinjuma Mwinyikambi
Kuna picha mashuhuri ya Mzee Mshume na Baba wa Taifa iliyopigwa Novemba 1962 wakati wa Uchaguzi Mkuu. 

Picha hiyo inamuonesha Mzee Mshume akiwa amevaa koti, kanzu na kofia amemshika Baba wa Taifa mkono akimsindikiza kupiga kura. 

Karika utawala wa Baba wa Taifa, magazeti ya ''Uhuru'' na ''Daily News,'' yamekuwa yakiitumia picha hii kila baada ya miaka mitano katika uchaguzi wa rais kama njia ya kuwahamasisha watu kupiga kura na kumchagua Baba wa Taifa. 

Friday, 18 August 2017


Bi. Mgaya Nyang'ombe


Yericko,
Kwa kuwa umependa kumbukumbu hizi za nyumbani kwetu Gerezani basi
nataka nikupe kisa kilicholeta taharuki kubwa ambayo naelezwa haijapata
kutokea katika historia ya TANU na Nyerere labda hadi Baba wa Taifa
anaaga dunia.

Siku za mwanzo za TANU viongozi wake walikuwa wakiwa na jambo zito
la kujadili walikuwa wakikutana nyumbani kwa Abdul Sykes Mtaa wa
Stanley na Sikukuu.

Walikuwa wakimaliza shughuli basi inakuwa chakula na vinywaji kujipongeza.
Siku hiyo baada ya kikao wakala chakula cha mchana.

Baada ya kula ghafla Nyerere akaanza kulalamika kuwa tumbo linamkata.
Nyerere akawa anajipindua huku na huku kwa maumivu.

Siku zote TANU walikuwa wakiishi chini ya hofu ya Nyerere kudhuriwa na
maadui wa TANU lakini katika chakula kile cha nyumbani kwake hapakuwa
na hofu kwani chakula chake kilikuwa kinatoka Kariakoo na kwa watu maalum
ambao Market Master, Abdul Sykes akiwafahamu na Mzee Mshume na ndiye
akikinunua, mpelekaji wa chakula hicho kwa Mama Maria alikuwa dereva wa
TANU, Said Kamtawa maarufu kwa jina Said TANU.

Nyerere kalala kwenye kochi anaugulia na taharuki ikazuka na minong'ono
haikuweza kukwepeka.

Nyerere kalishwa sumu!
Sumu Nyerere alishwe nyumbani kwa Abdul Sykes?
Uani jikoni walikuwa mama yake Nyerere Bi. Mgaya, Mama Maria, mama
yake Abdul Sykes Bi. Mruguru bint Mussa, 
mkewe Abdul Sykes, Mama
Daisy
.

Bi. Mgaya 
hakuweza kustahamili alipoona wanaume ingia toka kule ndani.

Aliposikia kuwa Nyerere anaumwa baada ya kula chakula kitu cha kwanza
kilichomjia ni kuwa mwanae kalishwa sumu akawa sasa mikono kichwani
analia na kutembea ua mzima.

Bi. Mgaya anasema Kizanaki na anachanganya na Kiswahili.
Ikawa patashika kumtuliza.

Wote waliokula chakula kile walikuwa salama na hawa ni watu waliokuwa
wakijuana vizuri na wakiaminiana mwisho wa imani.

Nani anaweza kupenya nyumbani kwa Abdul akampa sumu Nyerere?
Nani?

Mama Daisy ndiye alikua akinihadithia alipomaliza aliinamisha kichwa
akasema, ''Mwanangu MohamedAbdul na Nyerere wametoka mbali
sana na walikuwa zaidi ya ndugu.''

Iko siku nitakileta hapa kisa cha sanduku la fedha la Abdul Sykes.


Kushoto: Dossa Aziz, Julius Nyerere, Abdul Sykes na Lawi Sijaona

Sunday, 6 August 2017Mubindi,
Suala la takwimu nchi petu baina ya Waislam na Wakristo ni jambo nyeti
sana na kwa hakika Afrika yote hili ni jambo linaloleta ubishani mkubwa
sana.

Wakati naandika kitabu cha Abdul Sykes ilifika mahali lazima hili suala
nilizungumze.

Naweka hapo chini kile nilichosema:

''According to the 1957 population census, Muslims outnumbered Christians at a ratio of three to two. This, at that time, meant that Tanzania was a leading Muslim nation South of the Sahara. But in the first post-independence census of 1967 the total figures for Tanzania Mainland were 32% Christian, 30% Muslim and 37% local belief (August H. Nimtz Jr, Islam and Politics in East Africa, University of Minneapolis, 1980, p.11). These figures show Pagans as a leading majority in Tanzania. The 1967 census has not been able to show the reasons for the sudden decrease of Muslim population nor the growth of animists amidst believers in the span of the last ten years.

This was the last population census showing religious distribution.

Unfortunately power sharing in the political system in Tanzania is very much skewed against Muslims, although it is known that the stability of any nation depends on proper balancing of these facts. Different sources provide different Muslim -Christian religious distribution figures. These conflicting figures are as a result of sensitivity of the issue. Among African countries with sizable population of Muslims and Christians, like Tanzania and Nigeria,[1] the inquiry as to which faith commands a leading majority, is a source of potential conflict and controversy. Tanzania is of no exception. D.B. Barret[2]gives figures which show Muslims as a minority in Tanzania. The Muslim population is purported to be 26%, Christian 45%, local belief 28%. Tanzania National Demographic Survey figures for 1973 put Muslims in Tanzania slightly above Christians at 40%, Christians 38.9% and local belief 21.1%. But according to Africa South of The Sahara, [3] Muslims in Tanzania are a leading majority at 60%. This figure has remained constant in all its publications since 1982. Since research by Tanzanian Muslims on Islam is scant or almost non-existent, the issue of Muslim population has yet to be tackled from an Islamic point of view. [4]

Distribution of authority and power sharing is a factor which should not have been a cause of conflict in independent African countries. Ironically this has become a point of controversy only under indigenous governments.

It is a sensitive issue because ethnicity, religious identity and clanship is an important factor in independent African states. Power distribution and numerical strength has also to be reflected in the sharing of political power along those lines.

During colonial rule, distribution of power under ethnicity and religious bias in Africa by colonising powers were not perceived as so serious a breach of trust by subjects as to warrant civil upheavals.

Fortunately tribalism is not pronounced in Tanzania, but religion has been a factor of discrimination since colonial days.''

[1] Ali A. Mazrui, ‘African Islam and Competitive Religion: Between Revivalism and Expansion’, in Third World Quarterly Vol. 10. No. 2 April, 1988, pp. 499-518.
[2] D.B.Barret, Frontier Situations for Evangelisation in Africa ,Nairobi, 1976.
[3] Africa South of The Sahara, Europa Publication, London, No. 20, 1991, p. 1027.
[4]The only conclusive Muslim research is by Dar es Salaam University Muslim Trustee (DUMT), see 'The Position of Muslims and Islam in Tanzania', in Al Haq International (Karachi) September/October 1992.

Bahati mbaya nimeandika haya katika Kiingereza lakini tunaweza tukafanya mjadala kwa Kiswahili.

Katika hayo niliyoweka hapo juu nimefuta kipengele kimoja kinachosema kuwa takwimu za sensa ya mwisho iliyokuwa na kipengele cha dini ''zilichezewa.''

Nimekifuta makusudi kwa kuwa ingawa ipo ''citation,'' nina hakika kitasababisha mapambano makali hapa jamvini.

Sasa turudi latika hizi takwimu za CIA.

Nilikuwa nafanya mhadhara Chuo Kikuu Cha Iowa, Marekani kuhusu ''Uislam
na Siasa Tanzania Historia ya TANU na Uhuru wa Tanganyika.''

Katika mhadhara ule nilieleza sababu za Waislam katika takriban miaka 20
iliyopita kuwa na maandamano na mapambano ya mara kwa mara na serikali.

Nikaeleza sababu kuu ni kuwa Waislam wamekuwa pembeni katika elimu na
hivyo kuwa pembeni katika kugawana madaraka ya kuendesha nchi.

Waislam walitaka hili liangaliwe na serikali kwani ipo harufu ya hujuma.

Katika kipindi cha maswali na majibu na ilipobaki kama dakika tatu hivi nihitimishe,
ndipo likaja swali hili lililokuwa na takwimu za CIA na muulizaji alikuwa profesa wa
historia akasema kuwa wakipatacho Waislam wa Tanzania hiyo ndiyo haki yao kwa
kuwa wao ni wachache, yaani ni ''minority.''

Hili swali naamini liliwekwa hadi mwisho kwa kuwa katika mazungumzo yale walitaabika sana ni historia ya uhuru niliyokuwa nawafunulia, historia ya wazalendo Waislam katika kupambana na ukoloni, historia ambayo kwao wao ilikuwa ngeni.

Wao walizoea mihadhara ya kuja na historia rasmi iliyomtaja Mwalimu Nyerere 
peke yake kuwa ndiyo aliyoikomboa Tanganyika kutoka kwa Waingereza.

Hawakutaka nitoke pale kichwa juu kifua mbele walitaka wanifedheheshe kwa hizi
takwimu za CIA zinazonyesha kuwa Tanzania ina Waislam wachache na mambo
yote ni shwari ila kwa vurugu hizi za, ''Waislam wa siasa kali.''

Historia yangu ilikuwa imewahuzunisha.

Katika hadhira ile alikuwapo Prof. James Giblin aliyafanya utafiti na kuandika kitabu
kuhusu Vita Vya Maji Maji.

Alikuwapo pia Prof. Michael Lofchie aliyeandika kitabu kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar, ''Revolution in Zanzibar,'' na hawa wote wameishi Tanzania na wanaijua vyema.

[​IMG]
Prof. Michael Lofchie

[​IMG]
Prof. James Giblin

Jibu langu kwao halikuwa kwangu mimi kugonganisha takwimu zangu kama zilivyo
katika kitabu cha Abdul Sykes, na takwimu zao za CIA, la hasha.

Mimi nilijibu swali lao kwa kuwauliza wao swali.

Niliwaambia kuwa naomba wanionyeshe nchi yoyote duniani katika historia yao
wananchi walio pungufu yaani, ''minority,'' walionyanyuka na silaha mikononi
kupambana na taifa lililoingia katika nchi yao kwa nia ya kuwatawala.

Nikawarejesha katika hitoria ya Vita Vya Maji Maji na kuwaambia wafanye rejea
na waangalie ni nani waliunda majeshi ya kupambana na Wajerumani.

Nikawakumbusha kisa cha Sultani Abdulrauf Songea Mbano wa Wangoni
alivyonyongwa na Wajerumani kwa kuongoza vita dhidi yao.

Nikawaambia wafanye tena rejea waangalie harakati za siasa za uhuru zilipoanza
baada ya Vita Vya Pili Vya Dunia (1938 - 1945) ni nani walikuwa mstari wa mbele
katika, ''nationalist politics,'' Tanganyika?

Kweli inawezekana adui aingie katika nchi bila ya ridhaa ya wenye nchi na ikawa
walionyanyuka kupinga uvamizi huu wakawa ni wale, ''minority?''

''Majority,'' ya wenye nchi wako wako wapi hadi mapambano ya kuikomboa nchi iwe
mikononi kwa ''minority,'' na katika Tanganyika iwe Waislamu?

Ukumbi wote ulikuwa kimya.

Maprofesa wa historia ya Afrika walikuwa wanajaribu bila shaka kutafuta mfano
utakaoweza kupambana na hoja yangu.

Hawakuweza kuupata.

Nchi zote duniani mapambano ya ukombozi huongozwa na wale waliokuwa, ''majority.''

Nikamaliza kwa kusema kuwa sina ugomvi na takwimu za CIA lakini Waislam wa
Tanzania wanaujua ukweli.

Palepale Jonathon Glassman bingwa wa African History kutoka Northwestern University,
Evanston Chicago akaniomba niende chuoni kwake tukafanye madahalo kama ule
tuliofanya pale Universty of Iowa.

Glassman amekaa sana Pangani na Tanga mjini wakati anafanya utafiti wake na
kaandika kitabu ''Feats and Riots,'' anaijua vizuri Tanzania.

Nilikubali mwaliko na nilizungumza Northwestern University, Ukumbi wa Eduardo
Mondlane
.